Marekani yapinga ombi la Ukraine la kuwanyima visa raia wa Russia
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani amepinga ombi la Ukraine la kuwanyima visa raia wa Russia.
Mashinikizo ya kidiplomasia, vitisho na vikwazo vya Magharibi dhidi ya Russia vinaendelea sambamba na kuendelea vita na mapigano nchini Ukraine. Moscow nayo lakini haikutulia kimya, bali imekuwa ikijibu vikwazo na mashinikizo hayo ya madola ya Magharibi dhidi yake kulingana na inavyoona inafaa zaidi.
Shirika la habari la IRNA limemnukuu msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani akisema mbele ya waandishi wa habari kwamba, serikali ya Joe Biden tayari ilishachukua hatua za kubana utoaji visa kwa viongozi wa Kremlin hivyo hakuna haja ya kuchukuliwa hatua nyingine kama hizo.
Amesema, hivi sasa Marekani imejikita kwenye kuwatafuta na kuwatambua watu ambao wanafanikisha operesheni maalumu za kijeshi za Russia huko Ukraine.
Afisa huyo wa ngazi za juu wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani aidha amedai kuwa, Washington haitaki kuwafungia njia wakimbizi na wapinzani wa serikali ya Russia ambao amedai wanakabiliwa na uvunjaji wa haki za binadamu.
Kabla ya hapo, rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy alikuwa ameitaka Marekani iwanyime visa raia wote wa Russia bila ya kujali wapinzani na waungaji mkono wa vita vya Ukraine. Rais huyo aidha mara kwa mara amekuwa akizitaka nchi za Ulaya kuwawekea vikwazo raia wote tu wa Russia popote walipo ili kuzuia nchi za Ulaya kuwa vituo vya biashara na manunuzi kwa matajiri wa Kirusi.