Ulimwengu wa Spoti, Septemba 25
Ulimwengu wa Spoti, Septemba 25
Karibu tuangazie baadhi ya matukio ya spoti yaliyoshudiwa katika kona mbalimbali za dunia ndani ya siku saba zilizopita.
Iran ya Pili Mieleka ya Kujiachia
Timu ya taifa ya mieleka ya kujiachia (freestyle) ya Iran imeibuka mshindi wa pili katika Mashindano ya Dunia ya Mieleka huko Belgrade nchini Serbia. Jamhuri ya Kiislamu imemaliza ya pili kwenye mashindano hayo yaliyomalizika Jumanne ya Septemba 19, baada ya kuzoa medali moja ya dhahabu, 2 za fedha na shaba moja. Mwanamieleka wa Iran, Amir Hossein Zare alitwaa medali ya dhahabu katika Mashindano hayo ya Dunia ya Mieleka huko Belgrade nchini Serbia.

Zare wa mieleka mtindo wa kujiachia (freestyle), aliibuka kidedea baada ya kumzidia nguvu na maarifa hasimu wake Geno Petriashvili kutoka Georgia, na kumzima kwa alama 11-0 katika fainali ya wanamieleka wenye kilo 125. Medali za fedha za Iran zilitwaliwa na Amir Mohammad Yazdani na Hassan Yazdani katika safu za wanamieleka wenye kilo 70 na 86 kwa usanjari huo. Mohammad Nokhodi aliibuka mshindi wa tatu na kutunukiwa medali ya shaba katika kategoria ya wanamieleka wenye kilo 79. Marekani imeibuka kidedea kwenye mashindano hayo ya kimataifa kwa kuzoa alama 148, huku Iran ikimaliza ya pili kwa pointi 110. Georgia imefunga orodha ya tatu bora kwa kuchota alama 80.
Iran ya 2 Greco-Roman
Iran aidha iling'ara katika mieleka mtindo wa Greco-Roman kwenye mashindano hayo mjini Belgrade, na kuibuka mshindi wa pili baada ya kuzoa medali lukuki. Safu hii ilimaliza mashindano hayo Jumapili ya Septemba 24. Iran imemaliza ya pili nyuma ya Azerbaijan kwa kuzoa alama 87, mbali na medali moja ya dhahabu, moja ya fedha na mbili shaba. Ijumaa usiku wa Septemba 22, Muirani Amin Mirzazadeh alimsagasaga hasimu wake kutoka Uturuki, Rıza Kayaalp, na kutunukiwa medali ya dhahabu katika safu ya kilo 130. Mmisri Abdellatif Mohamed na raia wa Cuba, Óscar Pino walitwaa medali ya shaba kwenye katogoria hii. Mapema Ijumaa, Pouya Dadmarz aliinda Iran medali ya shaba kwenye safu ya kilo 55, huku raia mwenza, Alireza Mohmadi akibeba medali ya shaba katika kitengo cha kilo 82. Aidha mwanamieleka Muirani wa Greco-Roman, Alireza Mohmadi alishindwa kufurkuta Ijumaa mbele ya hasimu wake kutoka Azerbaijan, Rafig Huseynov katika fainali ya kilo 82 na kuishia kutwaa medali ya fedha.
Katika hatua nyingine, makarateka wa Iran wamezoa medali kibao katika Mashindano ya Kimataifa ya Karate nchini Ufaransa. Jamhuri ya Kiislamu imetwaa medali 5 za dhahabu, 4 za fedha na 5 za shaba katika kategoria mbalimbali kwenye mashindano hayo ya dunia.

