Ulimwengu wa Spoti, Okt 23
Karibu tuangazie baadhi ya matukio ya spoti yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita katika pembe mbalimbali za dunia, ukiwemo uungaji mkono wa wachezaji mbalimbali kwa wananchi madhulumu wa Palestina....
CAFA U14: Mabanati wa Iran waibuka kidedea
Timu ya kandanda ya wasichana ya Iran imeibuka kidedea kwenye Mashindano ya Ubingwa wa Asia kwa mabanati wenye chini ya miaka 14. Kina dada hao wa Iran walitwaa ubingwa huo siku ya Alkhamisi baada ya kuibamiza Tajikistan mabao 2-0 katika mchezo wa fainali uliopigwa katika Uwanja wa Dushambe katika mji mkuu wa Tajikistan.

Mabao ya Iran kwenye fainali ya mashindano hayo yaliyoandaliwa na Shirikisho la Soka Asia ya Kati (CAFA), yalifungwa na Fatemeh Lotfzadeh na Maryam Khalili. Wasichana hao wa Iran walianza mashindano hayo kwa matawi ya chini baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 na Kyrgyzstan, kabla ya kuinyoa Uzbekistan kwa kuizaba bao 1 bila jibu. Nchi sita wanachama wa shirikisho la CAFA ni Iran, Uzbekistan, Tajikistan, Kyrgyzstan, Afghanistan na Turkmenistan.
Soka: Iran yaichapa Qatar
Timu ya taifa ya soka ya Iran imetwaa ubingwa wa Mashindano ya Soka ya Jordan. Hii ni baada ya kuisasambua Qatar mabao 4-0 katika mchuano wa fainali wa mashindano hayo ya kieneo yaliyofanyika katika Uwanja wa Kimataifa wa Amman nchini Jordan. Team Melli ya Iran ilifunga mabao 4 ndani ya dakika 10. Mvua ya mabao ya Iran ilifunguliwa na Hossein Kanani kunako dakika ya 69, kabla ya Alireza Jahanbakhsh kufanya mambo kuwa 2-0 katika ya 73 ya mchezo. Vijana wa Iran waliendelea kutandaza gozi na kuwatia skulini wenzao wa Qatar. Bao la tatu la Iran lilitiwa kimyani na Sardar Azmoun kabla ya Kanani kuongeza lake la pili na la nne kwa Team Melli ambalo lilizamisha kabisa jahazi la Qatar.

Hapo awali, Iran iliichabanga Jordan mabao 3-1 katika mchuano wa nusu fainali uliopigwa Jumamosi ya wiki iliyopita mjini Amman. Mapema siku hiyo, Iraq iliitandika Jordan katika upigaji matuta kwenye mchuano wa kutafuta mshindi wa tatu na kutunukiwa medali ya shaba. Vijana wa Iran wanaonolewa na Amir Qalinoei wameshiriki mashindano hayo huko Jordan kama sehemu ya maandalizi ya fainali za Kombe la Asia baadaye mwaka huu, ambapo imepangwa katika Kundi C na Palestina, Umoja wa Falme za Kiarabu na Hong Kong.
Soka Afrika; Simba na Mazembe mambo safi
Klabu ya soka ya Simba ya Tanzania iliambulia sare ya mabao 2-2 iliposhuka katika dimba la Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam kuvaana na klabu ya Al Ahly ya Misri Ijumaa ya Oktoba 20, katika mchezo wa robo fainali ya Michuano ya African Football League. Katika mchezo huo ambao ulikuwa wa ufunguzi wa mashindano hayo mapya ya soka barani Afrika, Al Ahly ilifanikiwa kupata bao kipindi cha kwanza kabla ya mapumziko, kupitia kwa mshambuliaji wao Reda Slim na kwenda mapumziko wakiwa mbele kwa 1-0. Simba Sc ilirudi kipindi cha pili wakiwa na ari na kasi mpya kwani walitawala mchezo na kufanikiwa kupata bao la kusawazisha kupitia kwa Kibu Denis dakika ya 53 ya Mchezo.

