Aug 13, 2023 15:28 UTC
  • Sura ya At-T’uur, aya ya 13-21 (Darsa ya 961)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 961 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 52 ya At-T’uur. Tunaianza darsa yetu ya leo kwa aya yake ya 13 hadi 16 ambazo zinasema:

يَوْمَ يُدَعُّونَ إِلَىٰ نَارِ جَهَنَّمَ دَعًّا

Siku watapo sukumwa kwenye Moto kwa msukumo wa nguvu, 

هَٰذِهِ النَّارُ الَّتِي كُنتُم بِهَا تُكَذِّبُونَ

(Waambiwe): Huu ndio ule Moto mlio kuwa mkiukanusha!

أَفَسِحْرٌ هَٰذَا أَمْ أَنتُمْ لَا تُبْصِرُونَ

Je! Huu ni uchawi, au hamwoni tu?

اصْلَوْهَا فَاصْبِرُوا أَوْ لَا تَصْبِرُوا سَوَاءٌ عَلَيْكُمْ ۖ إِنَّمَا تُجْزَوْنَ مَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ

Uingieni, mkistahamili au msistahamili - ni mamoja kwenu. Hakika mnalipwa kwa mliyo kuwa mkiyatenda. 

Moja ya silaha waliyokuwa wakiitumia wapinzani wa Mitume ilikuwa ni kuituhumu miujiza iliyokuwa ikifanywa na Manabii hao wa Allah kwamba ni uchawi na mazingaombwe na wakawa wanasema: ni kama kwamba wanayaroga na kuyafanyia sihiri macho yetu kwa kuweka utando juu yake ili tusiweze kubaini uhakika wa mambo wanayofanya. Katika aya tulizosoma, Qur’ani inasema: Wakati watakapouona moto wa Jahannamu kwa macho yao na kuuhisi muunguzo wake, wataambiwa: Haya je ni uchawi na mazingaombwe! na macho yenu yanaona kimakosa kuwa ni Moto? Wapinzani na wakadhibishaji hao wa Mitume wa Mwenyezi Mungu walikuwa wakiwaambia kwa inadi, ubishi na ukaidi Mitume wao: ni mamoja tu mkituonya au msituonye, hayo mtuambiayo hayatuathiri chochote na wala sisi hatuyajali hayo mawaidha yenu. Aya hizi zinawaambia: Siku ya Kiyama pia wao wataambiwa: ni mamoja tu na hakuna tofauti yoyote ikiwa mtauvumilia Moto au mtaguna na kulalama, kwani hamuna njia yoyote ya kuiepuka adhabu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, matokeo ya ubishi, inadi na ukaidi mbele ya haki ni kufikwa na adhabu kali na nzito. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa adhabu za Kiyama ni za haki na uadilifu na ni matokeo ya amali na matendo ya mtu mwenyewe. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, kuzidunisha na kuzifanyia stihzai thamani safi na takatifu za dini hapa duniani kutafuatiwa na udhalilishaji na stihzai kwa mfanyaji wake Siku ya Kiyama.

Ifuatayo sasa ni aya ya 17 hadi ya 19 ya sura yetu ya At-T’uur ambazo zinasema:

 إِنَّ الْمُتَّقِينَ فِي جَنَّاتٍ وَنَعِيمٍ

Hakika wachamngu watakuwa katika Mabustani na neema, 

فَاكِهِينَ بِمَا آتَاهُمْ رَبُّهُمْ وَوَقَاهُمْ رَبُّهُمْ عَذَابَ الْجَحِيمِ

Wakifurahia yale aliyo wapa Mola wao Mlezi. Na Mola wao Mlezi atawalinda na adhabu ya Motoni.

كُلُوا وَاشْرَبُوا هَنِيئًا بِمَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ

Kuleni na kunyweni kwa raha kabisa kwa sababu ya mliyo kuwa mkiyatenda. 

