Jul 03, 2023 02:51 UTC
  • Waislamu duniani wazindua kampeni ya kususia bidhaa za Sweden

Waislamu katika mitandano ya kijamii wameanzisha kampeni kubwa ya dunia nzima ya kususia bidhaa zinazozalishwa na Sweden, kulalamikia kitendo kiovu cha kudhalilisha na kuvunjiwa heshima Qurani Tukufu nchini humo.

Kampeni hiyo imezinduliwa kufuatia mwito wa Kituo cha Kiislamu cha Al-Azhar cha Misri ambacho kimetaka kususiwa bidhaa za Uswidi ili kukabiliana na vitendo viovu vya kuvunjiwa heshima Qurani Tukufu katika mataifa ya Ulaya.

Al-Azhar imesema katika taarifa kuwa: Waislamu kote duniani hasa katika nchi za Kiarabu na Kiislamu wanapasa kususia bidhaa zote za Uswidi na kuchukua msimamo thabiti na wa umoja wa kuunga mkono Qurani yetu Tukufu, Maandiko Matakatifu ya Waislamu. 

Rais wa chama cha Istehkam-e-Pakistan (IPP), Abdul Aleem Khan amewapongeza Waislamu kote duniani kwa kuchangamkia kampeni hiyo ambayo imeshika kasi zaidi kwenye mtandao wa Twitter chini ya heshtegi #BoycottSwedishBrands (Susia Bidhaa za Sweden).

Hivi karibuni pia, wananchi wa Mauritania walitoa wito wa kukatwa uhusiano kati ya nchi za Kiislamu na Uswidi sanjari na kusisia bidhaa za nchi hiyo, kulalamikia kitendo hicho cha kuvunjiwa heshima Qurani Tukufu.

Aidha Mufti wa Oman, Sheikh Ahmad bin Hamad al Khalili, ametoa wito wa kususiwa bidhaa za Sweden kufuatia kuvunjiwa heshima Qurani Tukufu huko Sweden.

Jumatano ya Juni 28, raia wa Sweden kwa jina la Salwan Momika (37) alichoma moto na kuchana nakala ya Qurani Tukufu huko Stockholm mji mkuu wa nchi hiyo katika siku ya kwanza ya Sikukuu ya Idul-Adh'ha. Momika alitenda jinai hiyo baada ya polisi wa Sweden kumpa kibali cha kufanya maandamano dhidi ya Uislamu. 

Tags