Sura ya Adh-dhaariyaat, aya ya 38-46 (Darsa ya 957)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.
Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 957 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 51 ya Adh-Dhaariyaat. Tunaianza darsa yetu ya leo kwa aya yake ya 38 hadi ya 40 ambazo zinasema:
وَفِي مُوسَىٰ إِذْ أَرْسَلْنَاهُ إِلَىٰ فِرْعَوْنَ بِسُلْطَانٍ مُّبِينٍ
Na katika (khabari) za Musa (ziko alama na mazingatio pia), tulipo mtuma kwa Firauni na hoja wazi kabisa.
فَتَوَلَّىٰ بِرُكْنِهِ وَقَالَ سَاحِرٌ أَوْ مَجْنُونٌ
Lakini akakengeuka kwa sababu ya nguvu zake na akasema: Huyu ni mchawi au mwendawazimu!
فَأَخَذْنَاهُ وَجُنُودَهُ فَنَبَذْنَاهُمْ فِي الْيَمِّ وَهُوَ مُلِيمٌ
Basi tukamkamata yeye na majeshi yake na tukawatupa baharini, na yeye ndiye wa kulaumiwa.
Katika darsa iliyopita tulisoma aya zilizozungumzia adhabu iliyowashukia watu mafasiki wa kaumu ya Nabii Lut’ AS. Aya hizi zimegusia hatima ya Firauni na wafuasi wake na kueleza kwamba: alipoanza kutangaza wito wake wa Utume, Nabii Musa AS alimuendea kwanza Firauni kabla ya kuwalingania watu wa kaumu yake ya Bani Israili. Kwa sababu wakati ule taghuti huyo alikuwa akiwakandamiza na kuwanyongesha watu wa kaumu hiyo kwa kuwatesa na kuwanyanyasa wanaume na wanawake na kuwageuza watumwa na wajakazi wake. Kwa hivyo, ili kuikomboa kaumu ya Bani Israili kwa kuitoa kwenye makucha ya Firauni, Nabii Musa AS alimwendea kwanza taghuti huyo na akamthibitishia ukweli wa Utume wake kwa kumuonyesha miujiza na hoja madhubuti na za mantiki alizopewa na Mola wake. Lakini Firauni na wapambe wake hawakuubali wito wa haki waliolinganiwa. Walimwita Nabii Musa AS mchawi na mfanyamazingaombwe na kumtuhumu kuwa ni punguani na mwendawazimu. Lakini mwisho wa yote, adhabu ya Mwenyezi Mungu ilimnyakua Firauni na watu wake wakiwa hawana njia wala popote pa kukimbilia. Wote waligharikishwa ndani ya Mto Nile na kuishia kulaaniwa na umma na mataifa mbalimbali katika zama zote za historia. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, kuwakomboa watu kwa kuwatoa kwenye makucha na minyororo ya majabari na madhalimu ni mojawapo ya malengo ya harakati ya Mitume. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, watawala waovu na mafisadi huwachafulia majina yao na kuwavurumishia tuhuma za kuwaita wapotofu, wachawi au wendawazimu waja wema wa Allah wanaosimama kupambana kwa lengo la kurekebisha masuala ya jamii. Vilevile aya hizi zinatutaka tujue kwamba madola makubwa, nguvu zao na suhula zao zote yalizonazo ni dhaifu mno na si lolote si chochote mbele ya irada ya Allah Jalla Jalaaluh; kwa hivyo tunatakiwa tumtegemee na kutawakali kwake Yeye Mola na wala tusiwe na chembe ya woga wa kuyahofu madola hayo.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 41 na 42 za sura yetu ya Adh-Dhaariyaat ambazo zinasema:
وَفِي عَادٍ إِذْ أَرْسَلْنَا عَلَيْهِمُ الرِّيحَ الْعَقِيمَ
Na katika (khabari za) A'di (ziko alama na mazingatio pia) tulipo wapelekea upepo wa kukata uzazi, uangamizao.
مَا تَذَرُ مِن شَيْءٍ أَتَتْ عَلَيْهِ إِلَّا جَعَلَتْهُ كَالرَّمِيمِ
Haukuacha chochote ulicho kifikia ila ulikifanya kama mfupa uliooza.
