Nov 20, 2023 17:37 UTC
  • Hikma za Nahjul Balagha (34)

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Karibuni katika sehemu hii ya 34 ya mfululizo wa makala hizi fupifupi za Hikma za Nahjul Balagha. Leo pia tutaangalia kwa muhtasari hikma nyingine za Imam Ali bin Abi Talib AS kama ilivyonukuliwa kwenye kitabu cha Nahjul Balagha tukiwa na matumaini mtakuwa nasi hadi mwisho wa kipindi. Hii ni Hikma ya 34.

Katika Hikma ya 31 ya Nahjul Balagha, Imam Ali (AS) ameelezea nguzo za imani. Kwa kuzingatia umuhimu wa suala la imani na wajibu wa kuwa na ufahamu mzuri kuhusu hikma hii, tumeamua kuizungumzia na kuichambua katika vipindi sita mfululizo hii ikiwa ni sehemu ya nne ya kuichambua hikma ya 31 ya Nahjul Balagha. Leo tutazungumzia nguzo ya Jihadi kama ilivyotajwa na Imam Ali AS kwenye hikma hiyo.

Katika hikma hiyo ya 31 ya Nahjul Balagha, Imam anasema, imani ina misingi mikuu minne na kila msingi una matawi manne ambayo yakikusanyika pamja yanaunda nguzo kumi na sita za imani zinazohusiana na itikadi na matendo. Kwa yakini, kama mtu ataweza kushikamana na kuzitekeleza kikamilifu nguzo hizo 16 katika maisha yake, atakuwa kwenye kilele cha imani, na ni imani hiyo ndiyo inayoweza kuuongoza ulimwengu kwenye usalama, amani na haki, na kumpandisha mwanadamu hadi kwenye nafasi ya karibu sana na Mwenyezi Mungu na kukuza heshima na hadhi yake.

 

Leo kama tulivyotangulia kusema, tumeamua kuzungumzia kipengee cha Jihadi katika nguzo kuu za Imani ambapo Imam Ali AS anasema:

وَالْجِهَادُ مِنْهَا عَلَى أَرْبَعِ شُعَب: عَلَى الاْمْرِ بِالْمَعْرُوفِ، وَالنَّهْىِ عَنِ الْمُنْکَرِ، وَالصِّدْقِ فِی الْمَوَاطِنِ، وَشَنَآنِ الْفَاسِقِینَ

Na Jihadi nayo ina matawi manne: kuamrisha mema, kukataza maovu, ukweli mbele ya watu na uimara katika vita na mafasiki na waovu. 

Kuhusu na Jihadi, Imam Ali ameigawa nguzo hiyo muhimu ya imani katika mihimili minne. Anasema kuna jihadi ya moyoni, kuna jihadi ya ulimini, kuna jihadi katika matendo na hatimaye kuna jihadi ya kutumia silaha kwenye medani ya vita. Baada ya hapo Imam anazungumzia athari za kila tawi moja katika maisha ya mwanadamu na kusema:

فَمَنْ أَمَرَ بِالْمَعْرُوفِ شَدَّ ظُهُورَ الْمُؤْمِنِینَ وَ مَنْ نَهَى عَنِ الْمُنْکَرِ أَرْغَمَ أُنُوفَ الْکَافِرِینَ وَمَنْ صَدَقَ فِی الْمَوَاطِنِ قَضَى مَا عَلَیْهِ وَمَنْ شَنِئَ الْفَاسِقِینَ غَضِبَ لِلَّهِ، غَضِبَ اللَّهُ لَهُ وَأَرْضَاهُ یَوْمَ الْقِیَامَهِ

Mwenye kuamrisha mema humtia nguvu muumini mwenzake. Na mwenye kukataza maovu, huzirambisha mchanga pua za makafiri na wanafiki. Na anayepambana kiukweli katika medani za mapambano huwa ametekeleza ipasavyo majukumu yake ya kuwa mkweli na mwaminifu kwa raia wenzake na mwenye kuwachukia wahalifu kwa ajili ya kutafuta radhi za Allah, Mwenyezi Mungu atawaghadhibikia wahalifu hao na atamridhia yeye siku ya Kiyama. 

Mtu mwenye kuwachukia watendao maovu na wanaomkasirikia Allah, Mwenyezi Mungu pia atamghadhibikia mtenda maovu na kumlinda mwamrishaji mema mbele ya maadui zake na kumfurahisha Siku ya Kiyama. Mwenyezi Mungu anakasirika kwa ajili ya anayetenda mema na ameahidi kumfidia tabu anazopata duniani kwa kumpa radhi Zake Siku ya Kiyama.

Imepokewa hadithi kutoka kwa Imam Sadiq AS kwamba wakati Malaika wawili walipopewa amri ya kwenda kuuangamiza mji ambao watu wake walikuwa waovu walimwona mzee mmoja akiomba dua na kunyenyekea mno kwa Mwenyezi Mungu. Mmoja wa wale Malaika wawili alimwambia mwenzake, unamuona yule mzee anavyoomba dua? Tunaweza kuungamiza kweli mji huu ambao una mtu kama huyu? Hivyo Malaika wale walirejea kwa Mwenyezi Mungu  bila ya kutekeleza amri waliyopewa na kumuomba awasamehe na asiwape kazi ya kuungamiza mji ule. Sauti ikaja na kuwaambia, nendeni mkatekeleze amri yangu

فَإِنَّ ذَا رَجُلٌ لَمْ یَتَمَعَّرْ وَجْهُهُ غَیْظاً لِی قَطُّ:

kwani mtu yule mliyemuona, kamwe uso wake haujawahi kubadilika kwa ghadhabu kwa ajili Yangu.

Tags