China: Marekani ituondolee vikwazo iwapo inataka mazungumzo ya kijeshi
https://parstoday.ir/sw/news/world-i99340-china_marekani_ituondolee_vikwazo_iwapo_inataka_mazungumzo_ya_kijeshi
Beijing imesema serikali ya Rais Joe Biden wa Marekani sharti iiondolee China vikwazo iwapo inataka kufanyike mazungumzo ya ngazi ya juu ya kijeshi baina ya madola hayo mawili makubwa.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jun 30, 2023 03:24 UTC
  • China: Marekani ituondolee vikwazo iwapo inataka mazungumzo ya kijeshi

Beijing imesema serikali ya Rais Joe Biden wa Marekani sharti iiondolee China vikwazo iwapo inataka kufanyike mazungumzo ya ngazi ya juu ya kijeshi baina ya madola hayo mawili makubwa.

Liu Pengyu, Msemaji wa Ubalozi wa China mjini Washington amesema hayo na kufafanua kuwa, "Washington inajua mzizi wa ugumu wa mawasiliano ya kijeshi baina yake na Beijing. Sababu kuu ni vikwazo vya upande mmoja dhidi ya China."

Pengyu ameeleza bayana kuwa, vizingiti vya namna hivyo vinapaswa kuondolewa kabla ya kufanyika mabadilishano, mawasiliano na ushirikiano wa kijeshi baina ya mataifa hawa mawili.

Haijabainika aina ya vikwazo alivyokusudia Msemaji wa Ubalozi wa China mjini Washington, lakini maafisa wa Beijing wamekuwa wakitaka kuondolewa vikwazo dhidi ya Li Shangfu, Waziri wa Ulinzi wa Taifa wa China, alivyowekewa kwa kukataa kuzungumza na mwenzake wa Marekani, Lloyd Austin.

Aidha China imekuwa akiitaka Marekani ijiepushe na uraibu na tabia yake hiyo ya kuzishinikiza nchi nyingine zisizokubali kuburuzwa kwa kutumia vikwazo, mashinikizo na vitisho vya kutumia nguvu.

Hivi karibuni, Fu Cong, Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Kudhibiti Silaha katika Wizara ya Mambo ya China aliitaka Marekani iiondolee Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vikwazo haramu.

Marekani iko mstari wa mbele kuziwekea vikwazo nchi nyingine hasa Iran ili kujaribu kuizuia isifaidike kwa njia za amani na nishati muhimu sana ya nyuklia.