Aug 22, 2023 02:34 UTC
  • Jumanne, 22 Agosti, 2023

Leo ni Jumanne tarehe 5 Safar 1445 Hijria sawa Agosti 22 mwaka 2023.

Siku kama ya leo miaka 1384 iliyopita Ruqayyah binti mdogo wa Imam Hussein bin Ali (as) alikufa shahidi akiwa huko Sham kwa mtawala dhalimu Yazid bin Muawiyya. Ruqayyah ambaye pia anajulikana kwa jina la Fatima binti Hussein (as) alikuwa binti wa mwisho wa mjukuu huyo wa Mtume (saw) kutoka kwa mkewe, Ummu Is’haq binti Twalha. Wanahistoria wanasema mtoto huyo alikuwa na umri wa miaka 3, 4 au 7. Mtoto huyo alikuwa akimpenda sana Imam Hussein na aliandamana naye pamoja na familia yake katika medani ya Karbala. Baada ya kuuawa shahidi baba yake, ndugu na masahaba wa Imam, Ruqayya alikamatwa mateka na askari wa Yazid akiwa pamoja na watu wengine wa Nyumba ya Mtume na kupelekwa Sham. Huko alikuwa akilia mchana usiku. Wahistoria wanasema mtawala Yazidi aliamuru kichwa cha Imam Hussein kipelekwe na kutupwa mbele ya binti huyo mdogo ambaye alilia na kuzimia kisha akakata roho.

Katika siku kama ya leo miaka 396 iliyopita vilijiri vita vya mwisho vya La Rochelle kati ya Wakatoliki na Waprotestanti wa Ufaransa. Vita hivyo vilianza baada ya Waprotestanti kuchochewa na Uingereza. Wakatoliki ambao walikuwa wakiungwa mkono na vikosi vya jeshi la serikali ya Ufaransa chini ya uongozi wa Richelieu, Kansela mashuhuri wa nchi hiyo, walipigana vita na Waprotestanti ambao walikuwa wakipigania maeneo yao katika bandari ya La Rochelle. Vita hivyo vilimalizika baada ya mwaka mmoja kwa kupata ushindi Wakatoliki na kutekwa La Rochelle.

Miaka 325 iliyopita katika siku kama ya leo, mkataba wa pande tatu wa Russia, Poland na Denmark ulitiwa saini dhidi ya Sweden. Wafalme wa nchi hizo tatu walikuwa na lengo la kumuangusha Karl XII mfalme kijana wa Sweden ili kuikalia kwa mabavu nchi hiyo. Ni kwa msingi huo ndipo miaka miwili baadaye mnamo mwezi Aprili mwaka 1700 Miladia nchi wanachama wa mkataba huo wa pande tatu zikaamua kuishambulia Sweden, hata hivyo jeshi la mfalme Karl XII likakabiliana vilivyo na kutoa pigo kwa nchi vamizi.  Baada ya kufikia mapatano na Denmark, mwaka 1704 akaishambulia Poland na kuikalia kwa mabau. Hata hivyo mashambulio ya Sharel dhidi ya Russia hayakuzaa matunda.

Mfalme Karl XII wa Sweden

Siku kama ya leo miaka 163 iliyopita Paul Gottlieb Nipkow mmoja wa wavumbuzi wa televisheni alizaliwa huko Ujerumani. Nipkow alikulia katika familia maskini, lakini juhudi na irada kubwa ilimuwezesha kuendeleza masomo yake ya fizikia hadi chuo kikuu. Paul Gottlieb Nipkow alifanya utafiti mkubwa na hatimaye alifanikiwa kuvumbua transimita ya televisheni. Chombo hicho kilichobuniwa na Nipkow kiliweza kurusha mawimbi ya televisheni katika umbali wa mita 30 na baadaye transimita iliyotengenezwa na mvumbuzi huyo wa Kijerumani ilikamilishwa na wabunifu wengine.

Na miaka 159 iliyopita katika siku kama hiii ya leo, mkataba wa kihistoria wa Geneva ulitiwa saini baina ya nchi kadhaa za Ulaya, Asia na Amerika. Lengo la mkataba huo lilikuwa ni kuwasaidia majeruhi katika medani za vita.  Kwa mujibu wa mkataba huo, timu za madaktari, watoaji misaada na zana zao zinapaswa kutoegemea upande wowote na zisishambuliwe bali zibakie katika amani wakati wa vita. Mbunifu wa mkataba huo alikuwa Henry Dunant raia wa Uswisi.