Jul 28, 2023 02:24 UTC
  • Leo katika Historia, Ijumaa tarehe 28 Julai, mwaka 2023

Leo ni tarehe 10 Muharram 1445 Hijria sana na Julai 28 mwaka 2023.

Katika siku kama hii ya leo miaka 1384 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, moja kati ya vita mashuhuri katika historia ya Uislamu na mwanadamu, vilitokea baina ya majeshi ya haki na majeshi ya batili katika ardhi ya Karbala huko Iraq. Siku hii inajulikana kwa jina la A'shuraa. Katika siku hiyo mjukuu wa Mtume Muhammad (saw), Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib AS, alisimama kishujaa na wafuasi wake waaminifu 72, kukabiliana na jeshi la batili ili kuilinda dini ya Allah SW.

Hamasa ya Karbala ilikuwa dhihirisho la mambo mawili makuu. Kwanza ni ujasiri, ushujaa, moyo wa kujitolea, uaminifu pamoja na kuyapokea kwa moyo mkunjufu mauti ya kuuawa shahidi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, sifa walizojipamba nazo wapiganaji wachache wa jeshi la haki wakiongozwa na Imam Hussein AS dhidi ya Yazid bin Muawiya. Pili ni upeo wa ukatili, udhalimu na unyama ulioonyeshwa na jeshi batili la Yazid bin Muawiya.

Baada ya kupambana kishujaa, hatimaye mjukuu huyo wa Mtume Muhammad (saw) aliuawa shahidi katika siku kama ya leo akiwa pamoja na watu wengine wa familia ya Mtume (saw), na wafuasi wake waaminifu.

Tarehe 28 Julai miaka 294 iliyopita harakati ya kwanza ya mapambano ya watumwa weusi wa Marekani ilianza huko kaskazini mwa nchi hiyo. Waanzilishi wa harakati hiyo ambao walikuwa watu 44 walimuua kila mzungu waliyekutana naye katika njia yao kutoka Carolina Kusini kuelekea Florida. Lakini walizingirwa na jeshi la Waingereza na kuuawa kabla ya kuingia Florida na kupata uhuru. Baada ya hapo watumwa weusi waliendeleza mapambano ya ukombozi na kupigania haki zao za kiraia. Watumwa weusi walikuwa wakitekwa nyara au kununuliwa kutoka Afrika tangu mwanzoni mwa karne ya 17 na kupelekwa Marekani kwa ajili ya kuuzwa na kufanyishwa kazi kwa mabwana zao.

Harakati ya watumwa weusi Amerika ya Kaskazini

Siku kama ya leo miaka 202 iliyopita, nchi ya Peru ilijipatia uhuru wake na siku hii hutambuliwa kuwa ni siku ya kitaifa nchini humo. Peru ilikuwa sehemu ya asili ya watu waliostaarabika wa Inca na tokea karne ya 12 hadi ya 16 ufalme wa watu hao ndio uliotawala kaskazini magharibi mwa Amerika ya Kusini. Mwanzoni mwa karne ya 16 wakoloni wa Uhispania waliingia Peru na baada ya mauaji ya kikatili dhidi ya Wahindi wekundu hatimaye ardhi ya Peru ikatawaliwa na wakoloni wa Uhispania. Wahispania waliendelea kuikalia kwa mabavu ardhi hiyo sambamba na kupora mali na raslimali za watu wa Peru hali iliyopelekea kupamba moto mapinduzi ya wapigania uhuru nchini humo. Peru iko kaskazini magharibi mwa Amerika ya Kusini, huku ikipakana na nchi za Ecuador, Colombia, Chile, Brazil na Bolivia.   

Bendera ya Peru

Siku kama ya leo miaka 145 iliyopita, kulitiwa saini mkataba wa kihistoria wa Barlin, mwishoni mwa kongamano lililofanyika mjini humo kati ya wajumbe wa nchi za Russia, Ujerumani, Ufaransa, Uingereza na Austria. Mkutano wa Berlin ulifanyika kwa ombi la kansela wa wakati huo wa Ujerumani Otto Von Bismarck. Kutiwa saini mkataba huo kuliifanya Ujerumani kuwa na satua ya kisiasa na kijeshi na kuandaa uwanja wa kujitanua zaidi nchi hiyo. Kimsingi kutiwa saini mkataba huo wa Berlin kulikuwa moja ya mambo yaliyoandaa uwanja wa kutokea Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia. 

Mkutano wa Berlin

Miaka 109 iliyopita, wakati wa kukaribia kuanza Vita vya Kwanza vya Dunia, utawala wa kifalme wa Austria ulitangaza vita dhidi ya serikali ya Serbia kwa kisingizio cha kuuawa mrithi wa kiti cha ufalme wa nchi hiyo huko Serbia. Hata hivyo sababu kuu ya kutolewa tangazo hilo la vita ilikuwa ni upinzani wa wananchi wa Serbia dhidi ya uingiliaji wa Austria katika masuala ya ndani ya nchi yao na pia kufanyika uasi dhidi ya nchi hiyo. 

Siku kama ya leo miaka 47 iliyopita, tetemeko kubwa liliukumba mji wa Tangshan mashariki mwa China. Tetemeko hilo ambalo lilikuwa na ukubwa wa rishta 7.8, lilipelekea kuuawa watu wapatao laki sita na malaki kadhaa ya wengine kujeruhiwa sambamba na kuwa wakimbizi. Hata hivyo ripoti rasmi iliyotangazwa na viongozi wa China ilionyesha kuwa, idadi ya watu waliouawa katika tetemeko hilo ilikuwa laki mbili na 40 elfu. Hilo lilikuwa tetemeko kubwa zaidi kuwahi kuikumba China katika karne ya 20 na tetemeko kubwa kushuhudiwa tangu tetemeko la mwaka 1556 ambalo lilipelekea kuuawa kwa watu laki nane na elfu 30.