Sep 13, 2022 05:26 UTC
  • Ombi la kuilazimisha Marekani itimize wajibu wake wa uenyeji wa Umoja wa Mataifa

Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesema katika mahojiano kwamba Marekani na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres wana wajibu wa kuhakikisha ushiriki wa wawakilishi wote wa nchi wanachama katika mikutano ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa unatimia.

Akikumbusha kwamba Marekani bado haijatoa viza kwa ujumbe wa Moscow unaotazamiwa kushiriki vikao vya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Sergey Lavrov, Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesema: Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ana wajibu wa kudhamini ushiriki wa wajumbe wote wa nchi wanachama. Ana wajibu wa kuhakikisha kutimia ushiriki wa wajumbe wote katika shughuli za Umoja wa Mataifa, ikiwa ni pamoja na mikutano ya Baraza Kuu la umoja huo.

Vassily Nebenzia, Mwakilishi wa Kudumu wa Rusia katika Umoja wa Mataifa, pia alimwomba Guterres wiki iliyopita ahakikishe serikali ya Marekani inatoa viza kwa wakati kwa ujumbe wa Russia na wanahabari wanaofuatana nao wanaokwenda kushiriki vikao vya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Marekani ina historia ndefu na mbaya sana ya kutotoa huduma za uenyeji wa Umoja wa Mataifa katika jiji la New York, hasa kuhusu utoaji visa kwa maafisa na wanadiplomasia wanaohudumu katika umoja huo, na wakati huo huo kuwawekea vikwazo vya kila aina wanadiplomasia wa nchi pinzani au shindani wanaoazimia kutembelea maeneo tofauti ya mji huo.

Sergey Lavrov, Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia

Suala hilo limechochea mara kwa mara malalamiko ya nchi kama vile Russia, Iran, Cuba na Venezuela ambazo daima zimekuwa zikikabiliwa na vikwazo vya serikali mbalimbali za Marekani zinazozuia maafisa na wanadiplomasia wao kushiriki mikutano ya Umoja wa Mataifa hususan vikao vya Baraza Kuu la umoja huo.  Mwezi Septemba 2021, wawakilishi wa kudumu wa Iran, Russia, Syria, Cuba, Venezuela na Nicaragua katika barua ya pamoja kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa walipinga vikali hatua ya Marekani ya kukiuka makubaliano ya makao makuu ya Umoja wa Mataifa ya 1947 na kutaka suala hilo litafutiwe ufumbuzi wa kudumu mara moja. Barua hiyo ilisisitiza kwamba Marekani, ikiwa nchi mwenyeji, bado haitoi visa kwa wakati kwa ajili ya wawakilishi wa nchi hizo 6 kushiriki katika shughuli za Umoja wa Mataifa au kufanya kazi katika balozi zao za kudumu, na kwamba ilikuwa inawawekea vikwazo vya usafiri na matembezi katika Umoja wa Mataifa.

Kwa kutilia maanani kuwa Marekani ni mwenyeji wa makao makuu ya Umoja wa Mataifa, imekuwa ikitumia vibaya nafasi hiyo kuwanyima viza wanadiplomasia na maafisa wakuu wa nchi zinazopinga siasa zake za ubabe ulimwenguni. Hasa katika kipindi cha urais wa Donald Trump, misimamo mikali ilichukuliwa dhidi ya wanadiplomasia na maafisa wakuu wa nchi hizo kwa shabaha ya kuzuia uwepo wao au kuwawekea vizuizi katika harakati zao mjini Washington. Lengo la hatua hizo za Washington ni kushadidisha mashinikizo dhidi ya nchi hizo, na pia kuzuia uwepo wa wanadiplomasia wao na kuwawekea kila aina ya vikwazo ili kuwazuia kutekeleza majukumu yao. Akizungumzia vikwazo hivyo vya Marekani, Mohammad Reza Marandi mtaalamu wa masuala ya kisiasa anasema: Vikwazo hivi ni kinyume na ahadi ambazo Marekani imezitoa kuhusu Umoja wa Mataifa. Hii ni katika hali ambayo Umoja wa Mataifa hauko chini ya udhibiti wa Marekani, bali imepewa tu fursa ya uwenyeji wa taasisi hiyo muhimu ya kimataifa.

Kabla ya hapo na kutokana na misimamo ya kiuadui ya utawala wa Trump dhidi ya wanadiplomasia wa Iran na uwakilishi wa kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa, na pia kuwekewa vikwazo mbalimbali wanadiplomasia wa Russia wanaoazimia kwenda Marekani kwa ajili ya kushiriki vikao vya Umoja wa Mataifa, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mnamo tarehe 18 Disemba 2019 lilipitisha azimio kwa kauli moja, likilaani hatua ya Marekani ya kutotoa visa kwa wanadiplomasia wa Russia na kuitaka serikali ya Washington kuwaondolea wanadiplomasia wa Iran vizuizi vya kuingia nchini humo.

Kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa

Kwa mujibu wa makubaliano ya 1947 kati ya Umoja wa Mataifa na Marekani, nchi hiyo ikiwa mwenyeji wa makao makuu ya Umoja wa Mataifa, haipaswi kuwawekea vikwazo vya usafari maafisa wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa wanaopanga kushiriki katika shughuli za taasisi hiyo wala kuwawekea vizingiti wanapokuwa njiani kutoka makao hayo kuelekea ofisi zao za uwakilishi wa kudumu au kinyume chake. Kutolewa azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa katika muktadha huo kunaonyesha wazi kwamba siasa za mabavu za Washington na vikwazo vyake dhidi ya maafisa na wanadiplomasia wa nchi zinazopinga au kushindana na Marekani katika uga wa kimataifa ni jambo lisilokubalika kabisa kisheria. Licha ya azimio hilo na malalamiko ya mara kwa mara ya nch wanachama wa Umoja wa Matifa lakini bado serikali ya Marekani inadumisha siasa hizo za ubabe na udhalilishaji dhidi ya wanadiloamasia wa nchi pinzani, siasa ambazo zingalia zinatekelezwa pia na serikali ya hivi sasa ya Rais Joe Biden. Washington hadi sasa imekataa kutoa visa kwa Sergay Larov na ujumbe anaopasa kuandamana nao kwa ajili ya kushiriki vikao vya kila mwaka vya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Tags