Wanaharakati: Marekani haina nia ya kubadilisha sheria ya kumiliki silaha
https://parstoday.ir/sw/news/world-i9235-wanaharakati_marekani_haina_nia_ya_kubadilisha_sheria_ya_kumiliki_silaha
Wasomi, wadadisi wa mambo na watetezi wa haki za binadamu nchini Marekani wamesema serikali ya Washington haina azma ya kuangalia upya sheria ya kumiliki silaha licha ya mauaji ya kutisha ya hivi karibuni ya Orlando.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 15, 2016 02:57 UTC
  • Wanaharakati: Marekani haina nia ya kubadilisha sheria ya kumiliki silaha

Wasomi, wadadisi wa mambo na watetezi wa haki za binadamu nchini Marekani wamesema serikali ya Washington haina azma ya kuangalia upya sheria ya kumiliki silaha licha ya mauaji ya kutisha ya hivi karibuni ya Orlando.

Alice Bach, mwanaharakati wa amani na Profesa wa Masomo ya Kidini katika Chuo Kikuu cha Case Western Reserve mjini Cleveland jimbo la Ohio amesema Bunge la Kongresi la Marekani lilishindwa kupasisha sheria ya kudhibiti umiliki wa silaha huko nyuma na kwamba hakuna chochote kilichobadilika kufikia sasa kuashiria kuwa lina azma na irada ya kisiasa ya kuangalia upya sheria hiyo. Huku akiashiria mauaji ya wananafunzi 20 wa shule ya chekechea ya Sandy Hook katika mji wa Newtown, eneo la Connecticut Disemba 2012, baada ya kufyatuliwa risasi na jamaa aliyedaiwa kuwa na akili taahira, Alice Bach ambaye pia ni mtaalamu wa Biblia amesema kuwa, Wamarekani hawana matarajio yoyote ya kuangaliwa upya sheria hiyo baada ya mauaji ya Orlando. Wasi wasi wa wanaharakati na watetezi wa haki za binadamu nchini Marekani unajiri siku chache baada ya watu wasiopungua 50 kuuawa na wengine 53 kujeruhiwa katika ufyatuaji wa risasi uliotokea hivi karibuni katika mji wa Orlando jimbo la Florida. Ripoti zinasema kuwa, mauaji ya Orlando ni moja kati ya matukio yaliyosababisha mauaji makubwa ya ufyatuaji risasi katika historia ya Marekani. Uhuru wa kumiliki na kubeba silaha nchini Marekani umekuwa ukitajwa kuwa sababu ya mauaji ya raia elfu 33 kwa mwaka nchini humo.