Jumatano, Novemba 08, 2023
Leo ni Jumatano tarehe 23 Mfunguo Saba Rabiuthani 1445 Hijria inayosadifiana na tarehe 8 Novemba 2023 Milaadia.
Siku kama ya leo miaka 367 iliyopita, alizawa Edmond Halley, mtaalamu wa nyota wa nchini Uingereza. Halley alisoma katika kitengo cha Queen kilicho chini ya chuo kikuu cha Oxford, nchini humo na kuanza kujishughulisha na masuala ya utafiti wa nyota akiwa kijana mdogo, huku akifanya safari kuelekea kusini mwa dunia kwenye kisiwa kilichoko Bahari ya Atlantic. Edmond Halley alichukua muda mwingi katika kutalii nyota ambapo aligundua kwamba, kama ilivyo kwa sayari, nyota nazo zina obiti za duara dufu na kwa msingi huo wakati wa kurudi kwao unaweza kuhesabika. Mwaka 1704 alikuwa mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Oxford. Mnamo 1720, aliteuliwa kuwa mnajimu katika Royal Observatory huko Greenwich. Halley alifariki dunia mwaka 1742.
Katika siku kama ya leo miaka 349 iliyopita, alifariki dunia John Milton, malenga wa Kiingereza. Kazi za kwanza za ushairi za John Milton zilijulikana kwa majina ya Roho ya Huzuni na Roho ya Furaha. Kazi nyingine ya uandishi ya John Milton ni ile aliyoipa jina la Paradise Lost. Malenga Milton alikuwa akitetea suala la kutenganishwa serikali na kanisa, kuweko uhuru wa kuabudu na wakati huo huo huo aliunga mkono uchujaji wa taarifa uliokuwa ukifanywa na serikali.
Tarehe 23 Rabiuthani miaka 200 iliyopita alifariki dunia faqihi, mwanachuoni wa Hadithi na malenga mashuhuri wa Kiislamu, Allamah Ahmad Naraqi. Mwanazuoni huyo alizaliwa mwaka 1185 Hijria na kukulia katika mji wa Kashan katikati mwa Iran ambako alipata elimu kwa baba yake, Mullah Mahdi Naraqi. Miaka kadhaa baadaye alihamia katika mji mtakatifu wa Najaf, nchini Iraq na kupata elimu ya juu kwa maulamaa wakubwa wa mji huo. Msomi huyo mkubwa wa Kiislamu ameandika vitabu vingi vikiwemo vya "Miirajus Saada" na "Asrarur Hajj."
Siku kama ya leo miaka 128 iliyopita sawa na tarehe 8 Novemba mwaka 1895, miale ya X iligunduliwa na Wilhem Conrad Rontgen, mwanafizikia na mwanasayansi maarufu wa Ujerumani. Mtaalamu huyo mwaka 1901 alitunukiwa tuzo ya Nobel kwa kufanikiwa kugundua miale hiyo. Kwa kuwa hakutambua miale aliyoigundua, Rontgen aliamua kuipa jina la X. Miale hiyo hupenya kwa urahisi katika mwili wa mwanadamu na kwa ajili hiyo ni njia nzuri zaidi ya kuchukua taswira ya viungo au picha ya X-ray inayotumiwa kujua sehemu za ndani ya mwili zilizodhurika au kuvunjika.
Siku kama ya leo miaka 123 iliyopita alizaliwa Bi Margaret Mitchell mwandishi wa Kimarekani huko Atlanta katika jimbo la Georgia nchini humo. Baba yake Bi Mitchell alikuwa wakili wa mahakama. Kwa muda fulani alisomea fani ya udaktari, lakini baadaye alilazimika kukatisha masomo hayo kutokana na majonzi aliyokuwa nayo kufuatia kifo cha baba yake. Margaret allianza kazi ya uandishi akiwa na miaka 22. Alizidi kupata umashuhuri baada ya kuchapisha riwaya yake aliyoiita kwa jina la "Gone with The Wind."