Jumapili, 12 Novemba, 2023
Leo ni Jumapili 27 Mfunguo Saba Rabiuthani 1445 Hijria sawa na 12 Novemba 2023 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 126 iliyopita alizaliwa Ali Isfandiyari mashuhuri kwa jina la Nima Yushij, mwasisi wa mashairi ya kisasa nchini Iran. Isfandyari alizaliwa katika mojawapo ya vijiji vya mkoa wa Mazandaran kwa jina la Yush huko kaskazini mwa Iran. Malenga huyo baadaye alielekea Tehran na kuanza kujifunza lugha ya Kifaransa. Nima Yushij alianza kutunga mashairi na kubuni mfumo mpya wa mashairi. Miongoni mwa sifa za mfumo huo wa mashairi mapya ni kueleza masuala ya jamii kwa lugha nyepesi. Kazi muhimu zaidi ya malenga huyo mashuhuri wa Iran ni maarufu kwa jina la "Afsaneh". ***
Miaka 109 iliyopita katika siku kama ya leo, kulitolewa fatuwa ya Marajii Taqlidi wa Kishia na Maulamaa wakubwa wa Iraq kwa ajili ya kukabiliana na uvamizi wa Uingereza. Hiyo ilikuwa ni katika kkipindi cha kujiri Vita vya Kwanza vya Dunia. Katika zama hizo ardhi ya Iraq ya leo ilikuwa sehemu ya utawala wa Othmania ambapo wanajeshi wake hawakuwa na uwezo wa kulinda ardhi hiyo mbele ya Waingereza. Licha ya kuwa, Mashia wa Iraq walikuwa wamedhurika kutokana na ubaguzi na udhalimu wa utawala wa Othmania, lakini kutokana na fatuwa ya Maulamaa wao walijitokeza na kukabiliana na uvamizi wa Uingereza. ***
Katika siku kama ya leo miaka 105 iliyopita yaani Novemba 12 mwaka 1918, utawala wa kifalme ulikomeshwa nchini Austria na kuanza kipindi cha utawala wa Jamhuri baada ya kushindwa utawala wa Austria na Hungary katika Vita vya Kwanza vya Dunia na kutengana nchi hizo mbili. Mfalme wa mwisho wa Austria, Charles wa Kwanza ambaye alitawazwa kuwa mfalme wa nchi hiyo tarehe 21 Novemba mwaka 1916, alijiuzulu uongozi siku moja tu baada ya kutiwa saini makubaliano ya kusimamisha Vita vya Kwanza vya Dunia hapo tarehe 11 Novemba mwaka 1918 na kuomba hifadhi nchini Uswisi. ***
Siku kama ya leo miaka 81 iliyopita, vita vya kihistoria vilivyopewa jina la al-Alamein vilimalizika katika mji wenye jina kama hilo huko kaskazini mwa Misri kati ya wanajeshi wa Uingereza na jeshi la Manazi wa Ujerumani. Vita hivyo vilimalizika baada ya kushindwa jeshi la Ujerumani, japokuwa mapigano kati ya pande hizo mbili yaliendelea katika maeneo mengine ya kaskazini mwa Afrika. Amani kamili ilipatikana katika maeneo hayo baada ya kushindwa kikamilifu jeshi la Ujerumani wakati wa Vita vya Pili vya Dunia. ***
Miaka 67 iliyopita, askari wa utawala haramu wa Israel walifanya mauaji mengine ya umati dhidi ya Wapalestina wasio na hatia katika kambi kubwa ya Wapalestina mjini Rafah huko katika Ukanda wa Gaza. Jinai hiyo ilifanyika siku chache tu baada ya kutangazwa usitishaji vita baina ya Israel, Ufaransa na Uingereza dhidi ya Misri. Hujuma hiyo ya kinyama ilisababisha mauaji ya Wapalestina 110, wakiwemo wanawake na watoto na kujeruhi wengine 1,000. ***

Katika siku kama ya leo miaka 40 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Sayyid Ahmad Khansari, faqihi na marjaa mkubwa wa Kishia. Akiwa na umri wa miaka 20, Ayatullah Ahmad Khonsari alielekea mjini Najaf, Iraq na kustafidi na elimu kutoka kwa wasomi wakubwa kama vile Muhaqqiq Khorasani, Sayyid Muhammad Kadhim Yazdi, Shariat Isfahani na Muhaqqiq Naaini. Ayatullah Sayyid Ahmad Khonsari alielekea mjini Arak, Iran katika kipindi cha kuasisiwa chuo cha hauza cha mji huo na kujishughulisha na ukufunzi. Baadaye msomi huyo alishirikiana na Ayatullah Sheikh Abdul-Karim Hairi katika shughuli za tablighi na baada ya kuasisiwa hauza ya Qum, chini ya usimamizi wa Ayatullah Hairi Yazdi, Ayatullah Ahmad Khansari alikuwa imamu wa Swala ya jamaa katika chuo cha Faiziya mjini humo. Alishirikiana bega kwa bega na wanazuoni wa Kiislamu wakiongozwa na hayati Imam Ruhullah Khomeini katika harakati za Mapinduzi ya Kiislamu dhidi ya utawala muovu wa Shah. Msomi huyo amelea ma lufunza wasomi wakubwa kama Ayatullah Murtadha Mutahhari, Imam Musa Sadr na Sayyid Ridha Sadr. Mwaka 1370 Hijiria, Ayatullah Ahmad Khonsari alielekea mjini Tehran na kuwa imamu wa swala ya jamaa katika msikiti maarufu wa ‘Sayyid Azizullah’. Ameandika vitabu vingi katika taaluma za sheria na teolojia ya Kiislamu. ***
Katika siku kama ya leo miaka 6 iliyopita ulitokea mtetemeko wa ardhi uliokuwa na ukubwa wa 7 kwa kipimo cha Rishta katika mkoa wa Kermanshah huko magharibi mwa Iran na maeneo ya kandokando yake huko mashariki mwa Iraq. Kituo kikuu cha mtetemeko huo wa ardhi kilikuwa umbali wa kilomita 5 kutoka mji wa Ezgeleh na kilomita 11 chini ya ardhi. Mtetemeko huo ulihisika pia katika nchi za Uturuki, Kuwait na Saudi Arabia. Karibu watu 574 waliaga dunia kutokana na mtetemeko huo wa ardhi na wengine elfu 9,388 walijeruhiwa. Watu wengine elfu sabini walipoteza makazi yao. Idadi kubwa zaidi ya watu walipoteza maisha katika miji ya Qasr-e Shirin, Sarpol-e Zahab na Salas-e Babajani. ***