Jumanne, tarehe 9 Januari, 2024
Leo ni Jumanne tarehe 26 Jumadithani 1445 Hijria sawa na Januari 9 mwaka 2024.
Siku kama ya leo miaka 1437 iliyopita vita vya Dhatus Salasil vilimalizika kwa Waislamu kujipatia ushindi.
Vita hivyo vilianza baada habari kusambaa kuwa kikundi cha washirikina kilitaka kushambulia mji wa Madina. Baada ya habari hiyo kumfikia Mtume Muhammad (saw), aliwaamuru baadhi ya Waislamu waende kukabiliana na washirikina hao wakiongozwa na kamanda mmoja aliyetoka upande wa Muhajirina. Hata hivyo baada ya kujua uwezo mkubwa waliokuwa nao maadui, kundi hilo la Waislamu lilirejea Madina.
Mtume alimtuma kamanda mwingine lakini naye pia alirejea bila mafanikio. Wakati huo Mtume (saw) alimteua Ali bin Abi Twalib (a.s) kuongoza jeshi la Waislamu katika mapigano hayo. Imam Ali (as) aliwashambulia maadui kwa umahiri mkubwa na kurejea Madina na ushindi.

Siku kama ya leo miaka 232 iliyopita, kulitiwa saini makubaliano ya amani baina ya wafalme wawili wa utawala wa Othmania na Urusi, makubaliano ambayo yalihitimisha vita vya Ulaya katika karne ya 18.
Vita hivyo vilianza mwezi Agosti mwaka 1787 wakati utawala wa Othmania ulipotangaza vita dhidi ya Russia na Austria. Hii ni kwa kuwa nchi hizo mbili zilikuwa na mpango wa kuigawa dola ya Othmania.

Katika siku kama ya leo miaka 116 iliyopita, alizaliwa Simone De Beauvoir, mwandishi wa kike wa Ufaransa. Beauvoir alisoma elimu ya hisabati na falsafa katika chuo kimoja kikuu cha nchi hiyo na baada ya kuhitimu masomo akaanza kufundisha elimu ya falsafa. Simone De Beauvoir alikuwa mfuasi wa mrengo wa kushoto wa ufeministi, ambapo alitaka kuondolewa ubaguzi ndani ya jamii ya wanawake. Kitabu chake cha 'Jinsia ya Pili' ni moja ya athari zake mashuhuri katika uwanja huo. Hata hivyo mwanamke huyo alifuata njia ghalati zaidi, ambapo kupitia kampeni yake ya kile alichokiita kuwa ni kudai uhuru wa mwanamke, badala ya kusisitizia nafasi ya kimaumbile aliyonayo mwanamke, alihalalisha mwanamke kuavya mimba, kuishi bila ya kuolewa na kufanya usagaji, suala ambalo limekuwa na madhara makubwa kwa jamii ya wanawake. Bi. Simone De Beauvoir mwenyewe alikuwa na mahusiano haramu na profesa Jean-Paul Sartre kuanzia mwaka 1929 hadi mwaka 1980 alipofariki dunia, suala ambalo linadhihirisha undumakuwili wa kampeni za ufeministi. *

Siku kama ya leo miaka 102 iliyopita alizaliwa Ahmed Sékou Touré, kiongozi wa mapinduzi ya Guinea.
Touré aliingia katika mapambano ya kupigania uhuru wa nchi yake kutoka mikononi mwa mkoloni Mfaransa akiwa bado kijana. Mwaka 1952 Ahmed Sékou Touré alichaguliwa kuwa mkuu wa chama cha Demokrasia nchini Guinea na kuendeleza mapambano ya amani dhidi ya mkoloni huyo.
Hatimaye mwaka 1958 nchi hiyo ilipata uhuru na mwaka mmoja baadaye Touré akateuliwa kuwa rais na kusalia madarakani hadi mwaka 1984 alipofariki dunia.

Tarehe 9 Januari miaka 64 iliyopita ilianza operesheni ya kujenga bwawa kubwa la Aswan huko katika mto Nile nchini Misri.
Ujenzi wa bwawa hilo ulikuwa miongoni mwa mipango muhimu ya kiuchumi ya Misri iliyotangazwa mwaka 1953 na rais wa wakati huo wa nchi hiyo, Gamal Abdulnasir.
Nchi za Magharibi pia zilitangaza kuwa zilikuwa tayari kusaidia na kushiriki kwenye ujenzi wa Bwawa la Aswan. Hata hivyo baada ya mfereji wa Suez kutaifishwa na Rais Gamal Abdulnasir mwaka 1956 na vikosi vya Ufaransa, Uingereza na utawala wa Kizayuni kuendesha mashambulio ya pamoja dhidi ya Misri, serikali hizo za Magharibi zilikataa kusaidia ujenzi wa bwawa hilo.
Bwawa la Aswan huzalisha megawati 2100 za umeme na kusaidia shughuli za kilimo cha umwagiliaji katika eneo la kusini mwa Misri.

Januari 9 miaka 60 iliyopita ulitokea uasi mkubwa dhidi ya Marekani huko Panama kufuatia kupeperushwa bendera ya Marekani katika eneo la Mfereji wa Panama.
Wanajeshi wa Marekani waliwauwa na kuwajeruhi wananchi wengi wa Panama katika uasi huo. Marekani iliasisi vituo vya kijeshi katika maeneo 134 ya Panama wakati wa Vita vya Pili vya Dunia na kuikalia kwa mabavu kikamilifu nchi hiyo.

Siku kama ya leo miaka 46 iliyopita, maandamano makubwa ya kwanza ya wananchi Waislamu wa Iran baada ya Harakati ya 15 Khordad 1342 Hijria Shamsia yalifanyika mjini Qum hapa nchini dhidi ya utawala wa Shah. Maandamano hayo yalifanyika baada ya gazeti moja la alasiri kuchapisha makala iliyomvunjia heshima Imam Ruhullah Khomeini. Katika maandamano hayo wananchi na wanazuoni wa mji wa Qum walikusanyika katika Msikiti Mkuu wa mji huo na kutaka kuondolewa madarakani utawala wa Shah. Jeshi la Shah lilishambulia waandamanaji na kuua wengi miongoni mwao.
Baada ya tukio hilo wanazuoni wengi wa Kiislamu walipelekwa uhamishoni katika miji mbalimbali ya Iran na tarehe 19 Dei 1356 ilitambuliwa kuwa mwanzo wa kupamba moto harakati ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran.

Na siku kama ya leo miaka 7 iliyopita aliga dunia Ayatullah Ali Akbar Hashemi Bahremani maarufu kwa jina la Ali Akbar Hashemi Rafsanjani akiwa na umri wa miaka 82 kutokana na matatizo ya moyo.
Ayatullah Rafsanjani anatambuliwa kuwa miongoni mwa wanasiasa mashuhuri sana wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Alizaliwa katika kijiji cha Bahreman huko Rafsanjani katika familia tajiri kiasi na kupata elimu ya dini katika mji mtakatifu wa Qum. Huko alijiunga na wanaharakati waliokuwa wakipinga utawala wa dhalimu wa Shah waliokuwa wakiongozwa na hayati Imam Ruhullah Khomeini.
Ayatullah Rafsanjani alikamatwa na kufungwa jela mara kadhaa na utawala wa Shah. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu Rafsanjani alishika nyadhifa nyingi ikiwemo ya uspika wa Bunge, Rais wa jamhuri na mkuu wa Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Kiislamu.
