Dec 11, 2022 02:29 UTC
  • Waislamu wahadharishwa na usambazwaji wa nakala zilizopotoshwa za Qur'ani katika intaneti

Jumuiya ya Kimataifa ya Uislamu imetangaza kuwa, kuna nakala zilizopotoshwa za Qur'ani Tukufu zinazosambazwa katika baadhi ya tovuti zisizojulikana rasmi.

Kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran IRIB, Jumuiya ya Kimataifa ya Uislamu imeeleza katika taarifa kwamba, kuna nakala zilizopotoshwa za Qur'ani Tukufu katika baadhi ya tovuti za intaneti zikiwa na makosa mbalimbali yakiwemo ya kuongezwa na kupunguzwa vitu katika baadhi ya matini za nakala hizo.

Jumuiya ya Kimataifa ya Uislamu imewataka Waislamu wote na vilevile Waislamu wenye majukumu ya uongozi popote pale duniani wawatahadharishe watu na kutumia tovuti za intaneti zisizo eleweka na nakala zilizopotoshwa za Qur'ani zilizomo kwenye tovuti hizo.

Mbali na kubainisha masikitiko yake kwa kusambazwa nakala za aina hiyo za Qur'ani katika intaneti, Jumuiya ya Kimataifa ya Uislamu imewataka maulamaa na wanatablighi kulipa uzito maalumu suala la kuwaelimisha watu juu ya kadhia hiyo na kuwataka wajihadhari kutumia nakala za Qur'ani zinazosambazwa katika intaneti.

Kwa mujibu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Uislamu, hivi karibuni zimeshuhudiwa nakala zilizopotoshwa za Qur'ani Tukufu katika aplikesheni za Apple Store, Google Play na nyinginezo katika simu erevu za mkononi, zikiwa na makosa kadha wa kadha ya herufi, maneno au hata ya baadhi ya aya za Qur'ani Tukufu, na vilevile ubadilishaji wa sehemu au hata alama za visimamo vya kisomo, ambao unapelekea kubadilika madhumuni, maana na irabu za aya za Qur'ani.../

Tags