Dec 03, 2022 02:23 UTC
  • Ombi la Ulaya kwa China, mshaurini Putin asitishe vita Ukraine

Charles Michel, Rais wa Baraza la Ulaya, amekutana na kuzungumza na Rais Xi Jinping katika ziara yake rasmi nchini China. Katika mkutano huu, Michel alimwomba Xi kutumia ushawishi wa Beijing kwa Russia ili kusitisha vita nchini Ukraine.

Ombi hili la afisa wa juu zaidi wa Ulaya kwa Rais wa China linaonyesha kufeli kwa nchi za Magharibi katika kuihami Ukraine dhidi ya Russia. Ulaya pamoja na Marekani, wametumia nyezo zao zote hasa vikwazo vya pande zote dhidi ya Russia katika mgogoro wa Ukraine ili kuishinda Moscow katika mgogoro huo, lakini safari ya Rais wa Baraza la Ulaya nchini China na ombi lake kwa Beijng kutumia ushawishi wake kwa ajili ya kusimamisha vita huko Ukraine ni sawa na kukiri nchi za Magharibi kwamba zimefeli na kushindwa mkabala wa Russia.

Konstantin Vorontsov, mtaalamu wa masuala ya kimataifa wa Russia, anasema kuhusu jambo hili kwamba: "Magharibi imetoa kila kitu hata aina mbalimbali za satelaiti zake kwa Ukraine. Huu ni mchakato hatari sana ambao umeripotiwa kwa Umoja wa Mataifa." 

Sambamba na safari ya Charles Michel nchini China, ndege za kivita za nchi hiyo na Russia zilifanya mazoezi ya kupaa kwa pamoja, jambo ambalo limetajwa kuwa ni aina fulani ya kutunisha misuli na kuonesha muungano na umoja wa Beijing na Moscow dhidi ya madola ya Magharibi. Korea Kusini imetangaza kuwa anga yake imekiukwa; hata hivyo Russia imekanusha madai hayo na kutangaza kuwa, hakuna anga ya nchi yoyote iliyokiukwa.

Ndege za kivita za China na Russia

Ijapokuwa hadi sasa Russia na China hazijazungumzia lolote kuhusu muungano wa kijeshi baina ya pande hizo mbili, lakini utekelezaji wa baadhi ya mipango ya kijeshi kati ya nchi mbili hizo unaonyesha kuwa, zinajiandaa kwa tishio lolote la Jumuiya ya Kijeshi ya Nchi za Magharibi (NATO). Kwa sababu, NATO imedhamiria hasa kupanua eneo lake la kijiografia upande wa Masharikki, na mgogoro wa Ukraine ulisababishwa na msisitizo wa Marekani wa kupewa uanachama Ukraine katika jumuiya ya NATO, jambo ambalo Russia inalitambua kuwa ni tishio kwa usalama wake.

Ali Bigdeli, mtaalamu wa masuala ya kimataifa, anasema kuhusu suala hili kwamba: "Russia inahisi kutishiwa sana na upanuzi wa NATO kwenye mipaka yake; Uchina pia ina hali kama hiyo katika maji ya Bahari ya Kusini, kwa sababu ya uwepo wa meli za kivita za Marekani katika eneo hilo. Kwa sababu hiyo Moscow na Beijing zinakabiliana na vitisho vya pamoja na zinajiandaa kwa hali yoyote ile inayoweza kujitokeza."

Alaa kulli hal, safari ya Charles Michel nchini China, wakati Ulaya ikelekea kwenye msimu wa baridi kali, inaonesha udhaifu mkubwa wa nchi za bara hilo mbele ya hali ya kuendelea mgogoro wa Ukraine na athari zake mbaya kwa mahitaji ya nishati, suala ambalo limechochea maoni ya umma na watu wa Ulaya dhidi ya sera za misaada ya nchi za Magharibi kwa Ukraine ambazo zimezidisha mgogoro wa uchumi barani Ulaya. Hii ina maana kwamba, maoni ya wananchi barani Ulaya yanautambua mgogoro wa Ukraine kuwa ni mtego wa Washington kwa nchi za bara hilo, ambapo kwa kuzitumbukiza pande hizo mbili kwenye vita, sasa Marekani imeiweka Ulaya katika hali ngumu ya vikwazo katika maeneo tofauti na kuvurugika hali ya maisha ya watu wa bara hilo.

Vita vya Ukraine

Kwa sababu hiyo, mkuu wa Baraza la Ulaya amelazimika kufanya safari huko China na kuiomba nchi hiyo itumie ushawishi wake kusitisha vita nchini Ukraine. Inawezekana pia kwamba nchi za Ulaya hazikudhani kuwa vita hivyo vitaendelea kwa kipindi kirefu, na walikuwa wakamini kwamba mgogoro wa Ukraine ungesababisha machafuko nchini Russia dhidi ya Rais Vladimir Putin. Hata hivyo, usimamizi makini wa Rais Putin wa mgogoro wa Ukraine umerejesha mishale wa mgogoro huo kwa nchi za Magharibi, hasa nchi za Ulaya, ambazo zimejikuta katika hali ngumu ya kushawishi maoni yao ya umma kuendelea kutoa misaada kwa serikali ya Ukraine.

Tags