Musk amuanika mwanadiplomasia wa US anayechochea vita vya Ukraine
Bilionea wa Kimarekani, Elon Musk, ambaye ni mmiliki wa mtandao wa kijamii wa Twitter amemtuhumu mwanadiplomasia wa ngazi ya juu wa Marekani kuwa ndiye anayekoleza moto wa vita vya Ukraine.
Musk ambaye pia ni Afisa Mkuu Mtendaji wa kampuni ya magari, akili mashine na nishati safi ya Marekani ya Tesla amesema hayo katika ujumbe wake kwenye Twitter na kueleza kuwa, Victoria Nuland, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani anayesimamia masuala ya kisiasa kuwa ndiye anayeongoza kampeni ya kuchochea vita vya Ukraine.
Katika ujumbe huo aliouchapisha kwenye ukurasa wake wa Twitter, Elon Musk ameandika, "Hakuna mtu anayesukuma vita hivi (vya Ukraine) zaidi ya Nuland."
Musk ameunga mkono ujumbe wa Twitter wa mwanasaikolojia maarufu wa Canada, Jordan Peterson ambaye hivi karibuni alichapisha makala inayoulaumu utawala wa Rais Joe Biden wa Marekani kwa kuchochea moto wa vita Ukraine.
Makala hiyo iliyoandikwa na mwanahabari wa Russia, Igor Korotchenko imeikosoa serikali ya Biden kwa kuunga mkono mashambulizi ya Ukraine dhidi ya eneo la Crimea, ambalo lilijiunga na Russia mwaka 2014 baada ya kufanyika kura ya maoni ambapo zaidi ya asilimia 96 ya washiriki katika kura hiyo waliunga mkono suala hilo.
Hii ni katika hali ambayo, Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) jana Ijumaa ilitangaza kuwa itaipa Ukraine kifurushi kipya cha msaada wa silaha mbali mbali wenye thamani ya dola bilioni 2, zikiwemo ndege zisizo na rubani (droni).
Hii ni licha ya Moscow kuonya kwamba uamuzi wa kuirundikia silaha Ukraine utajibiwa vikali na Russia, wakati huu ambapo vita hivyo vimeingia mwaka wake wa pili.