Jumanne, Januari 16, 2024
Leo ni Jumanne tarehe 4 Rajab 1445 Hijria sawa na tarehe 16 Januari 2024 Milaadia.
Siku kama ya leo miaka 23 iliyopita yaani tarehe 16 Januari 2001, Rais Laurent Desire Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo alipigwa risasi na mmoja wa walinzi wake katika ikulu ya Rais na kujeruhiwa vibaya. Baada ya tukio hilo kulienea habari za kutatanisha juu ya hatima ya kiongozi huyo. Tarehe 18 Januari yaani siku mbili baadaye, serikali ya Kinshasa ilithibitisha kufariki dunia Rais Laurent Desire Kabila. Kabila alizaliwa mwaka 1939 huko Katanga na kupata elimu ya juu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Tanzania. Aliingia madarakani mwaka 1997 baada ya vikosi vya askari aliokuwa akiwaongoza kuuteka mji wa Kinshasa na kumlazimisha Mobutu Sese Seko, rais wa wakati huo wa Zaire ya zamani kukimbilia nje ya nchi.

Tarehe 26 Dey 1357 Hijria Shamsia yaani siku kama ya leo miaka 45 iliyopita, Muhammad Reza Pahlavi, mfalme wa mwisho wa Iran alitoroka nchini kwa kisingizio cha kwenda kupata matibabu nje ya nchi, baada ya kushadidi wimbi la harakati za Mapinduzi. Muhammad Reza Pahlavi alichukua kiti cha ufalme mwaka 1320 Hijria Shamsia baada ya serikali ya Uingereza kumpeleka uhamishoni baba yake, Reza Shah, kwa sababu aliiunga mkono Ujerumani wakati wa Vita vya Pili vya Dunia. Siku chache kabla ya tukio hilo, Imam Ruhullah Khomeini ambaye wakati huo alikuwa Ufaransa, alitoa ujumbe mzito akisema kuwa: "Safari ya Shah bila ya kung’oka madarakani haitabadilisha lolote na utawala wa kifalme nchini Iran unapaswa kuangushwa kikamilifu."

Siku kama ya leo miaka 74 iliyopita aliaga dunia Ayatullah Sayyid Muhsin Amin al Amili, alimu na mwanafasihi mkubwa wa Kiislamu. Alizaliwa mwaka 1284 Hijria katika eneo la Jabal Amili nchini Lebanon na kupata elimu ya msingi ya Kiislamu nchini humo. Ayatullah Sayyid Amin alielekea Najaf nchini Iraq akiwa na umri wa miaka 24 kwa shabaha ya kukamilisha elimu ya juu na kupata elimu kwa maulamaa wakubwa wa mji huo. Baadaye alielekea Syria na kutoa huduma kubwa za kufundisha Uislamu. Mwanazuoni huyo mkubwa wa Kiislamu ameandika vitabu vingi muhimu zaidi kikiwa kile cha A'yanul Shia chenye juzuu kumi. Katika kitabu hicho Sayyid Muhsin al Amin amearifisha vinara wa Kiislamu wa madhehebu ya Shia hususan maimamu watoharifu katika kizazi cha Bwana Mtume (saw) na mchango wao katika kuimarisha ustaarabu wa Kiislamu. Kitabu kingine cha msomi huyo ni Kashful Irtiyab fii Atba'I Muhammad bin Abdul Wahhab kinachofichua na kukosoa itikadi za kundi potofu la Kiwahabi.

Katika siku kama ya leo miaka 178 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 16 Januari 1846, vilianza vita baina ya Marekani na Mexico baada ya Washington kuishambulia nchi hiyo. Vita hivyo vilivyochukua muda wa miaka miwili, vilitokea baada ya Marekani kudai kwamba wahajiri wa nchi hiyo wanateswa nchini Mexico. Hata hivyo ukweli ni kuwa, Marekani ilianzisha mashambulizi hayo kwa lengo la kuyatwaa baadhi ya maeneo ya Mexico hususan eneo la Texas. Katika vita hivyo, Marekani iliyakalia kwa mabavu majimbo ya Texas, California, Nevada, Utah, Arizona na New Mexico.

Miaka 853 iliyopita mwafaka na siku hii ya leo, alifariki dunia malenga wa Kiislamu, Muhammad ibn Ali al-Wasiti maarufu kwa jina la Ibn Muallim. Alizaliwa mwaka 501 Hijiria. Mashairi ya malenga huyo yalibeba ujumbe wa maadili na tabia njema na masuala mengine ya kijamii kwa kutumia lugha nyepesi. Baadhi ya mashairi ya Ibn Muallim yanahusiana na masuala ya kiroho na kiirfani. Athari pekee ya Ibn Muallim ni kitabu cha tungo za mashairi ya malenga huyo.
