Russia yatishia tena kutumia silaha za nyuklia endapo uwepo wake utahatarishwa
Sep 04, 2022 06:33 UTC
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesema upo uwezekano wa nchi hiyo kutumia silaha za nyuklia endapo uwepo wake utahatarishwa.
Kwa mujibu wa chaneli ya televisheni ya Russia al Yawm, Sergei Ryabkov, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesisitiza kuwa, kwa kuzingatia mwongozo wake wa kijeshi, Moscow iko tayari kutumia silaha za nyuklia ikiwa itakabiliwa na tishio linalohatarisha uwepo wake.
Aidha Ryabkov amesema, kiwango cha uingiliaji unaofanywa na Marekani katika vita vya Ukraine na misaada ya kifedha na silaha inayolipatia mtawalia jeshi la nchi hiyo inazidi kuongezeka, jambo ambalo ni hatari, na tayari Russia imeshaionya Marekani mara kadhaa kuhusu madhara ya hatua yake hiyo.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia ameongeza kuwa, Marekani inafanya kila njia kuishinikiza Moscow kwa kila upande na kwa kisingizio cha vita vya Ukraine, lakini Russia haitishiki kwa hatua hizo na wala hazitaifanya ipoteze umakini wake.
Tangu vilipoanza vita nchini Ukraine hadi sasa, nchi za Magharibi na hasa Marekani, zimezidisha mashinikizo ya vikwazo dhidi ya Russia sambamba na kuipatia Ukraine aina mbalimbali ya silaha nyepesi na nzito, zana za kivita na mafuta, hatua ambazo sio tu hazijasaidia kumaliza mapigano, bali zimekoleza zaidi moto wa vita nchini humo.
Russia imetahadharisha mara kadhaa kuwa hatua ya Magharibi ya kuipelekea silaha Ukraine itarefusha mzozo tu katika nchi hiyo na kusababisha matokeo yasiyotabirika.../
Tags