Hikma za Nahjul Balagha (26)
Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Karibuni katika sehemu hii ya 26 ya mfululizo wa makala hizi fupifupi za Hikma za Nahjul Balagha. Leo pia tutaangalia kwa muhtasari hikma nyingine za Imam Ali bin Abi Talib AS kama ilivyonukuliwa kwenye kitabu cha Nahjul Balagha tukiwa na matumaini mtakuwa nasi hadi mwisho wa kipindi. Hii ni Hikma ya 26.
مَا أَضْمَرَ أَحَدٌ شَیْئاً إِلَّا ظَهَرَ فِی فَلَتَاتِ لِسَانِهِ وَ صَفَحَاتِ وَجْهِهِ
Hakudhamiria mtu yeyote chochote, ila kitu hicho hudhihirika kwenye ncha za maneno yake na kipaji cha uso wake.
Katika Hikma hii ya 26 ya Nahjul Balagha, Imam Ali AS anaashiria moja ya kanuni muhimu za saikolojia akisema:
مَا أَضْمَرَ أَحَدٌ شَیْئاً إِلَّا ظَهَرَ فِی فَلَتَاتِ لِسَانِهِ وَ صَفَحَاتِ وَجْهِهِ
Hakudhamiria mtu yeyote chochote, ila kitu hicho hudhihirika kwenye ncha za maneno yake na kipaji cha uso wake.
Kama mnavyojua wasikilizaji wapenzi, tabia na matendo ya mwanadamu ni dhihirisho la matakwa na nia zake ambazo hazifichiki bali huwa zinafunuliwa kimaumbile. Sehemu ya tabia hiyo ni uamuzi wa mtu wa kukimbia wakati wa khofu na tabia nyingine ni kusawijika uso na kutetemeka mkono wakati akiwa na ghadhabu.
Lakini wakati mwingine hutokea kwamba mtu huficha kitu ndani ya moyo na nafsi yake ambacho hataki mtu yeyote ajue. Kwa hivyo, utaona kuna aina fulani ya undumilakuwili baina ya maneno na matendo kwa upande mmoja na yale yanayompitikia ndani ya nafsi na moyo wake kwa upande wa pili.
Ikiwa mtu atakuwa mwangalifu kabisa juu ya matendo na maneno wake, huenda akaweza kuficha undumilakuwili wake huo baina ya dhahiri na batini yake, lakini akighafilika na kujisahau kidogo hufedheheka na kushitukia vitendo na maneno yake yanamuumbua kwa kufichua yanayoptikiana ndani ya nafsi yake.
Hii ni kanuni muhimu katika elimu ya saikolojia na ndiyo inayotumiwa sana kuwafanya wahalifu wengi wakiri uhalifu wao na kudumba na kufichua kile walichojaribu kuficha. Unafiki wa wanafiki pia kwa kawaida hufichuka kwa sura hiyo hiyo. Aya za 29 na 30 za Sura tukufu ya Muhammad zinasema: Je! Wenye maradhi nyoyoni mwao wanadhani kwamba Mwenyezi Mungu hatazidhihirisha chuki zao? Na tungelipenda tungelikuonyesha hao na ungeliwatambua kwa alama zao; lakini bila ya shaka utawajua kwa namna ya msemo wao. Na Mwenyezi Mungu anavijua vitendo vyenu..
Naam, bila ya shaka yoyote, Mwenyezi Mungu anavijua vitendo vyote vya viumbe Wake na lau angependa, angeweza kumfichua mmoja mmoja ndani ya Qur'ani Tukufu lakini hapo hapo Qur'ani inaliashiria suala hili kwamba, dalili za watu hao zinaonekana kwenye maneno na matendo yao.
Tab'an, kama ambavyo wanafiki na wahalifu wanaweza kutambuliwa kwa maneno yao ya kujigonga na yaliyojaa makosa au kwa rangi ya nyuso zao, watu wema na waumini wa kweli nao wanaweza kujulikana kwa njia hiyo hiyo. Katika sehemu moja ya aya ya 29 ya Surat Fat'h, Mwenyezi Mungu anawazungumzia waumini wake na jinsi tunavyoweza kuwatambua kwa kusema: Alama zao zi katika nyuso zao, kwa athari ya kusujudu.
Tab'an ni muhimu kutaja hapa kwamba athari ya kusujudu haimaanishi mabaka meusi ya sijda kwenye vipaji vya uso, bali ina maana kwamba nyuso zao zinang'ara, zinaonesha kuridhika, zina mvuto, zina utulivu, mtu ukiwaangalia unahisi kuwa na amani maalum ambayo yote hayo ni matunda ya usafi na ikhlasi zao katika ibada.