Kwa nini Marekani imejikita sana katika kuunga mkono ghasia nchini Iran
Karine Jean-Pierre Msemaji wa White House ameashiria namna Marekani ilivyojikika pakubwa katika machafuko na ghasia hapa nchini na kueleza kuwa: hata kama serikali ya Biden inaamini kuwa diplomasia ni njia bora zaidi ya kuizuia Iran kumiliki silaha za nyuklia lakini sasa Washington imejikita katika kuunga mkono ghasia na fujo nchini Iran.
Baadhi ya mikoa ya Iran katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita imekumbwa na ghasia na fujo ambazo zimejiri kwa uungaji mkono wa baadhi ya nchi za kigeni ikiwemo Marekani na nchi kadhaa za Ulaya. Viongozi wa Marekani wamejitokeza hadharani na kutangaza wazi kuunga mkono ghasia hizo hapa nchini. Mbali na matamshi hayo ya msemaji wa ikulu ya Marekani (White House), Ned Price Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya nchi hiyo pia amekiri kuwa serikali ya Marekani imeelekeza fikra zake zote katika ghasia na fujo zinazoendelea nchini hapa na kuituhumu Tehran kwamba haiko tayari kufikia mapatano. Rais Joe Biden wa Marekani pia amekiri kuwa nchi hiyo inaunga mkono kuendelea fujo na ghasia nchini Iran na kwamba eti wako pamoja na wananchi na wanawake shujaa wa Iran."
Inaonekana kuwa sababu ya kwanza inayoisukuma Washington kuunga mkono waziwazi ghasia na machafuko hapa nchini ni hii kwamba katika miaka ya karibuni Marekani imefanya jitihada kubwa kuuangusha mfumo wa kisiasa nchini Iran hata hivyo jitihada zake hizo zimegonga mwamba. Marekani aidha inaendeleza na kufuatilia sera za mashinikizo ya kiwango cha juu za serikali iliyopita ili kuipindua Jamhuri ya Kiislamu; kwani hata John Bolton Mshauri wa zamani wa Usalama wa Taifa wa Marekani aliwahi kusema kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitashuhudia kutimia mwaka wa arubaini wa maadhimisho ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Marekani imejikita katika kuzidisha upinzani na kuibua fujo nchini Iran baada ya kufeli kwa sera zake za mashinikizo ya kiwango cha juu dhidi ya Tehran. Hata kama hivi sasa viongozi wa Marekani wanafahamu vyema kwamba ghasia na fujo za karibuni haziwezi kuiangusha serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wala kulinganishwa na ghasia zilizowahi kushuhudiwa hapa nchini huko nyuma lakini wameamua kuunga mkono machafuko hayo ili kuyazuia yasisimame na hivyo kuandaa mazingira ya kudumishwa ghasia hizo nchini. Washington inadhani kuwa kuendelea kwa machafuko hayo tajwa kunaweza kuandaa uwanja wa kuidhoofisha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na hivyo kupata mwanya wa kuingilia masuala yake ya ndani; kama alivyobainisha hilo pia Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi katika hotuba yake ya karibuni kwamba, lengo la adui ni kuishughulisha serikali na maafisa wake katika machafuko ya ndani.
Sababu ya pili ya uungaji mkono wa Marekani kwa ghasia na fujo nchini Iran, ni kupata ridhaa ya utawala wa Kizayuni na utawala wa Aal Saud. Tel Aviv na Riyadh zinaamini kuwa serikali mpya ya Marekani haijaiwekea mashinikizo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kama ilivyokuwa serikali iliyopita ya nchi hiyo chini ya uongozi wa Rais Donald Trump. Ingawa kuna sababu nyingi za Washington kujiweka mbali kidogo kwa sasa na Riyadh na Tel Aviv lakini serikali ya Marekani inayoongozwa na chama cha Democrat imeamua kuwaunga mkono wafanyafujo nchini Iran ambao pia wanaungwa mkono na Riyadh na Tel Aviv katika jitihada za kujaribu kuzidisha kuungwa mkono chama hicho kutoka nje wakati huu wa kukaribia uchaguzi mdogo wa Kongresi ya nchi hiyo.
Sababu ya tatu na muhimu zaidi inahusiana na mazungumzo ya nyuklia. Mazungumzo hayo yalisitishwa tokea mwanzoni mwa mwezi Septemba mwaka huu baada ya Marekani kupinga matakwa yanayohusiana na haki za Iran ikiwemo haki ya Tehran kupatiwa dhamana ya kudumu na kufungwa kadhia ya masuala ya usalama katika wakala wa IAEA. Wiki kadhaa zilizopita na kufuatia Iran kuendelea kushinikiza juu ya ulazima wa kudhaminiwa matakwa yake kulijitokeza baadhi ya ishara kuhusu kukaribia kufikiwa mapatano hata hivyo ghasia na fujo zilizoshuhudiwa hapa nchini hivi karibuni zimetoa matumaini kwa White House kwamba kupitia hatua yake ya kuiwekea Tehran vikwazo vipya na kuwaunga mkono wafanya fujo inaweza kuiainishia Iran masharti ili itazame upya matakwa yake hayo.
Vikwazo kama walivyokiri shakhsia kama Richard Nephew ambaye ni mmoja wa wabunifu wa sera za vikwazo vya Marekani vimewapelekea viongozi wa serikali kubadili mahesabu yao kupitia kuiibua malalamiko ya umma na kutoa vitisho vya kuipindua serikali badala ya pande za Magharibi kustafidi na vikwazo hivyo kama karata ya kuweza kufikia muafaka katika mazungumzo. Ni wazi kuwa, kwa kuunga mkono machafuko na kuendeleza mashinikizo ya kijamii nchini Iran Marekani inafanya kila iwezalo kuwalazimisha viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wakubali mapatano ya nyuklia hasa bila ya kupatiwa ufumbuzi masuala ya kiusalama na kiulinzi.