Jumatano, Novemba 22, 2023
Leo ni tarehe 8 Mfunguo Nane, Jamadil Awwal 1445 Hijria inayosadifiiana na 22 Novemba 2023 Milaadia.
Siku kama ya leo miaka 204 iliyopita, alizaliwa Bi. Mary Ann Evans maarufu kwa jina la George Eliot, mwandishi wa riwaya na simulizi wa Uingereza. Akiwa mtoto mdogo, Evans alipendelea zaidi kusoma vitabu, na taratibu akaingia katika fani ya uandishi. Evans alikuwa na misimamo mikali ya dini ya Kikristo akiwa bado kijana. Hata hivyo misimamo hiyo ilipungua baadaye. Akiwa na umri wa miaka 30, Ann Evans alifasiri kitabu cha ‘Maisha ya Nabii Issa (as)’ (The Life of Jesus) kilichoandikwa na David Friedrich Strauss. Riwaya za Eliot zinahesabiwa kuwa miongoni wa vitabu maarufu zaidi vya karne ya 19 nchini Uingereza.
Miaka 132 iliyopita katika siku kama hii ya leo alifariki dunia mwanazuoni wa Kiislamu, Muhammad Baqir Zainul Abidin Khansari katika mji wa Isfahan nchini Iran. Alikuwa hodari katika elimu za fiqhi na hadithi na alipewa ijaza ya kunukuu Hadithi na wanazuoni wakubwa katika taaluma hiyo. Baada ya muda msomi huyo mkubwa ambaye alikuwa gwiji wa wasifu na shajara za maulamaa na wataalamu wa fiqhi ya Kiislamu, alishika hatamu za kuongoza chuo kikuu cha kidini cha Isfahan. Mirza Muhammad Baqir Khansari ameandika vitabu vingi na miongoni mwa vitabu vyake ni Raudhaatul Jannat na Hashiyatu Sharhil Lum'ah.
Siku kama ya leo miaka 122 iliyopita aliaga dunia Sheikh Muhammad Abduh ambaye alikuwa miongoni mwa wanazuoni mashuhuri wa Kiislamu katika mji wa Alexandria nchini Misri. Alipata elimu katika Chuo Kikuu cha al Azhar na kisha akahudhuria darsa za Jamaluddin Asadabadi, mwanazuoni aliyepigania uhuru wa nchi za Kiislamu. Baada ya kupelekwa uhamishoni Sayyid Jamaluddin, Sheikh Muhammad Abduh alichukua nafasi yake ya kufundisha na kutoa elimu kwa wanazuoni na wanafikra za Kiislamu. Hata hivyo Sheikh Abduh alibaidishiwa nchini Syria baada ya satuwa ya wakoloni wa Kiingereza kuenea nchini Misri. Baada ya kufunza kwa kipindi cha miaka sita nchini Syria alihamia Paris na kusaidiana na Sayyid Jamaluddin Asadabadi katika kuchapisha gazeti la al Uruwatul Wuthqaa.
Siku kama ya leo miaka 80 iliyopita, kufuatia kujiri kwa Vita vya Pili vya Dunia, nchi ya Lebanon ilijipatia uhuru wake. Lebanon ilitoka katika udhibiti wa utawala wa Othmania mnamo mwaka 1918 Miladia na kudhibitiwa baadaye na Ufaransa. Mwaka 1923 Miladia Ufaransa iliikalia nchi hiyo kwa idhini ya Umoja wa Mataifa. Tangu wakati huo Lebanon ikaanza kushuhudia siasa za ukoloni wa Mfaransa vikiwemo vitendo vya ubaguzi na machafuko. Nchi hiyo ilijipatia uhuru wake mwaka 1943.
Katika siku kama ya leo miaka 60 iliyopita, John F. Kennedy, rais wa wakati huo wa Marekani aliuawa na raia mmoja wa nchi hiyo akiwa ziarani katika mji wa Dallas huko katika jimbo la Texas. Kennedy alizaliwa mwaka 1917 na alikuwa mwakilishi wa bunge la Marekani kwa duru tatu kuanzia mwaka 1946 na duru moja alikuwa mwakilishi wa seneti ya nchi hiyo. Siku kadhaa baadaye Lee Harvey Oswald ambaye alimuua Kennedy naye pia aliuawa na mtu aliyejulikana kwa jina la Jack Ruby na polisi ya Marekani ilidai kuwa mtu huyo vilevile aliaga dunia baadaye akiwa jela kutokana na maradhi ya saratani.
Siku kama ya leo miaka 56 iliyopita, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipasisha azimio nambari 242 kuhusu Palestina. Miongoni mwa vipengee vya azimio hilo ni udharura wa kuondoka askari wa utawala ghasibu wa Israel katika ardhi zote za Palestina zilizokaliwa kwa mabavu Juni mwaka 1967 katika vita vya Waarabu na Israel, kusimamishwa operesheni za kijeshi na kutatuliwa kadhia ya wakimbizi wa Palestina kwa njia ya uadilifu. Hata hivyo kutokana na himaya ya pande zote ya Marekani na nchi za Magharibi kwa utawala ghasibu wa Israel, utawala huo haramu umekataa kutekeleza azimio hilo.
Katika siku kama hii ya leo miaka 52 iliyopita vikosi vya jeshi la Uingereza viliondoka Ghuba ya Uajemi baada ya kulikalia kwa mabavu eneo hilo kwa takriban karne mbili. Baada ya kudhoofika sana kwa Uingereza na kuanguka kwa ufalme wake kutokana na Vita vya Pili vya Dunia, pamoja na harakati nyingi za wananchi na kupata uhuru makoloni kadhaa ya Uingereza, mnamo 1968, serikali ya nchi hiyo ilitangaza sera ya kuondoka mashariki mwa Mfereji wa Suez. Kulingana na Waingereza, eneo hilo lilijumuisha Ghuba ya Uajemi, Bahari ya Oman, Singapore, Malaysia na maeneo mengine kadhaa. Hata hivyo, kabla ya kuondoka kwenye Ghuba ya Uajemi, London ilijaribu kuchukua hatua kutimiza malengo yake haramu na kuibua migawanyiko katika eneo hilo, ikiwa ni pamoja na kuimega na kujitenga Bahrain na Iran.