Sep 11, 2023 07:12 UTC
  • Ulimwengu wa Michezo

Haya ni baadhi ya matukio yaliyoshudiwa katika viwanja vya spoti katika kona mbalimbali za dunia ndani ya siku saba zilizopita.

Taekwondo: Iran yang'aa Lebanon

Timu za taifa za wanawake na wanaume za taekwondo za Iran zimeibuka za kwanza na pili kwa usanjari huo katika Mashindano ya Ubingwa wa Asia ya Makurutu wa Kijeshi huko Beirut, mji mkuu wa Lebanon. Timu ya wanawake ya Iran imeibuka kidedea baada ya kutwaa medali 5 za dhahabu, 2 fedha na moja ya shaba katika mashindano hayo yaliyofanyika baina ya Septemba 6 na 8. Kazakhstan imeibuka ya pili huku Korea Kusini ikifunga orodha ya tatu bora. Wanataekwondo 213 kutoka nchi 23 wameshiriki mashindano hayo ya bara Asia. Mahboobeh Mohammadnejad, mkufunzi mkuu wa timu ya wanawake wa Iran amebeba taji la kocha bora barani Asia, huku Muirani Mohammad Taherinasab akiteuliwa kuwa refa bora kwenye mashindano hayo.

Rais Ebrahim Raisi wa Iran amewapongeza wanataekwondo hao wa Kiirani kwa kung'ara kwenye mashindano hayo ya kibara na kuiweka Iran katika ramani ya dunia kwa mara nyingine tena. Katika ujumbe wake wa tahania ambapo pia amewapongeza makocha na mabenchi ya ufundi ya timu hizo za Iran, Sayyid Raisi amesema: Ushindi huo ni nembo iliyo wazi inayoashiria taifa lenye nguvu na izza, na ambalo daima linajitahidi na kujituma ili kuwapa furaha Wairani. Wakati huohuo, timu za taekwondo za walemavu za wanaume na wanawake za JKI zimetwaa ubingwa wa mashindano hayo ya bara Asia yanayofahamika kama parataekwondo. Timu ya wanawake imeibuka mshindi kwa kuzoa medali 4 za dhahabu na 2 za fedha, huku wenzao wa kiume pia wakitawazwa mabingwa kwa kuchota medali 2 za dhahabu, 3 za fedha na shaba moja katika duru ya nane ya mashindano hayo yaliyofanyika mjini Beirut. Uzbekistan na Kazakhstan zimeambulia nafasi ya pili na tatu kwa utaratibu huo katika safu ya wanawake, huku Uzbekistan na Taiwan zikibeba nafasi za pili na tatu kwa upande wa wanataekwondo wa kiume.

Soka: Iran yainyuka Bulgaria

Timu ya taifa ya soka ya JKI imeizaba Bulgaria bao moja la uchungu bila jibu katika mchuano wa kirafiki uliopigwa katika Uwanja wa Hristo Botev mjini Plovdiv, kusini mwa Bulgaria. Iran ilicheza mchezo wa kasi na kutandaza gozi, licha ya kuupigia ugenini katika mchuano huo wa Alkhamisi. Bao la pekee na la ushindi la Iran kwenye mchuano huo wa kirafiki wa kimataifa ulifungwa na Mohammad Mohebbi kunako dakika ya 14. Iran Jumanne hii itavaana na Angola katika mchuano mwingine wa kirafiki katika Uwanja wa Azadi hapa jiji Tehran. Hata hivyo mashabiki hawataruhusiwa uwanjani katika mchezo huo. Team Melli ya Iran kama inavyofahamika hapa nchini, inatumia mechi hizi za kirafiki kujifua na kupasha moto misuli, kuelekea fainali za Kombe la Asia za mwaka huu 2023, zikazoandaliwa na Shirikisho la Soka Asia AFC. Iran imepangwa katika kundi C Pamoja na Umoja wa Falme za Kiarabu, Palestina na Hong Kong.

