Hikma za Nahjul Balagha (28)
Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Karibuni katika sehemu hii ya 28 ya mfululizo wa makala hizi fupifupi za Hikma za Nahjul Balagha. Leo pia tutaangalia kwa muhtasari hikma nyingine za Imam Ali bin Abi Talib AS kama zilivyonukuliwa kwenye kitabu cha Nahjul Balagha. Ni matumaini yetu mtakuwa nasi hadi mwisho wa kipindi. Hii ni Hikma ya 28.
اَفْضَلُ الزُّهْدِ اِخْفاءُ الزُّهْدِ
Uzuhdi bora kabisa ni wa mtu anayeficha uzuhdi wake
Imam Ali AS anasema katika hikma hii ya 28 ya Nahjul Balagha kwamba: Aina bora ya uchamungu na kuitaliki dunia, ni kuficha mtu uchamungu wake.
Mwanzoni mwa Uislamu, baadhi ya watu waliojifanya Waislamu walikuwa wakija mbele za watu kwa sifa za ucha Mungu mkubwa, kuvaa nguo za watu wa chini kabisa, kuishi katika nyumba za kimaskini, kula chakula cha watu mafakiri na vitu kama hivyo. Kidhahiri walijifanya ni watu wa zuhdi na walioachana na mapambo ya dunia, lakini katika uhalisia wao hawakuwa watu wa zuhdi bali walikuwa wanafiki na watu wanaomshirikisha Allah na vitu vingine. Ndio maana Imam Ali AS katika hikma hii anasema, ucha Mungu wa kweli, zuhdi na kuitaliki duniani kikwelikweli hakumruhusu mtu kufanya ria na kuwatangazia watu. Kama anavyosema Imam Ali AS, wengi wa watu wa namna hiyo hulazimika kuacha uzuhdi wao hata huo wa kijuujuu na hushindwa kutumia vizuri rasilimali ya kimaanawi kujikinga na ugonjwa wa ria.
Katika mafundisho matukufu ya Uislamu, mtu mwenye zuhdi ni yule ambayo amejikabidhi kikamilifu kwa Mwenyezi Mungu, yule ambaye ana yakini kwamba hakuna lolote linaloweza kufanyika bila ya nguvu za Mwenyezi Mungu na chochote alicho nacho hakitokani na nguvu zake, bali kwa ridhaa ya Muumba wake. Yule ambaye hafungamani na mambo ya kidunia na kumsahau Allah aliyempa neema hizo. Ambaye kwake yeye kuwa karibu na Mwenyezi Mungu ni muhimu zaidi kuliko jambo lolote lile. Imam Ali AS ametoa ushahidi wa maana ya zuhdi katika aya ya 23 ya Surat al Hadid akisema, zuhdi yote imekusanywa kwenye maneno mafupi ya Qur'ani Tukufu yanayosema: Ili msihuzunike kwa kilicho kupoteeni, wala msijitape kwa alicho kupeni. Mtu asikae muda wote kuomboleza yaliyopita na pia asijisahau kupindukia kufurahia yanayokuja, bali amkumbuke Allah katika hali yoyote aliyo nayo.
Tab'an ni wajibu ifahamike kwamba, zuhd maana yake si mtu kujinyima kila kitu. Kwani kama alivyosema Mwenyezi Mungu kwenye Qur'ani Tukufu, waumini wana wajibu wa kutumia vilivyo neema walizotengewa na Mola wao lakini lililo muhimu ni kutoruhusu nyoyo zao kutekwa na neema hizo na kumsahau aliyewapa. Aya ya 23 ya Surat al Aaraf inasema: Sema: Ni nani aliyeharimisha pambo la Mwenyezi Mungu alilowatolea waja Wake, na vilivyo vizuri katika riziki. Sema hivyo ni kwa walioamini katika uhai wa duniani, na Siku ya Kiyama vitakuwa vyao wao tu. Namna hivi tunazieleza Ishara kwa watu wanaojua.
Ni kwa sababu hiyo ndio maana Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) alitutahadharisha tusiharamishe vilivyohalalishwa na Mwenyezi Mungu akisema: Zuhd haina maana ya mtu kujiharamishia vya halali alivyoneemeshwa na Mwenyezi Mungu, bali maana ya zuhd ni kuwa na yakini zaidi na kile kilichoko kwa Allah kuliko kile alicho nacho yeye.
Zahid ni mtu ambaye anapoangalia safari yake ndefu na akiba yake chache huiona dunia ilivyo tambara bovu na inavyopita haraka sana. Hivyo huwa hatetereki katika jitihada za kujikurubisha kwa Allah na kujenga Akhera yake. Yuko tayari kuvumilia kila kitu kwa nafsi na damu yake ili awe miongoni mwa waliofuzu Siku ya Kiyama.