Soka; Iran U23 yapeta
Timu ya taifa ya vijana wenye chini ya miaka 23 ya Iran imesogea mbele hadi raundi ya 16 ya Michezo ya Asia, baada ya kuibamiza Mongolia mabao 3-0. Vijana hao wanaonolewa na Reza Enayati walicheza mchezo uliokwenda shule kwenye pambano hilo la Jumapili lililopigwa katika Uwanja wa Hangzhou nchini China.
Mabao ya mabarobaro hao wa Kiirani yalifungwa na Mehdi Mamizadeh, Mohammad Omri na Aria Barzegar. Vijana hao watatoana udhia na Thailand siku ya Jumatano. Timu hiyo ililaziishwa sare tasa na Saudi Arabia, kabla ya kuishukia vibaya Vietnam na kuichabanga mabao 4-0.
Soka AFC: Persepolis yanyukwa na a-Nasr
Mechi za raundi ya 1 ya Ligi ya Klabu Bingwa barani Asia zilifanyika Jumanne. Mabingwa wa soka wa Iran, Persepolis walikuwa wenyeji wa timu yenye wachezaji wengi nyota ya al-Nasr ya Saudi Arabia wakiongozwa na nahodha wao, Cristiano Ronado, na walishindwa kutumia vyema methali ya mcheza kwao hutunzwa baada ya kushindwa katika mchezo huo. Ikicheza ugenini katika Uwanja wa Azadi jijini Tehran bila ya watazamaji, timu yaAl-Nasr ilishinda mechi hiyo kwa mabao 2:0.
Watoto wa mjini, Persepolis ya Iran, ilipata pigo la mapema baada ya fowadi mzoefu, Mehdi Torabi kulazimika kutolewa nje ndani ya dakika 10 za kwanza kufuatia jeraha, na nafasi yake kuchukuliwa na Shahab Zahedi. Mabao ya wageni yalifungwa katika kipindi cha pili na Abdulrahman Gharib na Mohammed Qasim.
Mbio za kufuzu WAFCON
Timu ya taifa ya soka ya Kenya ya wanawake Harambee Starlets, Ijumaa walishuka dimbani mjini Yaounde, Cameroon kumenyana na Indomitable Lionesses katika raundi ya kwanza kufuzu kwa Kombe la Afrika kwa Wanawake (WAFCON) 2024. Cameroon ambayo imeorodheshwa katika nafasi ya tatu Afrika na ya 56 duniani kwenye orodha ya FIFA, iliitandika Kenya Kenya ambayo inashikilia nafasi ya 28 Afrika na 147 duniani, bao 1-0 mjini Doula. Mshambuliaji Eliane Mambalamo aliwafungia wenyeji bao hilo la pekee na la ushindi kwa kichwa kunako dakika ya tisa ya mchezo.
Kenya sasa ina kibarua kizito, kwani italazimika kuitandika Cameroon mabao 2, watakapokutana tena kwenye mechi ya marudiano jijini Nairobi siku ya Jumanne ili isogee mbele kwa raundi ya pili. Mshindi atakutana na Gabon au Botswana kwenye raundi inayofuata baadaye mwaka huu. Botswana iliiadhibu Gabon mabao 4-1 katika mechi ya mkondo wa kwanza siku ya Ijumaa. Rwanda nayo licha ya kuupigia nyumbani siku ya Jumatano, walipokezwa kichapo cha mbwa cha mabao 7-0 na Ghana. Shirikisho la Soka la Rwanda limemsimamisha kazi mkufunzi wa timu hiyo ya taifa ya wanawake, Grace Nyinawumuntu, kwa kusema kuwa mahasimu wao wa kike wa Ghana walicheza kama wanaume uwanjani, na eti yumkini wana homoni za kiume.
Dondoo za Hapa na Pale
Mwanariadha nyota wa Kenya, Eliud Kipchoge ameonyesha weledi wake katika mbio za kilomita 42 baada ya kushinda taji lake la tano la Berlin Marathon nchini Ujerumani, Jumapili. Bingwa huyo alishinda marathon hiyo yake ya 16 kati ya 19 ameshiriki kwa saa 2:02:42 akifuta rekodi ya dunia ya 2:01:09 aliweka akishinda jijini Berlin mwaka 2022. Kipchoge, ambaye anapanga kushiriki Olimpiki jijini Paris nchini Ufaransa mwaka 2024, alisalia mbele pekee yake baada ya kilomita ya 32 kufuatia Muethiopia Derseh Kindie,24, kusalimu amri. Kipchoge alifuatiwa kwa karibu na Vincent Kipkemoi (2:03:13) na Muethiopia Tadese Takele (2:03:24).

Mkenya Sheila Chepkirui aliridhika na nafasi ya pili katika safu ya akina dada kwa kutumia saa 2:17:49 baada ya Muethiopia Tigist Assefa kuhifadhi taji kwa rekodi mpya ya dunia ya 2:11:52. Assefa amefuta rekodi ya Mkenya Brigid Kosgei ya 2:14:04 iliyowekwa kwenye Chicago Marathon mwaka 2019.
Kwengineko, kipa Andre Onana ameamua kubeba msalaba kwa matokeo duni ya Manchester United, baada ya kulimwa mabao 4-3 na Bayern Munich kwenye Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya mnamo Jumatano, katika siku ambayo Arsenal ilipata raha tele baada ya kuilipua PSV mabao 4-0. Casemiro alifunga mabao mawili naye Rasmus Hojlund goli moja, mashetani wekundu wa United wakizamishwa na Bayern kupitia kwa mabao ya Leroy Sane, Serge Gnabry, Harry Kane (penalti) na Matthys Tel katika Kundi A katiia Uwanja waAllianz Arena. Wabeba bunduki wa Arsenal walirejea kwa kishindo kwenye Klabu Bingwa Ulaya baada ya miaka sita kwa kumiminia PSV mabao kupitia kwa Bukayo Saka, Leandro Trossard, Gabriel Jesus na Martin Odegaard katika mchuano wa Kundi B uwanjani Emirates. United imefungwa mabao 14 katika mechi sita. Onana,27, aliomba kuhojiwa baada ya United kupoteza dhidi ya Bayern na akakubali kosa lilikuwa lake. United sasa imepoteza kwa mara ya nne katika mechi sita msimu huu. Katika Matokeo mengine ya Septemba 20; Real Madrid iliibamiza bao 1-0 Union Berlin, wakati ambapo Galatasaray ilikuwa inalazimishwa sare ya mabao 2-2 na Copenhagen. Benfica ilinyukwa mabao 2 bila jibu na Salzburg, Braga ilipokea 2-1 kutoka Napoli, Sevilla nayo ililazimishwa sare ya bao 1-1 Lens, kama ilivyolazimishwa Real Sociedad ilipochuana na Inter Milan.
………………MWISHO…………..