Sadio Mane akabiliwa na adhabu baada ya kumtandika ngumi mchezaji mwenzake
Bayern Munich imemsimamisha mshambuliaji Sadio Mane raia wa Senegal baada ya kumpiga usoni mchezaji mwenza Leroy Sane kufuatia kichapo cha Jumanne cha Ligi ya Mabingwa dhidi ya Manchester City.
Mane pia atapigwa faini na hatakuwa sehemu ya kikosi cha Bayern kwa ajili ya mchezo wao wa nyumbani wa Bundesliga dhidi ya Hoffenheim siku ya Jumamosi.
Sky Germany iliripoti kuwa mdomo wa Sane ulikuwa ukivuja damu baada ya ugomvi huo na wachezaji hao wawili walihitaji kutenganishwa na wenzao kwenye chumba cha kubadilishia nguo.
Taarifa kutoka Bayern ilisema: "Sadio Mane, 31, hatakuwepo kwenye kikosi cha FC Bayern kitakachocheza nyumbani dhidi ya 1899 Hoffenheim Jumamosi ijayo.
Sababu ni utovu wa nidhamu wa Mane baada ya mchezo wa Ligi ya Mabingwa wa FC Bayern dhidi ya Manchester City. Aidha, Mane atatoa faini. Wengi wameshangazwa na kitendo hicho cha Sadio Mane ambaye anafahamika kwa upole.
"Sane na Mane walionekana uwanjani wakizozana katika hatua za mwisho za mechi hiyo Jumanne usiku, ambapo Man City waliwatandika mabingwa hao wa Ujerumani mabao 3 kwa nunge kwenye Uwanja wa Etihad katika mchezo wa awali wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.