Erdogan anawania uchaguzi wa rais kwa mara ya mwisho
Rais Recep Tayyep Erdogan wa Uturuki amesema kuwa kwa mara ya mwisho atagombea kiti cha rais katika uchaguzi wa mwaka kesho 2023.
Uchaguzi wa Bunge na Rais wa Uturuki umepangwa kufanyika mwakani na wapinzani nchini humo wanataraji kuwa watafanikiwa kuhitimisha udhibiti wa miaka 20 wa kuwepo madarakani chama tawala cha Uadilifu na Usawa.
Rais Recep Tayyep Erdogan alisema jana pambizoni mwa ufunguzi wa miradi mbalimbali katika mji wa Samsun unaopatikana katika pwani ya kaskazini ya Uturuki kwamba: hii ni mara ya mwisho kwangu kugombea kiti cha urais.
Erdogan amesema: atagombea kiti cha urais mwakani kwa uungaji mkono wa wananchi na tutaanza kuiasisi Uturuki iliyotimiza miaka 100 na kisha kuwakabidhi vijana bendera hii iliyobarikiwa.
Amesema, amekuwa katika medani ya siasa tangu miaka 50 iliyopita na alijikita tu katika kuwahudumia wananchi.
Kulingana na mfumo mpya huko Uturuki, mtu anaweza kuchaguliwa mara mbili kuwa rais wa nchi. Muhula wa urais wa miaka mitano wa Erdogan unamalizika Juni mwaka kesho huku mijadali ikiendelea nchini iwapo anaweza kwa mara nyingine tena kugombea kiti hicho au la.