Aug 21, 2022 02:45 UTC
  • Wazayuni wajuta kumshinikiza Trump ajitoe katika makubaliano ya nyuklia JCPOA mwaka 2018

Wakuu wa masuala ya usalama wa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel wameonyesha majuto kwa hatua ya utawala huo ya kumshinikiza rais wa zamani wa Marekani Donald Trump ajitoe kwenye makubaliano ya nyuklia JCPOA mwaka 2018.

Ripoti iliyotolewa na chaneli ya televisheni ya utawala wa Kizayuni wa Israel ya KAN 11 kuhusu mazungumzo yanayohusiana na makubaliano ya nyuklia ya Vienna imeeleza kwamba, "viongozi wa masuala ya usalama wa Israel wanajuta; na sababu ni kuwa, baada ya Iran kupiga hatua kubwa katika mpango wake wa nyuklia hususan katika urutubishaji wa urani, hivi sasa nchi hiyo pamoja na madola makubwa wanaelekea kwenye mwafaka wa makubaliano yaleyale; na laiti kama Marekani isingejitoa kwenye makubaliano, Iran ingejizuia kupiga hatua hiyo".

Kwa mujibu wa ripoti ya televisheni ya KAN 11, wakuu wa masuala ya usalama wa Israel walidhihirisha majuto yao hayo katika kikao cha mashauriano kilichofanyika karibuni ambacho kilichohudhuriwa pia na waziri mkuu wa utawala huo haramu, Yair Lapid.

Trump alijitoa, Biden anadai anataka kurudi katika JCPOA

 

Televisheni hiyo ya Kizayuni imeongezea kwa kusema, Tel Aviv imezidisha mashinikizo yake kwa serikali ya Joe Biden kumtaka azingatie matakwa ya Israel katika mapatano yoyote yale ya nyuklia na Iran, hususan kuhusiana na kubakishwa mafaili ya uchunguzi dhidi ya Iran katika Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA na kurefushwa muda wa kufanyiwa ukaguzi vituo vyake vya nyuklia.

Kufuatia kuongezeka harakati za viongozi wa utawala wa Kizayuni wa Israel za kuingilia mazungumzo ya nyuklia ya mjini Vienna, msemaji wa wizara ya mambo ya nje  ya Marekani Ned Price ametangaza kuwa, nchi hiyo na mshirika wake Israel wanatofautiana kimbinu kuhusu makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.../

Tags