Kocha wa Simba Sc alifanya mabadiliko kwa baadhi ya wachezaji kipindi hicho cha pili, mabadiliko ambayo yalizaa matunda, kwani baada ya kuingia Sadio Kanoute alifanikiwa kupachika bao zuri na kuwafanya Simba kuwa mbele 2-1. Dakika tatu baadae, Al Ahly walisawazisha kupitia kwa nyota wao Karhaba katika dakika ya 63 ya mchezo. Wakati huohuo, klabu ya TP Mazembe ya DRC ilivaana na Esperence ya Tunisia katika mchuano mwingine wa Ligi ya Kandanda Afrika katika Uwanja wa Mkapa. Katika mechi hiyo ya Jumapili, Mazembe ilifanikiwa kutanguliza mguu mmoja mbele kwenye nusu fainali ya African Football League baada ya kuichapa Esperance bao 1-0. Bao la Mazembe lilifungwa na Cheick Fofana dakika ya 11, na sasa wataenda nalo Tunisia kwenye mechi ya marudiano Oktoba 25.
Mazembe inakuwa ni timu ya pili kupata ushindi kwenye AFL ambapo kabla yao, Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini ilipata ushindi mnono wa ugenini wa mabao 2-0 ilipochuana na Petro De Luanda katika Uwanja wa Estádio 11 de Novembro nchini Angola. Huko Nigeria, Enyimba ilitoana udhia na Wydad Casablanca ya Morocco, ambapo Waarabu walivuna ushindi mwepesi wa bao 1-0, lililofungwa na Yahya Jabrane kunako dakika ya 39 kupitia mkwaju wa penati. Huku hayo yakiarifiwa, Rais wa Shirikisho la Kandanda Duniani (FIFA) Gianni Infantino aliwakuna mashabiki wa kandanda waliofika uwanjani Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, alipozungumza kwa lugha teule ya Kiswahili wakati wa uzinduzi wa michuano hiyo mipya ya AFL. Alikuwa miongoni mwa viongozi mashuhuri wa kimataifa waliohudhuria hafla iliyofanyika kuzindua ligi mpya. Mashindano haya yanatarajiwa kuimarisha kandanda ya klabu barani Afrika.
Dondoo za Hapa na Pale
Algeria imesitisha shughuli zote za michezo na kitamaduni zinazofadhiliwa na serikali ili kuonyesha mshikamano na wananchi wa Palestina katika Ukanda wa Gaza, ambao wanakabiliwa na mashambulizi ya anga na mzingiro wa Israel. Shirika la habari la ENTV limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, Wizara ya Vijana na Michezo ya Algeria imechukkua uamuzi huo ili kuwaunga mkono wananchi mashujaa wa Palestina na kuwaenzi wahanga wa jinai za utawala wa Kizayuni kwenye Ukanda wa Ghaza. Haya yanajiri huku wanamichezo mbalimbali wa Kiislamu walitumia kurasa zao za mitandao ya kijamii kulaani jinai zinazoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza wakikakbiliwa na mashinikizo ya Wamagharibi. Ufaransa imetishia kumpokonya uraia mchezaji nyota wa klabu ya Al-Ittihad ya Saudia, Karem Benzema kwa kutangaza uungaji mkono wake kwa wananchi madhulumu wa Palestina.

Ufaransa imetishia pia kumpokonya tuzo ya Ballon D'or mchezaji huyo wa zamani wa Real Madrid kwa hatua yake hiyo ya kusimama na wananchi wa Ukanda wa Gaza wanaokabiliwa na jinai za kutisha za utawala haramu wa Israel. Na kama hilo halitoshi, Kwa upande mwingine, mmoja wa wawakilishi wa Bunge la Ujerumani ametoa wito wa kufukuzwa kwa Noussair Mazraoui, nyota wa soka wa Morocco na mchezaji wa timu ya Bayern Munich ya Ujerumani katika klabu hiyo na Ujerumani kwa ujumla. Wito huo umetolewa baada ya Mazraoui, kulitakia ushindi taifa la Palestina dhidi ya utawala unaouawa watoto wa Israel. Gazeti la Bild la Ujerumani pia limedai kuwa Noussair Mazraoui anaunga mkono ugaidi baada ya kuwatetea raia wa Gaza wanaouawa na Israel! Youcef Atal, mwanasoka maarufu kutoka Algeria na mchezaji wa klabu ya Nice nchini Ufaransa, pia anaandamwa na wanasiasa wa Ufaransa baada ya kuukosoa utawala haramu wa Israel. Anwar El Ghazi, mchezasoka Mholanzi mwenye asili ya Morocco, mkataba wake na klabu ya "Mainz" ya Ujerumani umevunjwa baada ya mashabiki wa klabu hiyo kumshambulia kwa kuwaunga mkono watu wa Gaza. Aidha Mesut Özil, nyota wa zamani wa timu ya taifa ya Ujerumani na klabu za Arsenal na Real Madrid, anandamwa vikali baada ya kuchapisha ujumbe kwenye mitandao ya kijamii ukiwa na bendera za Uturuki na Palestina.
Na kwa kutamatisha, Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza inaombeleza kifo cha Bobby Charlton, mchezaji nyota wa zamani wa Manchester United na bingwa wa Kombe la Dunia la mwaka la 1966. Habari za kifo cha galacha huyo wa zamani wa kusakata kambumbu ilitangazwa Jumamosi wakati wa mapunziko ya michuano mitano ya EPL. Habari hiyo ya tanzia ilizima shamrashamra za ushindi uliovunwa na Mancheter City na Liverpool kwenye mechi zao siku hiyo. City ilivunja nuski ya kushidwa mechi mbili mfululizo kwa kuitandika Brighton mabao 2-1. Liverpool nao waliigaragaza Everton mabao 2-0 katika debi la Merseyside siku hiyo ya Jumamosi. Arsenal walitoka nyuma na kufanya mambo kuishia kwa suluhu ya mabao 2-2 walipotoana jasho na Chelsea katika Uwanja wa Stamford Bridge. Gunners wapo kileleni mwa jedwali la EPL wakiwa na alama 21, pointi sawia na City. New Castle imeipiku Brighton na kupanda hadi nafasi ya tano, baada ya kuicharaza Crystal Palace mabao 4-0. Brentford iliichapa Burnley mabao 3-0 nyumbani, wakati Wolves walikuwa wanaambulia ushindi wa mabao 2-1 ilipovaana na Bournmouth.
.........................MWISHO...............