Wakazi wa London waadhimisha Siku ya Kimataifa ya Quds Jumapili hii
Mikusanyiko na maandamano mbalimbali ya kuunga mkono Palestina yamefanyika mjini London leo Jumapili katika kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Quds.
Imam Khomeini (M.A) Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mwaka 1979 aliiitangaza Ijumaa ya mwisho ya mwezi mtukufu wa Ramadhani kila mwaka kuwa Siku ya Kimataifa ya Quds na kuanzia mwaka huo hadi sasa maeneo mbalimbali duniani hufanya maandamanao katika siku hiyo kuwaunga mkono na kuonyesha mshikamano kwa wananchi wa Palestina, na vilevile kulaani vitendo vya kiuhasama vya utawala wa Kizayuni dhidi ya Palestina na Msikiti Mtukufu wa al Aqsa.
Wakazi wa London mji mkuu wa Uingereza wao kwa upande wao leo Jumapili wameadhimisha siku ya Kimataifa ya Quds kwa kuandamana katika mitaa mbalimbali ya mji huo. Wakazi wa mji huo wameandamana hadi mbele ya ubalozi wa utawala wa Kizayuni wa Israel na kulaani jinai za utawala huo dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina.
Kuhani wa Kiyahudi Yacoub Weiss amesema katika mahojiano aliyofanyiwa na Iran Press huko London kwamba: Tunaunga mkono haki za Wapalestina na ninaona huu ni wajibu wetu nikiwa kama Myahudi."
Huku akisisitiza kuwa Uzayuni ni fikra ya kisiasa, Kuhani huyo wa Kiyahudi amesema, kinyume na namna wengi wanavyofikiri, Wazayuni si Wayahudi.
Wakati huo huo mwanamama mmoja aliyeshiriki kwenye maandamano hayo ya London ya maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Quds ameiambia Iran Press kwamba: Serikali za nchi za Magharibi na hasa ya Uingereza zimenyamaza kimya mbele ya jinai za Israel dhidi ya wananchi wa Palestina.
Maadhimisho ya Siku ya Kmataifa ya Quds mwaka huu yamekuwa na umuhimu maalumu kwa kuzingatia matukio ya karibuni katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina na mashambulizi ya mara kwa mara ya Israel huko Quds na katika msikiti Mtukufu wa al Aqsa.