China yamshambulia Biden kwa kudai kuwa Rais Xi ni dikteta
https://parstoday.ir/sw/news/world-i99060-china_yamshambulia_biden_kwa_kudai_kuwa_rais_xi_ni_dikteta
Beijing imekosoa vikali matamshi ya Rais Joe Biden wa Marekani aliyedai kuwa Rais Xi Jingping wa China ni dikteta.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jun 22, 2023 02:34 UTC
  • China yamshambulia Biden kwa kudai kuwa Rais Xi ni dikteta

Beijing imekosoa vikali matamshi ya Rais Joe Biden wa Marekani aliyedai kuwa Rais Xi Jingping wa China ni dikteta.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China, Mao Ning amesema matamshi ya Biden yanachukiza, yanasikitisha, ni ya kichochezi  na yanaonesha hulka ya kupenda uchokozi wa wazi wa kisiasa ya Washington. 

Mao Ning ameeleza bayana kuwa, matamshi hayo ya Biden yanakiuka wazi kanuni za kidiplomasia mbali na kwenda kinyume na uhalisia wa mambo.

Biden juzi Jumanne akiwa California alidai kuwa, Rais Xi hakuwa na ufahamu wowote juu ya puto la China kuingia katika anga ya Marekani mapema mwaka huu, na eti jambo hilo ni fedheha kubwa kwa madikteta.

Xi na Biden

Akijibu bwabwaja hizo, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China amesema, matamshi ya Biden yanakanyaga wazi wazi hadhi ya kisiasa ya China.

Ameeleza bayana kuwa, Marekani ndiyo chanzo cha kuvurugika amani katika eneo, na kwamba inapasa iache hatua zake hatarishi na za kichochezi.

Kuhusu madai hayo ya kuingia puto la China katika anga ya Marekani, Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya China amesema, "Marekani ilipotosha ukweli kuhusu tukio hilo, na hiyo inaashiria dhati ya ubeberu na ubabe wa Marekani."