Korea Kaskazini, dola lenye nguvu za nyuklia
(last modified Mon, 12 Sep 2022 02:17:57 GMT )
Sep 12, 2022 02:17 UTC
  • Korea Kaskazini, dola lenye nguvu za nyuklia

Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong-un ametia saini sheria ambayo kwa mujibu wake nchi hiyo sasa inatambuliwa rasmi kuwa ni dola lenye nguvu za kijeshi za nyuklia.

Bunge la Korea Kaskazini nalo limepasisha sheria inayofanana na hiyo, ya kuitangaza rasmi Korea Kaskazini kuwa ni dola lenye nguvu za atomiki. 

Aidha Kiongozi wa Korea Kaskazini amesisitiza kuwa, nchi yake kamwe haitoachana na silaha zake za nyuklia kwani kumiliki silaha hizo ni udharura wa usalama wa kitaifa wa nchi hiyo.

Hatua hiyo ya Kiongozi wa Korea Kaskazini na bunge la nchi hiyo ni majibu ya wazi na makali kwa ombi la hivi karibuni la serikali ya Korea Kusini ambayo imeitaka Pyongyang ikabidhi silaha zake za nyuklia na iachane kabisa na siasa zake za kumiliki silaha hizo ili Korea Kusini iweze kufungua miradi yake ya maendeleo na kuwekeza huko Korea Kaskazini. 

Tab'an hii si mara ya kwanza kwa serikali mbalimbali za Korea Kusini kutoa pendekezo kama hilo kwa jirani yao Korea Kaskazini.

Kiongozi wa Korea Kaskazini akikagua nguvu za kijeshi za nchi hiyo

Katika makala yake maalumu, gazeti la Washington Post limetoa uchambuzi kuhusu Korea mbili likisema kuwa, mashinikizo ya kiwango cha juu ya Ikulu ya Marekani (White House) dhidi ya Korea Kaskazini yameshindwa kabisa. Gazeti hilo limesisitiza kuwa, Korea Kaskazini imefikia kiwango cha juu ya kujiamini kiasi kwamba hivi sasa ni dola lenye nguvu za nyuklia na linatumia silaha hizo kuzizuia nchi nyingine hata zisifikirie kuivamia kijeshi nchi hiyo. Korea Kaskazini inazihesabu siasa za Marekani kwenye eneo hilo kuwa ni hatari kwa usalama wake. Ni kwa sababu hiyo ndio maana Pyongyang inalazimika kujiimarisha mno kijeshi ikiwa ni pamoja na kujimarisha kwa makombora yenye uwezo wa kubeba vichwa vya nyuklia.

Hii ni katika hali ambayo Marekani imeiwekea Korea Kaskazini vikwazo vikali mno, lakini vikwazo hivyo vimeshindwa kuipa Marekani ilichokuwa inatafuta. Kitendo cha kibeberu cha Marekani cha kupeleka manuwari zake za kivita katika maji yanayopakana na Korea Kaskazini na China na kitendo chake cha kuweka mfumo wa makombora ya kisasa huko Korea Kusini ni miongoni mwa hatua za kiistikbari za Marekani ambazo zinahesabiwa na Korea Kaskazini kuwa ni tishio kubwa kwa usalama wake wa kitaifa.

Hatua ya hivi sasa ya Korea Kaskazini ya kutangaza rasmi kuwa nchi hiyo ni dola lenye nguvu za silaha za atomiki, imefunga milango yote ya kuzungumzia silaha za nyuklia za Pyongyang. Mara kwa mara Marekani imekuwa ikitaka nguvu za atomiki za Korea Kaskazini ziwekwe mezani kujadiliwa, lakini hivi sasa Pyongyang imetangaza waziwazi kwamba, silaha zake za atomikki si kitu kabisa cha kujadiliwa na inabidi jamii ya kimataifa na dunia nzima ikiwemo Marekani itambue kuwa Korea Kaskazini sasa ni dola rasmi la nyuklia

Korea Kaskazini imejiimarisha vilivyo kwa makombora kukabiliana na vitivyo vya kila upande

 

Hossein Ahan, mtaalamu wa masuala ya kimataifa anasema: Korea imegawika mara mbili. Upande mmoja ni ule uliopiga hatua kubwa za kiviwanda yaani Korea Kusini na upande wa pili ni uliojiimarisha vilivyo kinyuklia yaani Korea Kaskazini. Upande wa kusini wa Korea unafanya juhudi za kutumia nguvu zake za kiviwanda kuushawishi upande wa kaskazini uachane na silaha za nyuklia ili uweze kuwa kama upande wa kusini wenye maendeleo ya viwanda, lakini hakuna matumaini hata kidogo kuwa Korea Kaskazini inaweza kuachana na nguvu zake za nyuklia.

Marekani nayo inaendeleza vitisho vyake kwa Korea Kaskazini suala ambalo si tu linahatarisha usalama wa nchi hiyo, bali linautia hatarini pia usalama wa eneo zima la Asia Mashariki. Korea Kaskazini nayo haikubakishiwa chaguo lolote jingine isipokuwa kujiimarisha kisilaha ili kukabiliana na vitisho vya kila kona vinavyoikabili nchi hiyo.

Wakati huo huo Kiongozi wa Korea Kaskazini ametia saini sheria ya kuitangaza rasmi nchi hiyo kuwa ni dola la silaha za nyuklia baada ya kupasishwa na Bunge, ni tangazo la wazi kabisa kwamba Pyongyang haitaki mchezo katika kadhia nzima ya silaha zake za nyuklia.

Tags