Wamarekani wana hofu ya kuibuka ghasia baada ya uchaguzi
Utafiti mpya umeonesha kuwa, akthari ya wananchi wa Marekani wana wasiwasi wa kuibuka ghasia na machafuko ya kisiasa baada ya uchaguzi wa katikati ya muhula unaotazamiwa kufanyika karibuni hivi.
Matokeo ya utafiti huo yanaonesha kuwa, Wamarekani 9 kati ya kila Wamarekani 10 wanahofia kuzuka ghasia za baada ya uchaguzi wa katikati ya muhula utakaofanyika Jumanne ijayo ya Novemba 8.
Utafiti huo umebainisha kuwa, thuluthi moja ya Wamarekani, wawe wafuasi wa chama cha Republican au Democrat wanaunga mkono na kuhalalisha ghasia hizo za kisiasa.
Utafiti huo, kwa mujibu wa televisheni ya Press TV ya Iran, umefichua kuwa, vitisho dhidi ya wajumbe wa Kongresi ya Marekani vimeongezeka mara kumi zaidi ya ilivyokuwa miaka mitano iliyopita.
Ikumbukwe kuwa, kikao cha Kongresi ya Marekani ambacho kilifanyika kwa lengo la kupasisha ushindi wa uchaguzi wa rais wa Novemba 3, 2020 huko Marekani kilikabiliwa na shambulio la wafuasi wa aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Donald Trump na kusimama kwa masaa kadhaa.
Watu wasiopungua watano wakiwemo maafisa usalama wa nchi hiyo waliuawa katika shambulio hilo la kutisha, huku wengine kadhaa wakijeruhiwa. Weledi wa mambo wanasema shambulizi hilo dhidi ya jengo la Kongresi tarehe 6 Januari 2021 ulikuwa uasi uliochochewa na Donald Trump, na ilikuwa hujuma dhidi ya Kongresi, Katiba na demokrasia.
Trump amewahi kusema kuwa, iwapo atagombea na kushinda urais katika uchaguzi wa mwaka 2024, atawasamehe na kuagiza kuachiwa huru watenda jinai waliohusika na shambulizi hilo dhidi ya jengo la Kongresi lililofanywa na wafuasi wake.