Moja ya mbinu zinazotumiwa na Qur’ani katika kuwalingania watu ni kufuatanisha pamoja hofu na tamaa, na maonyo na bishara njema ili mtu yeyote yule asikate tamaa ya kupata rehma za Allah SWT na kwa upande mwingine asiujaze moyo wake matarajio ya kupindukia na yasiyo na maana. Katika muendelezo wa yaliyozungumziwa katika aya zilizopita zilizobainisha adhabu itakayowafika motoni makafiri na wakadhibishaji wa haki, aya hizi tulizosoma zinaashiria malipo ya thawabu watakayolipwa Peponi waja waliojitakasa na maovu wakamcha Mwenyezi Mungu na kueleza kwamba: Watu wa Peponi watakuwa na furaha kwa namna mbili. Ya kwanza ni ya kutunukiwa atiya na neema zisizohesabika ambazo Allah SWT ameziweka kwa ajili yao; na ya pili ni kupata rehma na fadhila zake Mola zitakazopelekea wao wasamehewe makosa yao na kuepushwa na adhabu ya Moto. Watu wa Peponi, nao pia kama walivyo wa Motoni wataona katika ulimwengu huo wa akhera matokeo ya amali zao. Ukubwa na uzito wa adhabu na thawabu watakazolipwa watu na Allah utategemea ukubwa na udogo wa amali zao njema na mbaya walizofanya duniani pamoja na athari zake. Miongoni mwa tunayojifunza kutokana na aya hizi ni kwamba, ufunguo wa Pepo ni usafi wa nafsi, uchamungu na kujitakasa na maovu. Kuwa na imani peke yake hakutoshi na hakusaidii, bila ya taqwa na kumcha Mola. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa mtu yeyote anayekuwa na taqwa hapa duniani itakayomfanya aichunge na kuiepusha nafsi yake na machafu na maovu, Siku ya Kiyama Allah SWT atamuepusha na yeye pia na adhabu ya Moto. Vilevile aya hizi zinatutaka tutambue kwamba Pepo haipatikani vivi hivi bila kuigharimikia. Ni kama alivyonena malenga mashuhuri wa Kiswahili Shaaban Robert: Bila dhiki hutukuki na bila usumbufu huwi mtukufu.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 20 na 21 za sura yetu ya At-T’uur ambazo zinasema:

مُتَّكِئِينَ عَلَىٰ سُرُرٍ مَّصْفُوفَةٍ ۖ وَزَوَّجْنَاهُم بِحُورٍ عِينٍ

Watakuwa wameegemea viti vya enzi vilivyo pangwa kwa safu. Na tutawaoza mahuru-l-aini.

وَالَّذِينَ آمَنُوا وَاتَّبَعَتْهُمْ ذُرِّيَّتُهُم بِإِيمَانٍ أَلْحَقْنَا بِهِمْ ذُرِّيَّتَهُمْ وَمَا أَلَتْنَاهُم مِّنْ عَمَلِهِم مِّن شَيْءٍ ۚ كُلُّ امْرِئٍ بِمَا كَسَبَ رَهِينٌ

Na walio amini, na dhuriya zao wakawafuata kwa Imani, tutawakutanisha nao dhuriya zao, na wala hatutawapunja hata kidogo katika (thawabu za)  amali zao. Kila mtu atafungika na (amali) alizozichuma.

Aya hizi zinagusia fadhila na rehma zingine za Allah kwa watu wa Peponi na kueleza kwamba: Watu wa Peponi watapata neema ya kujuana na kusuhubiana na waja wema na waliotakasika na watakuwa na majlisi na vikao vya raha na furaha. Mwenyezi Mungu Mtukufu amewawekea wake safi na wazuri wa kustaajabia. Kwa wanaume waumini, wamewekewa wanawake wazuri na jamili; na wanawake waumini wametengewa wanaume waliopambika kwa ukamilifu; na baina yao yatajengeka mazoea na mafungamano na kupeana utulivu wao kwa wao. Bali si hasha pia wanawake na wanaume waumini ambao hapa duniani waliishi pamoja katika mema na furaha, huko akhera pia wakaendelea kuishi pamoja maisha ya mke na mume. Kwa upande wa watoto walio waumini, nao pia wataungana na wazazi wao ili kukamilisha familia yao ya Peponi na kuwafanya wazidi kuwa na hali na mambo yatakayowaongezea furaha na ukunjufu wa nyoyo. Na tab’an kwa rehma na fadhila zake, Allah SWT atayafumbia macho baadhi ya mapungufu ya amali za watoto hao ili waweze kufikia daraja za wazazi wao na kuwa pamoja nao katika maisha hayo ya milele ya huko akhera. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, huko Peponi pia staha, heshima na mipaka ya maingiliano ya watu kimwili itazingatiwa; na mahusiano kati ya mwanamke na mwanamme yatakuwa ya kindoa, si maingiliano ya kiholela. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, wale ambao hapa duniani walijichunga na kujiepusha na kuwatazama kimatamanio wale wasio maharimu zao, huko akhera watakuwa na wake jamili na wa kuvutia mno. Aidha aya hizi zinatutaka tufahamu kwamba uumini ndicho kigezo cha kutumia katika kufunga ndoa na kujenga familia katika Uislamu; kwa hivyo wanandoa na watoto wao walio waumini watakuwa pamoja huko Peponi pia. Halikadhalika aya hizi zinatuelimisha kuwa, hitajio la kuwa na mke au mume na hamu ya kuwa na mtoto ni kitu kilichomo ndani ya maumbile ya mtu. Kwa sababu hiyo, huko Peponi hitajio hilo la kimaumbile na kifitra la mwanadamu limezingatiwa pia. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 961 ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atujaalie mwisho mwema, na akatukutanishe Peponi na wazazi wetu, wake na waume zetu pamoja na vizazi vyetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/

 

Tags