Dec 29, 2022 02:24 UTC
  • Jibu kali la Moscow kwa tishio la Marekani la kumuua Putin

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Russia amesema kuwa matamshi ya maafisa wa Marekani katika Wizara ya Ulinzi ya nchi hiyo Pentagon, kuhusu pigo la kukata kichwa cha Kremlin kwa hakika ni tishio la kutaka kumuua kigaidi Rais wa Russia.

Sergey Lavrov, Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia ameongeza kuwa Washington imeenda mbali sana kufuatia baadhi ya maafisa wa Pentagon kutishia kutoa pigo kwa kukata kichwa cha Kremlin, na kuwa Moscow inalichukulia tishio hilo kumaanisha jaribio la kutaka kumuua kigaidi Rais Vladimir Putin wa nchi hiyo. Amesema, mtu aliye na mawazo na fikra kama hizo anapaswa kufikiria vizuri kuhusu matokeo ya hatua kama hiyo.

Jibu kali la Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia kuhusu tishio la hivi karibuni la Pentagon la kutaka kumuua Putin linaashiria juhudi zinazofanywa na Washington kwa ajili ya kupanua vita vya Ukraine, kufuatia kufichuliwa hatua zake za uharibifu na washirika wake katika ardhi ya Russia. Kwa hakika, serikali ya Biden imeanzisha vita mseto dhidi ya Russia ambapo inatumia mbinu zote za nguvu zikiwemo za kisiasa, kidiplomasia, kiuchumi na kibiashara, nishati, usalama na kijeshi, nguvu laini, propaganda na vita vya kisaikolojia dhidi ya Moscow.

Sergey Lavrov

Kwa kuzingatia kuwa Rais Vladimir Putin amekuwa na angali ana nafasi muhimu katika kuiongoza Russia na hatua inazochukua kimataifa na hasa kuhusiana na vita vya Ukraine, si jambo la kushangaza kwa Marekani kutaka kutekeleza hatua ya kigaidi ya kumuua rais huyo ili kujaribu kuondoa njiani kizingiti muhimu kinachozuia kufikiwa malengo ya Washingtton sio barani Ulaya pekee bali ulimwenguni kote. Bila shaka, Marekani ina historia ya kutoa vitisho kama hivyo na vita vya kisaikolojia dhidi ya Putin.

Uhusiano wa Marekani na Russia umekuwa ukidorora tangu Rais Joe Biden wa Marekani aingie madarakani Januari 2021 ambapo Washington imeongeza maradufu misimamo na vitendo vyake vya uhasama dhidi ya Russia. Biden alianza kudhihirisha uadui wake wa wazi dhidi ya Putin tangu alipochukua hatamu za uongozi ambapo katika mahojiano aliyofanyiwa mnamo Machi 2021, alimtaja Rais Vladimir Putin kama muuaji. Matamshi hayo yalikuwa hayajawahi kusikika tena kutoka kwa watawala wa Merikani dhidi ya viongozi wa Moscow na hivyo kukabiliwa na radiamali kali kutoka kwa Russia.

Vyacheslav Volodin, Spika wa Bunge la Russia, Duma, aliyataja matamshi hayo ya Biden dhidi ya Putin kuwa ishara ya kushindwa kwake kukabiliana na Russia na kusisitiza kuwa shambulio dhidi ya Putin ni shambulio dhidi ya Russia. Baada ya kuanza vita nchini Ukraine katikati ya Machi 2022, na huku akitangaza msaada mpya wa kijeshi wa dola milioni 800 kwa Ukraine, Joe Biden alimtuhumu Rais Vladimir Putin kwa mara ya kwanza kuwa ni mhalifu wa vita. Msimamo huo wa rais wa Marekani kwa kweli unaonyesha kina cha tofauti na uhasama wa Washington kwa Moscow, na wakati huo huo kubainisha mtazamo halisi wa watawala wa Marekani kuhusu viongozi wa Russia.

John Bolton

Inaonekana kwamba lengo la mwisho la Washington ni kumshusha hadhi Putin hadi kufikia kiwango cha madikteta kama Omar al-Bashir, rais wa zamani wa Sudan, ambaye anatafutwa na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC, na kisha kumtuhumu kuhusika na uhalifu wa kivita nchini Ukraine na hatimaye kutaka afuatiliwe kisheria na mahakama hiyo. Pamoja na hayo suala la Marekani kutaka kumuua kigaidi Rais Putin linachukuliwa kuwa tishio lisilo la kawaida. Bila shaka, katika miaka ya nyuma John Bolton, mshauri wa usalama wa taifa la Marekani wakati wa urais wa Donald Trump, alimuonya Rais Vladimir Putin kuhusu uwezekano wa matumizi ya silaha za nyuklia huko Ukraine, na kusema kulikuwa na uwezekano wa Washington kutekeleza mauaji dhidi yake.

Katika mahojiano mnamo Oktoba 2022, huku akijibu swali la iwapo Merikani ingeweza kumuua kiongozi mkubwa na mshuhuri kama Putin, Bolton alisema rais wa Russia alipaswa kutambua kuwa hata kama suala hilo lingechukua muda kutekelezwa lakini alipaswa kuwajibishwa.

Tags