Feb 06, 2023 11:07 UTC
  • Waislamu waandamana Uholanzi kulaani kuvunjiwa heshima Qur'ani

Waislamu nchini Uholanzi wamefanya maandamano katika mji wa Hague, kulaani kitendo cha kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu nchini humo.

Mamia ya Waislamu walikusanyika jana Jumapili katika medani ya jijini Hague, wakiwa wamebeba mabango yenye maandishi yanayolaani kitendo cha kuidhalilisha Qur'ani Tukufu katika nchi hiyo na nchi nyingine ya Ulaya ya Sweden.

Katika maandamano hayo ya jana mjini Hague, Waislamu waliokusanyika katika medani ya makao makuu ya kiidara ya Uholanzi, walisoma Aya za Qur'ani Tukufu na pia kuswali Swala kwa jamaa.

Akizungumza katika maandamano hayo, Tahsin Cetinkaya, Mkuu wa Wakfu wa Utamaduni wa Kiislamu wa Uturuki amesema vitendo vya chuki dhidi ya Uislamu vimeshtadi nchini Uholanzi katika miaka ya hivi karibuni, huku Waislamu, misikiti na taasisi za Kiislamu zikihujumiwa na kushambuliwa na watu wenye chuki dhidi ya dini hiyo tukufu.

Mwishoni mwa mwezi uliopita, Edwin Wagensveld, mwanasiasa wa mrengo wa kulia na mwenye chuki kubwa dhidi ya Uislamu wa Uholanzi, kwa kejeli, dharau na majivuno alichana kurasa za Qurani Tukufu katika mji wa Hague kadamnasi ya watu na kamera. 

Maandamano ya kulaani kuvunjiwa heshima Qurani nchini Iran

Mwanasiasa huyo alienda mbali zaidi na kuzichoma moto kurasa hizo za Qur'ani Tukufu alizozichana, kitendo ambacho kiliwaghadhabisha na kuumiza nyoyo na hisia za Waislamu kote duniani.

Mataifa na jumuiya za Kiislamu kote duniani zimeendelea kulaani kitendo cha kuvunjiwa heshima Qurani Tukufu katika nchi za Ulaya za Uholanzi na Sweden. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Lebanon, Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu, Qatar, Misri, Jordan, na Palestina ni miongoni mwa nchi zilizochukua msimamo dhidi ya kitendo hicho cha kuchukiza nchini Uholanzi na Sweden.

Tags