Feb 08, 2023 03:17 UTC
  • Indhari ya Antonio Guterres kuhusu kubadilika vita vya Ukraine na kuwa vita vya dunia

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametahadharisha kwamba, hatua zozote za kuchochea mgogoro wa Russia na Ukraine huenda zikaitumbukiza dunia katika vita vipana na vikubwa zaidi.

Antonio Guterres, alitoa indhari hiyo siku ya Jumatatu katika hotuba yake mbele ya Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na kuongeza kuwa, ulimwengu unakaribia kutumbukia katika vita vikubwa zaidi. Guterres ameeleza kuwa, "Jamii ya kimataifa si tu inatembea (taratibu) ndotoni ikielekea katika vita vikubwa zaidi, lakini inaelekea kwa upesi kwenye vita hivyo. Matumaini ya amani yanazidi kufifia, huku nafasi ya kupanua zaidi mgogoro na umwagaji damu ikiendelea kuwa kubwa zaidi."

Guterres amebainisha kuwa, changamoto za kimataifa za kipindi kilichopita bado zingalipo, na mchakato wa kuimarisha amani na maendeleo endelevu uko hatarini. Amesema, 'Iwapo kila nchi itafungamana na wajibu wake kwa mujibu wa Hati ya Umoja wa Mataifa, haki ya amani itadhaminiwa."

Indhari ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu kuchukua wigo mpana zaidi vita vya Ukraine na kuwa vita vya dunia inatolewa katika hali ambayo, kwa kuzingatia kwamba, mzozo huo hivi sasa unaingia katika mwaka wake wa pili kuna kila ishara za kupanuka wigo wa vita hivyo hasa kwa kuzingatia utendaji haribifu wa madola ya magharibi yakkiongozwa na Marekani.

Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa

 

Ukweli wa mambo ni kuwa, moto wa vita vya Ukraine utazidi kuwaka hasa kutokana na sera chafu za madola ya Magaribi na hasa hatua ya madola hayo ya kutoa misaada mikubwa ya kijeshi na kisilaha kwa Ukraine ambayo haijawahi kushuhudiwa. Ni kwa kuzingatia ukweli huo ndio maana wajuzi wa mambo wanaamiini kuwa, moto wa vita hivyo badala ya kuzimikka utazidi kuwaka na kupanuka wigo wake.

Marekani licha ya kupiga nara za ulazima wa kuhitimishwa vita vya Ukraine, lakini kivitendo imekuwa ikichochea vita hiyo, lengo lake likiwa ni kuidhoofisha Russia na kuishughulisha zaidi na mzozo huo. Ili kufikia lengo hilo, serikali ya Washington imekuwa ikiwashajiisha waitifaki wake wa Kimagharibi na hasa wa Ulaya na hata kuwashinikiza ili waongeze utumaji misaada ya kijeshi na silaha huko Ukraine.

Marekani na washirika wake sio tu kwamba, hawajapunguza misaada yao ya kijeshi la silaha kwa Ukraine, bali filihali wameipatia nchi hiyo silaha, zana na suhula za kisasa zaidi za kivita.

Dmitry Medvedev, Naibu Mwenyekiti wa Baraza la Usalama wa Taifa la Russia alionya mwishoni mwa mwezi uliopita wa Januari kwamba: Dunia inakabailiwa na hatari ya vita vya tatu vya dunia kutokana na chuki na uhasama dhidi ya Moscow na kwamba, hatari hiyo ipo karibu.

Silaha kwa ajili ya Ukraine

 

Kadhalika alisisitiiza kuwa, Russia itafanya kila iwezalo kuzuia kutokea maafa ya atomiki na vita vya tatu vya dunia na kuongeza kuwa, kama sisi hatutapa dhamana ya uhakika ya usalama wa Russia, mzozo huu utaendelea kwa sura isiyo na mpaka na hivyo kuufanya ulimwengu uelekee katika njia ya vita vya tatu vya dunia na katika maafa ya atomiki.

Licha ya indhari na maonyo haya, lakini kambi ya Magharibi imekuwa ikipuuza yote haya. Kwa mtazamo wa viongozi wa Masgharibi ni kuwa, kuibuka na ushindi Russia katika vita vya Ukraine tena katika hali NATO inaisadia Kiev itakuwa na maana ya kukosa itibari asasi hiyo ya kijeshi na kuifanya Russia izidi kuwa na satuwa, nguvu na ushawishi kieneo na kimataifa na hivyo kubadilisha mahesabu ya kiusalama, kijeshi na kisiasa ya madola ya Ulaya.

Kadhalika kwa mtazamo wa Rais wa sasa wa Marekani Joe Biden na maafisa wa ngazi za juu wa kijeshi na kiusalama wa serikali yake ni kuwa, vita vya Ukraine ni fursa isiyo na mithili na kuonyesha upinzani dhidi ya Russia kadiri inavyowezekana na hatimaye kuidhoofisha nchi hiyo na kwa muktadha huo kuzuia kikamilifu kuundika kambi ya kadhaa. Ni kwa kuzingatia ukweli huo ndio maana viongozi hao wamejianda na hivyo kuhakikkisha kuwa, wanazuia kwa gharama yoyote ile kupata ushindi Russia katika vita vya Ukraine.

Katika upande wa pili Russia inaamini kuwa, lengo la madola ya Magharibi la kuendelea vita vya Ukarine ni kuidhoofisha Moscow kadiri inavyowezekana na hatimaye kuigawa. Kwa kuzingatia hali hiyo, vita vya Ukraine siyo tu kwamba, havitafikia tamati hivi karibuni, lakini kwa kuzingatia misaada mikubwa ya kijeshi ambayo haijawahi kushuhudiwa ya madola ya Magharibi kwa Ukraine, wigo wa vita hivyo utapanuka na kuchukua mkondo mpana zaidi. Anga inayotawala katika kadhia ya Ukraine imeongeza uwezekano wa Russia kutumia silaha za atomiki na ulimwengu kushuhudia vita vya tatu vya dunia. Katika mazingira kama haya, ulimwengu utakuwa katika ukingo wa kuangamia kikamilifu.

Tags