Sep 10, 2022 02:20 UTC
  • Korea Kaskazini: Hatutasalimisha silaha zetu za nyuklia

Kiongozi wa Korea Kaskazini amesema kamwe Pyongyang haitasalimisha silaha zake za nyuklia au kutumia suala la kuharibu silaha hizo za maangamizi kujadiliana na Marekani.

 Shirika rasmi la habari la Korea Kaskazini (KCNA) liliripoti habari hiyo jana Ijumaa, likimnukuu Kim Jong-un, kiongozi wa nchi hiyo aliyesisitiza kuwa, Marekani inafanya jitihada za kudhoofisha mfumo wa ulinzi wa nchi hiyo, lakini kamwe Pyongyang haitasambaratisha silaha zake za nyuklia.

Kim amepongeza hatua ya Bunge la nchi hiyo ya kupasisha sheria mpya ya kusimamia silaha za nyuklia za nchi hiyo na kueleza kuwa, "Kuhalalishwa silaha za nyuklia kwa misingi ya sheria kuna umuhimu mkubwa katika kuchora mstari; sasa hatutafanya mijadala kuhusu silaha hizo." 

Kiongozi wa Korea Kaskazini ameikosoa vikali Marekani kwa kuliwekea vikwazo taifa hilo ili kulishinikiza liharibu silaha zake za nyuklia na kusisitiza kuwa, mahesabu hayo ghalati ya Washington katu hayatafanikiwa hata baada ya miaka 100.

Makombora ya nyuklia ya Korea Kaskazini

Washington imekuwa ikiishinikiza Korea Kaskazini iharibu silaha zake za nyuklia katika hali ambayo, takwimu rasmi zilizotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani (Pentagon) mwaka jana zilieleza kuwa, nchi hiyo imerundika vichwa 3,750 vya nyuklia kwenye maghala yake ya silaha.

Hata hivyo hakuna uhakika ni kwa kiwango gani zinaendana na ukweli halisi kuhusu silaha za nyuklia zilizohifadhiwa kwenye maghala ya silaha hizo nchini humo.

Tags