Nabii Hud AS ni Mtume aliyepelekwa kwa watu wa kaumu ya A’di; watu ambao walikuwa wakiishi kusini mwa Bara Arabu. Kwa upande wa kimwili, watu wa kaumu ya A’di walikuwa na nguvu sana, warefu wa vimo na wenye maungo mapana na makubwa mno. Watu hao walikuwa na ustadi mkubwa na weledi wa aina yake wa kujenga majengo makubwa na marefu kwenye majabali na milima. Lakini badala ya kuwaamini na kuwafuata Mitume wa Mwenyezi Mungu, walikuwa wakiwatii watawala madhalimu na majabari na kusimama kuipinga haki mpaka Allah SWT akawateremshia adhabu kali ya maangamizi. Upepo mkali sana wa kimbunga uliwavumia, ukawapeperusha na kuwapiga na ardhi mithili ya mabua na majani makavu. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, upepo, ambao ni dhihirisho la rehma za Mwenyezi Mungu kutokana na kuyasukuma mawingu kutoka sehemu moja hadi nyingine na kupelekea kunyesha mvua inayootesha mimea na miti, wakati mwingine huwa dhihirisho la ghadhabu za Mwenyezi Mungu kwa kuleta uharibifu mkubwa wa kuwahilikisha na kuwaangamiza waovu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, maji na upepo ni miongoni mwa vitu vya kimaumbile, lakini vinafanya kazi kwa amri ya Allah SWT; na kwa irada yake Yeye Mola huwagharikisha na kuwaangamiza madhalimu.
Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 43 hadi 46 ambazo zinasema:
وَفِي ثَمُودَ إِذْ قِيلَ لَهُمْ تَمَتَّعُوا حَتَّىٰ حِينٍ
Na katika (khabari za) Thamudi (ziko alama na mazingatio pia) walipo ambiwa: Stareheni kwa muda mdogo tu.
فَعَتَوْا عَنْ أَمْرِ رَبِّهِمْ فَأَخَذَتْهُمُ الصَّاعِقَةُ وَهُمْ يَنظُرُونَ
Wakaasi amri ya Mola wao Mlezi. Basi uliwanyakua moto wa radi na huku wanaona.
فَمَا اسْتَطَاعُوا مِن قِيَامٍ وَمَا كَانُوا مُنتَصِرِينَ
Basi hawakuweza kusimama wala hawakuweza kujipigania.
وَقَوْمَ نُوحٍ مِّن قَبْلُ ۖ إِنَّهُمْ كَانُوا قَوْمًا فَاسِقِينَ
Na kaumu ya Nuhu (tuliiangamiza) kabla (yao). Hakika hao walikuwa watu mafasiki.
Nabii Saleh AS alikuwa Mtume wa kaumu ya Thamudi. Watu wa kaumu hiyo walimtaka Nabii wao huyo awaonyeshe muujiza wa ajabu ili kuthibitisha ukweli wa Utume wake. Muujiza wenyewe ni kumtoa kwenye jabali ngamia aliye hai! Nabii Saleh AS aliwapa indhari watu wake kwa kuwaambia: ikiwa hilo litathibiti na nyinyi mkaikataa na kuikadhibisha haki mjue kwamba mtaangamizwa. Lakini watu wa kaumu ya Thamudi, waliendelea kung’ang’ania takwa lao wakidhani kwamba muujiza kama huo hauwezi kutokea. Kwa qudra ya Allah SWT ngamia mwenye maungo makubwa alitoka jabalini; lakini badala ya kaumu ya Thamudi kuamini na kumkubali Nabii Saleh AS kuwa ni Mtume wa haki, walimkadhibisha na kuamua kumuua ngamia yule wa muujiza. Licha ya kumuua ngamia, watu wa Thamudi walipewa muhula wa siku tatu ili watubie, lakini hawakukubali katu kufanya hivyo; na hatima yao ikawa ni kupigwa na moto wa radi kali uliowasambaratisha, wakashindwa kuinuka na kuomba msaada. Halikadhalika, licha ya jitihada kubwa za miaka na miaka zilizofanywa na Nabii mteule wa Allah Nuh AS za kuwalingania na kuwaelekeza watu wake kwenye uongofu, ni wachache tu miongoni mwao waliikubali haki, na akthari yao walikufuru na kuendeleza maovu na maasi waliyokuwa wakifanya, mpaka mwishowe, wao pia wakaangamizwa na tufani kubwa ya gharika na mafuriko. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, kanuni na utaratibu thabiti aliouweka Allah ni kuwapa watu waovu muhula na fursa ya kutubu. Wasipofanya hivyo, hufikwa na adhabu hapa duniani au huko akhera. Funzo jegine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, watu wa kaumu na mataifa wasiopata ibra na mazingatio kwa yaliyozisibu kaumu na umma zilizopita wakarekebisha mwenendo wao, wao wenyewe watakuwa somo la mazingatio kwa watakaokuja baada yao. Wa aidha aya hizi zinatutaka tujue kwamba, vitu vyote vya kimaumbile yakiwemo maji, upepo na moto wa radi vinaweza kuwa madhihirisho ya ghadhabu za Mwenyezi Mungu na kupelelekea kuangamizwa kaumu ya watu waovu na mafasiki. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 957 ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atutakabalie toba zetu, atusamehe madhambi yetu na aufanye mwema mwisho wetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/