Iran na IAEA zaafikiana kurejesha ushirikiano; Araghchi aonya
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i130628-iran_na_iaea_zaafikiana_kurejesha_ushirikiano_araghchi_aonya
Iran na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) zimefikia makubaliano yenye lengo la kuandaa njia ya kurejesha ushirikiano kati ya pande hizo mbili.
(last modified 2025-09-10T06:40:53+00:00 )
Sep 10, 2025 06:40 UTC
  • Iran na IAEA zaafikiana kurejesha ushirikiano; Araghchi aonya

Iran na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) zimefikia makubaliano yenye lengo la kuandaa njia ya kurejesha ushirikiano kati ya pande hizo mbili.

Makubaliano hayo yalitiwa saini baina ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi na Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo la Umoja wa Mataifa la kusimamia masuala ya nyuklia, Rafael Grossi jana Jumanne mjini Cairo. Misri ni mwenyeji wa mazungumzo kati ya pande hizo mbili.

Makubaliano hayo yamekuja baada ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kusitisha ushirikiano na wakala huo kufuatia mashambulizi ya Israel na Marekani dhidi ya vituo muhimu vya nyuklia vya Iran mwezi Juni.

Tehran ilisimamisha ushirikiano huo kwa mujibu wa sheria iliyopasishwa na Majlis ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran), kupinga azimio dhidi ya Iran lililoidhinishwa na IAEA chini ya mashinikizo ya Magharibi na Israel; azimio lililotumiwa na wavamizi kujaribu kuhalalisha mashambulizi hayo.

Akizungumza pambozini mwa Grossi wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliofuatia kuidhinishwa kwa makubaliano hayo, mwanadiplomasia huyo mkuu wa Iran ameyataja kuwa ni kilele cha mazungumzo ya kutimiza "maelewano ya jinsi majukumu ya ulinzi ya Iran yatatekelezwa" kwa kuzingatia matukio yanayotokana na uchokozi huo usio halali.

Ameongeza kuwa, makubaliano hayo yanahakikisha haki zisizoweza kuondolewa za Tehran kwa shughuli za amani za nishati ya nyuklia chini ya Mkataba wa Kuzuia Uzalishaji na Uenezaji wa Silaha za Nyuklia (NPT), wakati pia ukizingatia mahitaji ya kiufundi na uthibitishaji wa IAEA.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza kuwa, "Ujumbe uko wazi: Jamhuri ya Kiislamu haitakubali kamwe kuweka hatarini mamlaka yake ya kujitawala, haki zake, au usalama wake."