Juhudi za China za kumaliza mgogoro wa Ukraine
https://parstoday.ir/sw/news/world-i95344-juhudi_za_china_za_kumaliza_mgogoro_wa_ukraine
Rais Xi Jinping wa China, amesema kuwa mpango wa nchi yake wa kutatua mzozo wa Ukraine unaakisi maoni ya ulimwengu, na kuwa vipengee 12 vya mpango huo vitaondoa kabisa taathira hasi za mgogoro huo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 21, 2023 03:22 UTC
  • Juhudi za China za kumaliza mgogoro wa Ukraine

Rais Xi Jinping wa China, amesema kuwa mpango wa nchi yake wa kutatua mzozo wa Ukraine unaakisi maoni ya ulimwengu, na kuwa vipengee 12 vya mpango huo vitaondoa kabisa taathira hasi za mgogoro huo.

Rais Xi Jinping amesema matatizo makubwa na tata kwa kawaida huwa hayana njia rahisi na ya mkato ya kuyatatua. Jingping amewasilisha mpango wa kutatuliwa kwa amani mgogoro wa Ukraine katika hali ambayo mpango huo unapingwa vikali na nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani. Katika miezi ya karibuni China imeingia katika uwanja wa kimataifa kama mpatanishi muhimu na mwenye taathira kubwa katika mkondo wa kuleta amani kimataifa na kieneo. Imewasilisha mpango wenye vipengee 12 kwa ajili ya kutatua mgogoro wa Ukraine, mpango ambao umepuuziliwa mbali na Marekani inayodai kuwa unahudumia maslahi ya Russia.

Kwa msingi huo katika mkesha wa safari yake huko Russia, ambayo inathibitisha mwenendo wa kuimarika uhusiano wa Beijing na Moscow, Rais Jinping ameutetea mpango huo wa amani kwa hoja kuwa umeandaliwa bila ya upendeleo wowote na kwa viwango vya kimataifa.

Rais Xi Jinping akiwa na mwenyeji wake Rais Vladimir Putin mjini Moscow

Li Kan, mtaalamu wa masuala ya kimataifa anasema: "Mpango wa China wenye vipengele 12 umezingatia masuala na maslahi yote ya pande zinazohusika katika mgogoro huo, na kwa kuwa lengo na nia ya mpango huo ni kusaidia kuleta amani na usalama nchini Ukraine, ni mpango wa kiwango cha kimataifa uliosimama juu ya msingi wa matakwa ya ulimwengu, na ndio maana Rais wa China ameutetea kikamilifu na kutaka uungwe mkono kimataifa.

Kwa sasa Rais Xi Jingping yuko nchini Russia ambapo anajadiliana na Rais Vladimir Putin wa nchi hiyo kuhusiana na masuala ya pande mbili na kimataifa, hasa mgogoro wa Ukraine. Kwa kutilia maanani kuwa China tayari imetangaza msimamo wake kuhusu njia za kutatuliwa mgogoro huo, ni wazi kuwa mazungumzo ya pande mbili yanaweza kuchangia pakubwa katika kutatuliwa kisiasa mzozo huo.

Kwa mujibu wa tangazo la Wizara ya Mambo ya Nje ya China, mpango wa nchi hiyo wenye vipengele 12 unajumuisha usitishaji vita na kusimamishwa vikwazo vya Magharibi dhidi ya Russia, jambo ambalo viongozi wa Marekani wanaonekana kutoafikiana nalo baada ya kupinga hivi karibuni suala la usitishaji vita huko Ukraine, na hivyo kuthibitisha kivitendo kuwa hawana nia wala wala hamu yoyote ya kuhitimisha mgogoro wa nchi hiyo.

Muda mfupi kabla ya kuanza safari ya Jinping huko Moscow Rais Putin wa Russia pia alikaribisha msimamo wa China usiopendelea upande wowote katika mgogoro wa Ukraine na hivyo kuwathibitishia walimwengu kuwa Russia iko tayari kusimamisha mgogoro huo kwa njia ya kidiplomasia na kuwa ni Marekani ndiyo inaendelea kuweka vizingiti katika njia hiyo.

Abulfazl Zuhrevand, mtaalamu wa masuala ya kimataifa anasema kuhusu suala hilo kwamba siasa za Marekani ni kuchochea zaidi mgogoro wa Ukraine na kuidhoofisha Russia. Ni kwa msingi huo ndio ikawa inafanya juhudi zote kwa ajili ya kutoa mashinikizo dhidi ya Moscow. Hii ni katika hali ambayo Russia imethibitisha kivitendo kwamba inao uwezo wa kutosha wa kusimama imara mbele ya mashinikizo ya kisiasa, kiuchumi na kiusalama ya Marekani na nchi nyingine za Magharib, na hilo ni jambo ambalo linaikasirisha sana Marekani.

John Kirby

Kwa vyovyote vile, matamshi ya John Kirby, mratibu wa mawasiliano ya kistratijia wa Baraza la Usalama wa Kitaifa la Marekani, kwamba Marekani itapinga ombi lolote la kusitisha mzozo wa Ukraine baada ya ziara ya Xi Jinping nchini Russia, yanathibitisha wazi uhasama na chuki ya Marekani dhidi ya China. Nchi hiyo ya Magharibi ina wasiwasi kwamba, kwa kutekeleza siasa za kusaidia kuimarisha na kuleta amani duniani, China itaweza kuzima siasa za ubeberu za Marekani ulimwenguni na hivyo kuathiri vibaya kiburi na ubabe wa nchi hiyo katika ngazi za kimataifa. Hii ni katika hali ambayo nchi za eneo zinakaribisha kwa moyo mkunjufu mipango ya kuimarisha amani na usalama na hivyo kuthibitisha kuwa zina kiu ya amani na wakati huo huo kupinga siasa za mabavu na udikteta zinazotekelezwa na Marekani katika pembe tofauti za dunia.