Nov 11, 2023 03:29 UTC
  • Jumamosi, 11 Novemba, 2023

Leo ni Jumamosi tarehe 26 Mfunguo Saba Rabiuthani 1445 Hijria sawa na 11 Novemba 2023 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 980 iliyopita, alizaliwa huko Marv, moja ya miji ya Khurasan ya zamani ulioko Turkmenistan ya sasa, Ainuz-Zaman Qatwan Marvazi, mtaalamu wa hesabati, tabibu na mwanafalsafa wa Kiislamu. Qatwan Marvazi alikuwa na umahiri mkubwa katika elimu za hesabati, falsafa, fasihi na elimu ya dini ya Kiislamu. Hata hivyo binafsi alipendelea sana elimu ya tiba. Marvazi ambaye alikuwa akijishughulisha na kutoa huduma ya tiba katika mji wa Marv aliandika vitabu kadhaa na moja ya vitabu hivyo ni 'Kaihaan Shenakht' ambacho kinahusu elimu ya hesabati. Ainuz-Zaman Qatwan Marvazi alifariki dunia mwaka 548 Hijria. ***

Ainuz-Zaman Qatwan Marvazi,

 

Siku kama ya leo miaka 927 iliyopita alifariki dunia Hassan al-Sabbah mwasisi wa utawala wa Ismailiyah nchini Iran. Sabbah alizaliwa mwaka 445 Hijiria mjini Qum na akiwa mtoto pamoja na familia yake alielekea mjini Ray, kusini mwa mji wa Tehran. Akiwa mjini hapo alijifunza masomo ya dini ya Kiislamu na Ushia. Hata hivyo akiwa kijana alijiunga na madhehebu ya Ismailiyah. Wafuasi wa kundi hilo kinyume na Mashia wengine baada ya Imam Swadiq (as) walikataa kumtambua mtoto wa mjukuu huyo wa Mtume (saw) yaani al-Imam al-Kadhim (as) kuwa Imam na badala yake wakamtambua mtoto mwingine wa Imam Swadiq, yaani Ismail kuwa ndiye Imam. Baada ya Hassan al-Sabbah kujiunga na kundi hilo alielekea nchini Misri kwa lengo la kujifunza mafundisho zaidi ya Ismailiyah. Wakati huo viongozi wa Ismailiyah walikuwa ni makhalifa wa utawala wa Fatwimiyah nchini Misri. Mwaka 473 Hassan al-Sabbah alirejea Iran na kuanza kueneza mafundisho ya kundi hilo katika maeneo tofauti ya Iran. Mwaka 483 alidhibiti ngome imara ya Alamūt karibu na mji wa Qazvin na ukawa mwanzo wa harakati ya mapambano dhidi ya utawala wa Seljuk uliokuwa unatawala Iran. Utawala wa Ismailiya chini ya uongozi wa Hassan al-Sabbah ulidhibiti pia ngome tofauti za kaskazini mashariki, kusini na hata katikati ya Iran sambamba na kuua viongozi wengi wa utawala wa Seljuk. Sabbah alifahamika kwa ubora huku akitabahari katika elimu za theolojia, falsafa na elimu ya nyota. Aliwaaachia wafuasi wake vitabu kadhaa. ***

Hassan al-Sabbah

 

Siku kama ya leo miaka 134 iliyopita, alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 68 Ayatullah Mullah Ahmad Khoeiini Qazvini, mtaalamu wa sheria za Kiislamu (fiqhi), mtafiti na mtaalamu wa Hadithi wa Kishia. Baada ya kuhitimu masomo ya msingi alielekea Qazvin na baada ya hapo alielekea Isfahan kwa ajili ya masomo ya juu. Baada ya kustafidi na maulama wakubwa wa mji wa Isfahan alifanya ziara katika maeneo matakatifu nchini Iraq ambapo alikaa miaka kadhaa akijiendeleza kimasomo. Alirejea Qazvin na kuanza kazi ya ufundishaji na kutoa fatwa. Ayatullah Mullah Ahmad Khoeiini Qazvini ameacha athari kadhaa kama vile 'Mi’raajul-Wusuuli ila ilmil-Usuul’ chenye juzuu mbili, ‘Lawaamiu fil-Fiqhi’ chenye juzuu tatu na ‘Mir-atul-Muraadi fi Ilmir-Rijaal.’ ***

Ayatullah Mullah Ahmad Khoeiini Qazvini

 

Siku kama ya leo miaka 105 iliyopita, Vita vya Kwanza vya Dunia vilifikia kikomo baada ya kutiwa saini mkataba wa kuacha vita hivyo. Vita vya Kwanza vya Dunia vilipiganwa kuanzia mwaka 1914 hadi 1918 kati ya nchi waitifaki yaani serikali za Russia, Uingereza, Ufaransa na Italia kwa upande mmoja, na nchi za Ujerumani, Bulgaria, Utawala wa Othmania na ufalme wa Austria na Hungary kwa upande wa pili. Watu zaidi ya milioni 15 waliuawa katika vita hivyo na wengine milioni 20 kujeruhiwa. Vilevile vilisababisha hasara inayokadiriwa kuwa zaidi ya dola bilioni 150 kwa nchi zilizopigana vita hivyo. ***

Kutiwa saini mkataba wa kuacha vita 

 

Miaka 48 iliyopita katika siku kama ya leo, Angola ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Mreno. Wakoloni wa Kireno kwa mara ya kwanza waliingia katika ardhi ya Angola mwaka 1483 Miladia. Wakati huo, ardhi ya Angola ilikuwa sehemu ya ufalme wa Kiafriika wa Congo.***

 

Siku kama ya leo miaka 189iliyopita, aliaga dunia Yasser Arafat Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina na kiongozi wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) katika hospitali moja mjini Paris, Ufaransa. Alizaliwa mwaka 1929 na kuanza harakati za mapambano dhidi ya utawala dhalimu wa Israel akiwa katika rika la ujana. Mwaka 1946, Yasser Arafat alielekea nchini Misri kwa ajili ya masomo ya juu katika Chuo Kikuu cha Cairo na miaka mitano baadaye alihitimu masomo katika taaluma ya Usanifu Majengo. Mwaka 1965 alirejea Palestina na kuasisi Harakati ya Fat-h ili kupambana na utawala wa Tel Aviv. Miaka minne baadaye alichukua hatamu za kuongoza PLO hadi alipoaga dunia. ***

Yasser Arafat

 

Tags