Soka: Tanzania yatinga AFCON

Timu ya taifa ya soka ya Tanzania Taifa Stars imejikatia tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2023 baada ya kutoa sare ya bila kufungana na wenyeji Algeria katika mchezo wa mwisho wa Kundi F, usiku wa Alkhamisi ya Septemba 7 katika Uwanja wa Mei 19 mjini Annaba. Kwa matokeo hayo ya sare tasa, Taifa Stars inamaliza na pointi nane, nyuma ya vinara, Algeria wenye pointi 16 na wote wanafuzu fainali za AFCON zitakazopigwa Ivory Coast mwaka huu 2023. Stars na Algeria zimezipiku Uganda iliyomaliza na pointi saba na Níger pointi mbili. Hii inakuwa mara ya tatu kihistoria kwa Tanzania kufuzu AFCON baada ya mwaka 1980 nchini Nigeria, na 2019 nchini Misri. Rais Samia Suluhu Hassan ameliongoza taifa katika kuwanyooshea mkono wa tahania wachezaji wa Taifa Stars kwa mafanikio hayo. 

Katika mechi nyingine ya mwisho ya Kundi F siku ya Alkhamisi, Níger walichapwa mabao 2-0 na Uganda katika Uwanja wa Marrakech nchini Morocco. Hata hivyo Niger na Uganda zimeshindwa kufuzu kutokana na kumaliza nafasi ya tatu na ya nne katika kundi. Mbali na Tanzania na Algeria, timu nyingine zilizofuzu AFCON 2023 ni Ivory Coast, Burkina Faso, Visiwa vya Cape Verde, Misri, Equatorial Guinea, Guinea Conackry, Guinea Bissau, Mali, Morocco, Nigeria, Senegal, Afrika Kusini, Tunisia na Zambia.

Nikudokeze tu kwamba, klabu ya Yanga ya Tanzania siku ya Jumamosi itashuka dimbani kuvaana na Al-Merrikh ya Sudan jijini Kigali Rwanda, katika mchuano wa kwanza wa raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika utakaopigwa katika Uwanja wa Pele (nyuma ukijulikana kama Nyamirambo), mjini Kigali. Wananchi msitubwage.

Dondoo za Hapa na Pale

Bingwa wa Afrika na Jumuiya ya Madola mbio za mita 100, Mkenya Ferdinand Omanyala ameibuka mfalme wa mbio za Boris Hanzekovic Memorial Continental Tour, zilizotifuliwa jijini Zagreb nchini Croatia, Jumapili. Wiki chache baada ya kuonyeshwa kivumbi kwenye Riadha za Dunia jijini Budapest nchini Hungary alipomaliza nafasi ya saba kati ya washiriki nane Agosti 20, Omanyala ametwaa taji la Zagreb kwa sekunde 9.94. Afisa huyo wa polisi amefuatwa kwa karibu na Oblique Seville kutoka Jamaica (10.07) na bingwa wa Olimpiki, Marcell Jacobs kutoka Italia (10.08) katika nafasi tatu za kwanza.

Mbali na hayo, waandaaji wa tuzo ya Ballon d’Or wametaja orodha ya wachezaji 30 wanaowania tuzo hiyo kwa mwaka 2023; ambapo baadaye watachujwa hadi kupatikana mshindi atakayetangazwa Oktoba 30, Paris Ufaransa. Walioteuliwa ni pamoja na Julian Alvarez, Nicollo Barella, Karim Benzema, Yassine Bounou, Kevin De Bruyne, Ruben Dias, Ilkay Gundogan, Erling Haaland na Harry Kane. Wengine ni Randal Kolo Muani, Khvicha Kvararskhelia, Robert Lewandowski, Kylian Mbappe, Lionel Messi, Luka Modric, Martin Odegaard, André Onana, Bukayo Saka, Mohamed Salah, Bernardo Silva na Vinisicius Jr.

Na kwa kutamatisha rais wa shirikisho la soka la Uhispania aliyesimamishwa kazi kwa unyanyasaji wa kingono, Luis Rubiales amejiuzulu. Rubiales alimbusu kiungo wa kati Jenni Hermoso kwenye midomo baada ya ushindi wa fainali ya Kombe la Dunia ya Wanawake ya Uhispania. Haya yanajiri siku chache baada ya Mwendesha mashtaka wa Uhispania kuwasilisha malalamiko katika mahakama yake kuu dhidi ya rais huo wa shirikisho la soka kwa ufuska huo. Shirikisho la soka duniani Fifa lilimsimamisha kwa muda Rubiales na kumfungulia mashtaka ya kinidhamu. 

……………..TAMATI………….