Zarif: Iran inaweza kuwa mshirika muhimu wa kibiashara wa Ujerumani
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza kuwa hakuna mtu anayeweza kusababisha madhara katika ushirikiano wa kiuchumi kati ya Iran na Ujerumani na kwamba Iran ikiwa ni nchi iliyopiga hatua inaweza kuwa mshirika muhimu wa kibiashara wa Ujerumani.
Muhammad Javad Zarif alisema jana usiku mbele ya waandishi wa habari baada ya kufanya mazungumzo na mwenzake wa Ujerumani Frank Walter Stainmeier huko Berlin kuwa, uhusiano wa Iran na Ujerumani umeimarika pakubwa na ni wa siku nyingi. Amesema, kuwepo makampuni ya Kijerumani na taasisi za kifedha na kibenki za nchi hiyo hapa Iran na kushirikiana kiuchumi Iran na Ujerumani ni kwa ajili ya maslahi ya nchi mbili na vile vile kwa ajili ya amani na uthabiti katika eneo na ulimwenguni kwa kwa ujumla.
Zarif amesema kuwa Iran na Ujerumani zina mitazamo inayokaribiana na katika sekta mbalimbali kwa ajili ya kudumisha amani na usalama katika eneo na kuongeza kuwa, makundi yenye misimamo mikali hayatoacha kutekeleza hujuma katika eneo lolote. Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa umoja na mshikamano unahitajika ili kuendesha mapambano dhidi ya makundi hayo.
Katika mazungumzo hayo naye Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani ameashiria rekodi ya uhusiano mzuri na wa siku nyingi kati ya Iran na Ujerumani na kueleza kuwa Ujerumani inataka kuwa na ushirikiano ulioimarika kati yake na Iran katika nyanja zote.