Jan 11, 2023 09:18 UTC
  • Muelekeo wa kiundumakuwili na wenye mgongano wa Marekani kuhusiana na JCPOA

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Ned Price amesema, hatua ya upande mmoja iliyochukuliwa na serikali ya rais wa zamani wa nchi hiyo Donald Trump ya kujitoa kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA ni kosa kubwa zaidi la kistratejia lililofanywa katika miaka ya karibuni kwa upande wa sera za nje za Washington.

Price ameyasema hayo katika mkutano na waandishi wa habari, ambapo sambamba na kukosoa sera za serikali ya Trump kuhusiana na kadhia ya nyuklia ya Iran amesisitiza kwa kusema: "serikali hii (ya Joe Biden) inauchukulia uamuzi wa serikali iliyotangulia kuhusiana na kujitoa katika JCPOA kuwa ni moja ya makosa makubwa zaidi kufanywa katika sera za nje za Marekani katika miaka ya karibuni".

Mbali na kukosoa pia sera ya "mashinikizo ya juu kabisa" ya serikali ya Trump dhidi ya Iran, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani amesema: "ni wazi kwamba hatua hii ilikuwa haifai. Historia imetufunza kuwa mashinikizo ya kiuchumi huwa na ufanisi zaidi yanapofanyika kwa uratibu na mashauriano na washirika na waitifaki wetu wengine; na ndio sababu ya sisi kuthamini ushirikiano na waitifaki na washirika wa Ulaya hususan Troika ya Ulaya". 

Licha ya kauli hiyo ya msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani ya kukiri kwamba Washington ilifanya kosa kubwa kujiondoa katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, lakini jambo linaloonyesha kuwepo muelekeo wenye mgongano katika mtazamo wa Marekani kuhusiana na JCPOA ni kung'ang'ania msimamo wa kuyaweka kando mazungumzo ya Vienna. Kuhusiana na suala hilo, katika mkutano aliofanya na waandishi wa habari Jumatano ya tarehe 4 Januari, Ned Price alithibitisha kusitishwa kwa mazungumzo ya kufufua makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na akasema: "kutokana na kukandamizwa wapinzani nchini Iran, kwa sasa, serikali ya Joe Biden imejikita katika kutoa msukumo na uungaji mkono kwa watu wa Iran". Price akadai pia kwa kusema: "mnamo Septemba iliyopita makubaliano ya kufufua JCPOA yalikuwa yameshafikiwa na tayari kusainiwa, lakini upande wa Iran ulikataa kuyasaini kwa kutovikubali vipengee vyake; na ni kwa msingi huo tangu miezi kadhaa iliyopita JCPOA imeondolewa kwenye ajenda za Marekani na kwa sasa tumeelekeza jitihada zetu zote katika kuunga mkono haki za kimataifa za watu wa Iran na kukabiliana na uhusiano wa kijeshi unaoendelea kukua uliopo baina ya Iran na Russia".

Kuthibitisha na kusisitizia kwamba kujitoa Trump katika JCPOA lilikuwa kosa la kistratejia kwa upande mmoja, na kuibebesha lawama Iran za kuvunjika mazunguzo ya Vienna sambamba na kutamka kinagaubaga kuwa JCPOA haipo tena kwenye ajenda na vipaumbele vya Marekani kwa upande mwingine, kunadhihirisha misimamo ya kiundumakuwili ya serikali ya Biden kuhusiana na makubaliano hayo ya nyuklia. Licha ya masisitizo chungu nzima na ya kila mara yanayotolewa na rais mwenyewe wa Marekani na viongozi wengine waandamizi wa serikali yake kuhusu ulazima wa kuyalinda makubaliano ya JCPOA na kufanya juhudi za eti kuyafufua, lakini baada ya kuzuka machafuko hivi karibuni nchini Iran, Washington na washirika wake wa Ulaya waliyachukulia machafuko hayo kuwa fursa ya kipekee ya kuidhoofisha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran; na kwa ndoto zao za alinacha wakadhani kwamba Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu utaporomoka na kutoweka. Na ndio maana hawakufanya juhudi yoyote ya kuanzisha tena mazungumzo ya Vienna; na badala yake, Washington ikatumia muda wake wote kupigia upatu na kuunga mkono machafuko na wavurugaji amani ndani ya Iran na kuchukua hatua za kila aina ili kuhakikisha moto wa fujo na machafuko hayo unazidi kuwa mkubwa.

Ukweli ni kwamba serikali ya Biden, kwa upande mmoja inadai kutumia diplomasia katika kuamiliana na Iran kuhusiana na kadhia ya JCPOA, na sambamba na kutumiana salamu na Tehran kwa njia isiyo ya moja kwa moja na kutilia mkazo mazungumzo; na kwa upande mwingine inaingilia masuala ya ndani ya Iran kwa kujaribu kuwachochea na kuwahamasisha wafanya fujo na wavuruga amani. Hata hivyo hatua hizo zimeshindwa vibaya na kwa namna ya kufedhehesha na kudhihirika wazi kuwa fujo na machafuko haviwezi kuuyumbisha Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Avril Haines

Mnamo mwanzoni mwa Septemba 2022, Avril Haines mkurugenzi wa intelijensia ya taifa ya Marekani aligusia kuhusu kutokea fujo na machafuko ndani ya Iran na akaeleza kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hailioni suala hilo kama tishio kwa uthabiti wake.

Nukta muhimu na ya kustaajabisha pia ni kwamba, licha ya serikali ya Biden kukiri kuwa kujitoa Marekani katika JCPOA lilikuwa kosa kubwa na la kistratejia, lakini ingali inaendeleza, tena kwa nguvu zote, sera ya Trump iliyogonga mwamba ya uwekaji vikwazo dhidi ya Iran ijulikanayo kama "mashinikizo ya juu kabisa"; na huku ikiamua kuyaweka kando mazungumzo ya uondoaji vikwazo imeamua kuunga mkono kwa kila hali machafuko ndani ya Iran ili kufikia malengo yake batili. Washington ingali inadhani kuwa itaweza kufikia malengo yake hewa na batili kwa njia ya kushadidisha mashinikizo dhidi ya Tehran na kuingilia zaidi masuala ya ndani ya Iran; ilhali kusimama imara Iran kupitia sera yake ya muqawama wa kiwango cha juu kabisa kumefelisha na kusambaratisha sera ya vikwazo ya Marekani na kushindwa kila mara pia Washington yenyewe katika kukabiliana na Iran.../

Tags