Wasiwasi kuhusu hasara za Ulaya katika vita vya Ukraine
(last modified Mon, 05 Dec 2022 07:46:37 GMT )
Dec 05, 2022 07:46 UTC
  • Wasiwasi kuhusu hasara za Ulaya katika vita vya Ukraine

Baada ya kupita takriban miezi 10 tangu kuanza vita vya Ukraine na thari zake mbaya, mkuu wa Baraza la Ulaya amekiri kwamba, nchi za bara hilo zimepata hasara zaidi katika vita hivyo kuliko Marekani.

Licha ya kukiri kwamba vita vya Ukraine vimeziathiri Ulaya na Marekani kwa njia tofauti na kwamba Ulaya imepata hasara zaidi, mkuu wa Baraza la Ulaya, Charles Michel, amesema: Nchi za Magharibi zinaendelea kutuma silaha Ukraine. 

Nchi za Ulaya ambazo ziliingia katika vita vya Ukraine kwa kufuata sera za Marekani na kuchukua hatua kali eti za kuiadhibu Russia ikiwa ni pamoja na kuiwekea vikwazo vya aina mbalimbali, sasa zinakabiliwa na matatizo makubwa ya kiuchumi, kisiasa na kijamii huku vita hivyo vikiendelea. Watu wa Ulaya wanakabiliwa na wimbi la wakimbizi kutoka Ukraine ambao imekuwa vigumu sana kukidhi mahitaji yao kama malazi, chakula na kadhalika kutokana na matatizo ya kiuchumi yanayozikabili nchi hizo. Sambamba na hayo, nchi hizo za Ulaya zenyewe ziko katika hali mbaya ya upatikanaji wa nishati, hasa mafuta ya petroli na chakula, kutokana na kutegemea gesi na mafuta ya Russia. Suala hili limeifanya hali ya kiuchumi ya wananchi wengi wa nchi hizo kuwa mbaya, kiasi kwamba sasa wana wasiwasi mkubwa kutokana na msimu wa baridi unaobisha hodi; suala ambalo limeibua maandamano ya kijamii barani Ulaya. 

Maandamano Ulaya

Vita vya Ukraine pia vimeudhoofisha Umoja wa Ulaya na kuyumbisha nafasi ya umoja huo, kiasi kwamba makundi ya mrengo wa kulia katika nchi mbalimbali wanachama wa umoja huo yamepata nguvu zaidi, na baadhi ya nchi sasa zinajadili suala la kujitenga na Umoja wa Ulaya na kuwa huru. Baadhi ya nchi wanachama wa EU pia hazikubaliani na sera za Umoja wa Ulaya za kuingia katika vita vya Ukraine na zinalitambua jambo hilo kuwa ni kinyume na matakwa, mahitaji na maadili ya watu wa Ulaya. 

Kufuatia hali hiyo, Florian Philippot, kiongozi wa Chama cha Wazalendo cha Ufaransa (National Front) ametoa wito wa kujitoa katika Umoja wa Ulaya na kusema: "Umoja wa Ulaya na kiongozi wa Kamisheni ya Umoja huo wanatekeleza sera ya kiimla, na kwa sababu hiyo, Ufaransa inapaswa kuondoka kwenye muungano huu."

Kwa upande mwingine, nchi za Ulaya ambazo zilitarajia kupata msaada na uungaji mkono wa Washington, zimejikuta zikipuuzwa na Marekani. Washington si tu kwamba imepuuza mahitaji ya nchi za Ulaya na matarajio yao ya kupokea misaada ya kifedha na isiyo ya kifedha bali pia imekataa kuzidhaminia mahitaji yao ya mafuta na kinyume chake imetumia vibaya fursa hiyo na kuziuzia nishati na gesi kwa bei ya juu. Suala hilio limeibua malalamiko ya baadhi ya viongozi wa nchi za Ulaya, akiwemo Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron. Kuhusu suala hili Macron amesema: "Marekani inauza gesi yake kwa Ulaya kwa bei ya juu mara 3 hadi 4 zaidi ya bei ya gesi katika soko lake la ndani."

Emmanuel Macron

Kwa sasa nchi za Ulaya hazina chaguo ila kukidhi sehemu ya mahitaji yao ya nishati kutoka Marekani. Viongozi wa nchi za Ulaya wanaendelea kusaidia na kushirikiana na Ukraine katika vita, licha ya kwamba vita hivyo vimedhoofisha nguvu zao za kiuchumi na kisiasa katika nyanja za kimataifa. Inaonekana kwamba suala hili limefifiza ndoto ya kuunda jeshi moja la Ulaya bali hata Umoja wa Ulaya wenyewe unalazimika kufanyia marekebisho baadhi ya sera zake katika medani za kimataifa. Safari ya Charles Michel, Rais wa Baraza la Ulaya, nchini China na ombi lake kwa nchi hiyo kusaidia mchakato wa kumaliza vita vya Ukraine ni kukiri kwamba Wazungu wamedhoofika na kugonga mwamba, na sasa wananyoosha mkono wa kuomba msaada kwa nchi nyingi kama China.

Tags