Putin aongeza idadi ya wanajeshi wa Russia, wapindukia milioni 1
Rais Vladimir Putin wa Russia amesaini dikrii ya kuongeza idadi ya wanajeshi wa nchi hiyo, huku operesheni maalumu ya kijeshi ya Moscow dhidi ya Ukraine ikiingia mwezi wa saba.
Dikrii hiyo iliyochapishwa katika tovuti ya Ikulu ya Kremlin inasema kuwa, jeshi la Russia linaongeza idadi ya vikosi vyake kwa askari 137,000, na sasa litakuwa na jumla ya wanajeshi milioni 1.15.
Kwa mujibu wa dikrii hiyo iliyosainiwa jana Alkhamisi na Rais Putin, jeshi la Russia litakuwa na askari zaidi ya milioni mbili kufikia Januari mwaka ujao 2023.
Mwaka 2017, Rais Putin alisema idadi ya askari wa nchi hiyo ilikuwa milioni 1.9, wakiwemo wanajeshi zaidi ya milioni moja wa vikosi mbalimbali vya nchi hiyo.
Ingawaje dikrii iliyosainiwa Alkhamisi haijaeleza sababu ya Moscow kuongeza idadi ya wanajeshi wake, lakini hatua hiyo imekuja wakati huu ambapo vikosi vya Russia vinafanya jitihada za kudhibiti maeneo ya mashariki ya Ukraine.
Moscow ilianzisha operesheni maalumu nchini Ukraine mnamo Februari 24, kwa lengo la kuizuia nchi hiyo isiendelee kujitanua kuelekea upande wa mashariki, kwa madhara ya usalama wa Russia.