China yaongeza bajeti ya kijeshi sambamba na kuongezeka mikwaruzano na Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i94790-china_yaongeza_bajeti_ya_kijeshi_sambamba_na_kuongezeka_mikwaruzano_na_marekani
Serikali ya China imeongeza bajeti yake ya kijeshi kwa asilimia 7.2 hadi dola bilioni 224 ikilinganishwa na mwaka jana sambamba na kuendelea kushuhudiwa mivutano kati ya nchi hiyo na Marekani.
(last modified 2026-04-26T10:08:53+00:00 )
Mar 06, 2023 06:28 UTC
  • China yaongeza bajeti ya kijeshi sambamba na kuongezeka mikwaruzano na Marekani

Serikali ya China imeongeza bajeti yake ya kijeshi kwa asilimia 7.2 hadi dola bilioni 224 ikilinganishwa na mwaka jana sambamba na kuendelea kushuhudiwa mivutano kati ya nchi hiyo na Marekani.

Kufuatia kuongezeka mivutano kati ya Washington na Beijing na baada ya ombi lililotolewa na Waziri Mkuu wa China Li Keqiang la kuimarishwa utayari wa kijeshi wa jeshi la nchi hiyo, Beijing inakusudia kuongeza bajeti yake ya ulinzi kwa asilimia 7.2 mwaka huu.
Ongezeko la bajeti ya kijeshi ya China mwaka huu ni kubwa kidogo kuliko ongezeko la mwaka jana na limevuka utabiri wa wastani wa ukuaji wa uchumi wa serikali.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, bajeti ya taifa ya China iliyotolewa leo imeonyesha kuwa yuan trilioni 1.55 (sawa na dola bilioni 224) zimetengwa kwa bajeti ya kijeshi.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, bajeti ya ulinzi ya China itatoa mguso kwa majirani wa nchi hiyo na Marekani, ambayo inadai eti inatiwa wasiwasi na malengo ya kimkakati ya China na hatua zake za kulipanua jeshi lake.
Li Keqiang

Katika ripoti yake ya kazi kwa ajili ya kikao cha mwaka cha bunge la nchi hiyo, Waziri Mkuu wa China Li Keqiang amesema: "operesheni za kijeshi na ujengaji uwezo na utayari wa China kwa ajili ya mapigano ya kivita lazima "ziratibiwe vyema katika utekelezaji wa majukumu makuu na ya asili."

Hivi karibuni Wizara ya Mambo ya Nje ya China ilisisitiza kuwa Marekani ndiyo chanzo cha tishio la nyuklia duniani na kuongeza kuwa: "Washington inaibua nadharia ya kitisho cha China ili ipate kisingizio cha kuyasheheni zaidi maghala yake ya silaha".../