Utafiti: Marekani haipo tayari kuingia vitani na China
https://parstoday.ir/sw/news/world-i93266-utafiti_marekani_haipo_tayari_kuingia_vitani_na_china
Kituo cha Kimataifa cha Tafiti za Kistratejia (CSIS) kimeonya kuwa, Marekani haina ubavu wala akiba ya kutosha ya silaha na zana za kijeshi za kuiwezesha kuingia katika makabiliano ya kijeshi na China.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 24, 2023 23:00 UTC
  • Utafiti: Marekani haipo tayari kuingia vitani na China

Kituo cha Kimataifa cha Tafiti za Kistratejia (CSIS) kimeonya kuwa, Marekani haina ubavu wala akiba ya kutosha ya silaha na zana za kijeshi za kuiwezesha kuingia katika makabiliano ya kijeshi na China.

Taasisi ya CSIS ambayo inategemea ufadhili wa kampuni za silaha na zana za kijeshi kama Lockheed Martin, Boeing, na General Dynamics imesema kuwa, kwa mujibu wa utafiti wake, sekta ya ulinzi ya Marekani haiendani na mazingira ya sasa katika ushindani wa kuwa na akiba ya kutosha au kuzalisha silaha.

Kituo cha Kimataifa cha Tafiti za Kistratejia kimeeleza bayana kuwa, iwapo vita vitaibuka ghafla kati ya Marekani na China kwa ajili ya Taiwan, yumkini Marekani itashindwa kutokana na uhaba wa silaha, haswa kwa kuzingatia kuwa imeipa Ukraine silaha nyingi yakiwemo makombora na mitambo ya rada.

CSIS imesema imefuatilia mazoezi kadhaa ya kijeshi yaliyofanywa na Marekani hivi karibuni na kubaini kuwa, Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) huenda ikaishiwa na makombora muhimu ndani ya wiki ya kwanza ya makabiliano tarajiwa baina yake na China juu ya Taiwan.

Beijing imekuwa ikisisitiza kuwa, kisiwa cha Taiwan ni sehemu ya ardhi kuu ya China. Aidha China mara kadhaa imesisitiza kuwa, Marekani ndiyo chanzo cha kuvurugika amani katika eneo, ikiwa ni pamoja na Bahari ya Kusini ya China, na kuitaka Washington iache hatua zake hatarishi na za kichochezi.

Kwa mujibu wa Beijing, uwepo wa Marekani katika eneo na mazoezi ya kijeshi yanayofanywa mara kwa mara na nchi hiyo na washirika wake (Korea Kusini na Japan), ndio sababu ya mvutano unaoshuhudiwa katika eneo hilo, na imeshatoa indhari mara kadhaa kuhusiana na uwepo huo wa kijeshi wa Washington.