Uturuki yawasilisha malamiko rasmi kuhusu kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu huko Denmark
Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki imemwita balozi wa Denmark nchini humo ili kutoa malalamiko yake ya kupinga kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu katika nchi hiyo ya Ulaya.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki imetoa taarifa na kusema: "Tunalaani kwa maneno makali kwamba uhalifu wa chuki uliofanywa nchini Denmark tarehe 24 Machi dhidi ya Kitabu chetu Kitukufu, Qur'ani, na bendera yetu tukufu umeruhusiwa kutekelezwa tena tarehe 31 Machi katika mwezi Mtukufu wa Ramadhani."
Taarifa hiyo imesema kwamba Balozi wa Denmark, Danny Annan aliitwa kwenye wizara hiyo mjini Ankara na kufahamishwa kwamba Uturuki inalaani vikali na kupinga kitendo hicho kiovu cha kuvunjia heshima Qur'ani Tukufu.
"Kwa mara nyingine tena tunatoa wito kwa mamlaka ya Denmark kuchukua hatua zinazofaa dhidi ya wahusika wa uhalifu huu na kuchukua hatua madhubuti kuzuia kutokea tena kwa uchochezi huo," iliongeza wizara hiyo.
Aidha taarifa hiyo imesema, "kutoa ruhusa kwa kitendo hicho kiovu chini ya kivuli cha uhuru wa kujieleza hakukubaliki kabisa na kitendo kama hicho hakiwezi kuhalalishwa ,"
Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki imeongeza kuwa, kitendo hicho "ni uthibitisho wa wazi kwamba chuki dhidi ya Uislamu, chuki dhidi ya wageni, ubaguzi na ubaguzi wa rangi vimeongezeka barani Ulaya."
Wiki iliyopita pia Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran alilaani wimbi la kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu na makundi yenye misimamo mikali ya mrengo wa kulia nchini Denmark na katika nchi nyingine za Ulaya.
Nasser Kan'ani, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran alikosoa vikali wimbi hilo la kuvunjiwa heshima Kitabu Kitukufu cha Waislamu katika nchi kadhaa za Ulaya na kueleza kuwa, vitendo hivyo vinahatarisha amani na kuishi kwa utangamano jamii ya wanadamu.
Miezi ya hivi karibuni kumeshuhudiwa vitendo kadhaa vya uchomaji wa Qur'ani, au majaribio ya kufanya hivyo, na watu au makundi yenye chuki dhidi ya Uislamu kaskazini mwa Ulaya na nchi za Nordic.