Wanaopinga 'Brexit' waandamana wakitaka UK ijiunge tena na EU
(last modified Mon, 24 Oct 2022 04:00:55 GMT )
Oct 24, 2022 04:00 UTC
  • Wanaopinga 'Brexit' waandamana wakitaka UK ijiunge tena na EU

Makumi ya maelfu ya watu wamefanya maandamano katika mji mkuu wa Uingereza, London wakishinikiza nchi hiyo irejee katika Umoja wa Ulaya.

Waandamanaji hao waliokusanyika kutoka pembe zote za Uingereza, walifanya maandamano kuanzia barabara ya Park Lane hadi Medani ya Bunge jijini London, huku wakisisitiza kuwa, hatua ya UK kujiondoa EU (Brexit) imeisababishia nchi hiyo madhara mengi.

Waandamanaji hao walionekana wakipeperusha bendera za Umoja wa Ulaya huku baadhi wakiwa wamebeba mabango yenye jumbe zisemazo "Brexit kamwe isingefanikiwa' na 'Ni wakati wa kujiunga upya na EU.'

Aidha wananchi hao wa Uingereza wametumia jukwaa la maandamano hayo kulalamikia mfumko wa bei na gharama ya juu ya maisha inayowasakama, pamoja na mgogoro wa nishati.

Mmoja wa waandamanaji kwa jina la Joshua Allotey ambaye amekuwa akipinga Brexit tokea mwaka 2019, amenukuliwa na vyombo vya habari akisema, "Hapo baadaye katika utekelezwaji wa Brexit, hatutaweza kuuza au kununua (bidhaa) kutoka Ulaya."

Naye Oliver Jackson, mfanyakazi wa kampuni ya Dorset amesisitiza kuwa, Brexit imekuwa kifo cha taratibu ambacho kimekuwa kikiifyonza Uingereza kwa miaka mingi sasa. Mwanzoni mwa 2020, Uingereza ilijiondoa katika Umoja wa Ulaya, baada ya kupita takribani miongo minne ya kuweko katika umoja huo.

Maandamano hayo yamejiri wakati huu ambapo Uingereza inakabiliwa pia na mgogoro wa kisiasa. Siku chache zilizopita, Waziri Mkuu wa Uingereza, Liz Truss alijiuzulu wadhifa wake huo baada ya kuushikilia kwa siku 45 tu. Amekuwa akikabiliwa na mashinikizo makubwa kutoka ndani ya chama cha kihafidhina kufuatia sera ya kiuchumi ambayo imekosolewa sana.

 

Tags