Jul 09, 2023 02:38 UTC
  • Rosemary Anne DiCarlo
    Rosemary Anne DiCarlo

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Masuala ya Kisiasa, amehutubia kikao cha Baraza la Usalama cha kukagua utekelezwaji wa azimio nambari 2231, na kuelezea kuwa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA ndio chaguo bora zaidi la kuhakikisha "hali ya amani ya mpango wa nyuklia wa Iran."

Rosemary Anne DiCarlo amesema katika taarifa yake kwamba: "Disemba 2022, ambayo ilikuwa mara yangu ya mwisho kuripoti kwenye Baraza hili, pande zote kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na Marekani zilithibitisha kurudi kikamilifu katika utekelezaji madhubuti makubaliano hayo ndio chaguo pekee lililopo kwa ajili ya kutatua masuala yanayohusiana na mpango wa kuzalisha nishati ya nyuklia wa Iran.

Duru ya mwisho ya mazungumzo ya kuondoa vikwazo vilivyowekwa na nchi za Magharibi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilifanyika Vienna mwaka jana, lakini mazungumzo yalisimamishwa hapo baadaye. Katika uwanja huo Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Masuala ya Kisiasa anasema: "Diplomasia ndiyo njia pekee ya kushughulikia ipasavyo masuala ya mpango wa nyuklia wa Iran. Ni muhimu kwa pande zote kuanzisha tena mazungumzo haraka iwezekanavyo na kufikia makubaliano juu ya maswala yaliyosalia." DiCarlo amesisitiza kuwa: "Kuhusiana na hilo, narudia ombi la Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa Marekani la kuondolewa vikwazo au kutoa misamaha ya vikwazo hivyo kama ilivyoainishwa katika makubaliano ya JCPOA, na ninaomba kuongezwa muda wa misamaha inayohusiana na biashara ya mafuta na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran."

Rosemary Anne DiCarlo

Tarehe 8 Mei 2018, aliyekuwa rais wa Marekani, Donald Trump alitangaza rasmi kujitoa nchi hiyo katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA. Baada ya hatua hiyo, utawala wa Trump ulitupilia mbali utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa JCPOA na azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, licha ya upinzani mkubwa wa kimataifa, na akaiwekea Iran vikwazo visivyokuwa na kifani kwa shabaha ya kuishinikiza kukubali matakwa yake haramu. Trump pia alipinga mpango wowote wa kulindwa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.

Hatua hiyo ya Marekani ilikwenda kinyume kabisa na masharti ya JCPOA na Azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, na ilitegemea matakwa ya kidhalimu ya Washington na kwa lengo la kuzuia nchi nyingine zisiwe na ushirikiano wowote wa nyuklia na Iran. Utawala wa Trump ulidai kuwa kampeni ya mashinikizo ya juu kabisa ingeilazimisha Iran kusalimu amri kwa matakwa kumi na mbili ya Marekani, yaliyotolewa na Mike Pompeo, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mei 2018. 

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilitekeleza majukumu yake yote hadi mwaka mmoja baada ya kujitoa Marekani katika JCPOA, lakini baada ya hapo ikatangaza kuwa itapunguza utekelezaji wa majukumu hayo kwa kutegemea baadhi ya vipengee vya makubaliano hayo yenyewe.

Baada ya kuchukua hatua 5 za kupunguza utekelezaji wa majukumu yake, hatimaye Iran ilitangaza mnamo Januari 5, 2020 kwamba haitabana tena shughuli zake za kuzalisha nishati ya nyuklia.

Mnamo Septemba 2020, wakati wa kampeni za uchaguzi wa rais wa Marekani, Rais wa sasa wa nchi hiyo, Joe Biden, alikiri kwamba Donald Trump alifanya makosa kwa kujitoa katika JCPOA na kuchukua hatua kinyume na maslahi ya taifa la Marekani na kuifanya nchi hiyo itengwe zaidi. Hata hivyo, tangu mwanzoni mwa urais wake, yaani Januari 2021, kivitendo Biden ameendelea kutumia sera ya mashinikizo ya juu kabisa dhidi ya Iran; na bila kutaja ni nchi gani iliyojiondoa katika JCPOA, anasema kuchukua hatua Iran ndiyo sharti la Marekani kurejea katika mapatano hayo. Biden Ameahidi kwamba iwapo Iran itarejea katika utekelezaji kamili wa JCPOA, Washington nayo itarejea katika mapatano hayo.

Joe Biden

Joseph Cirincione, mtaalamu wa masuala ya kisiasa wa Marekani anasisitiza kuwa hadi hivi sasa Biden ameendeleza kampeni ya Trump ya mashinikizo makubwa dhidi ya Iran bila mafanikio na kusema: "Biden asiporekebisha mwenendo wake, kuna hatari ya kupoteza mapatano hayo muhimu ya nyuklia. Kinyume na mtazamo usio wa kimantiki wa serikali ya Biden, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetangaza kuwa "itarejea katika utekelezaji wa JCPOA pale Marekani itakapofuta vikwazo vyote kivitendo, si kwa maneno au kwenye karatasi."

Ingawa Rais Joe Biden wa Marekani aliahidi kabla ya uchaguzi wa rais wa mwezi Novemba 2020 kuirejesha nchi hiyo katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, na baada ya kuchaguliwa aliendelea kutoa ahadi na matamshi hayo. lakini ushahidi wa mienendo na misimamo ya Washington vinaonyesha kuwa kimsingi Marekani haikusudii kurejea kwenye JCPOA ya 2015. Caitlin Johnstone, mwandishi wa habari wa Australia, anasema: "Sera ya Biden kuhusiana na Iran ni sawa na sera za Trump mkabala wa Jamhuri ya Kiislamu."

Nukta muhimu ni kuwa licha ya kwamba Marekani imejitoa katika JCPOA, lakini wakati huo huo haina nia ya kutangaza kifo cha makubaliano hayo ya nyuklia na kuingia katika "ulimwengu usio na JCPOA". Kwa hivyo, mazungumzo ya JCPOA hayatatangazwa kuwa yamefikia mwisho na kugonga mwamba. Wakati huo huo, tangazo rasmi la Umoja wa Mataifa kuhusu ulazima wa kuondolewa vikwazo vya upande mmoja vya Marekani dhidi ya Iran ili kurejesha mapatano ya JCPOA linaonyesha msimamo wa shirika hilo la kimataifa kuhusu sharti muhimu la kurejea JCPOA katika mkondo wake madhubuti na sahihi.

Tags