Ijumaa, Januari 19, 2024
Leo ni Ijumaa tarehe 7 Rajab 1445 Hijria, sawa na 19 Januari 2024 Milaadia.
Siku kama ya leo miaka 1140 iliyopita alizaliwa Ibn Tarrar mpokezi wa hadithi na mwandishi wa fasihi wa Kiislamu huko Iraq.
Bin Tarrar ambaye ni jina lake ni Abul Fat'h Muafi bin Zakaria bin Yahya alikuwa miongoni mwa maulama wa Kishafii na alitabahari katika elimu za fiqhi, hadithi na fasihi. Msomi huyo wa Kiislamu aliandika vitabu vingi katika uwanja wa fiqhi. Vilevile aliandika vitabu katika taaluma ya fasihi ya lugha ya Kiarabu kikiwemo kile alichokiita "al Jalisu Wal Aniis".Bin tarrar alifariki dunia mwaka 390 Hijria mjini Baghdad akiwa na umri wa miaka 85.
Siku kama hii ya leo miaka 288 iliyopita alizaliwa mvumbuzi na mhandisi wa Kiingereza James Watt. Msomi huyo alipendelea na kuvutiwa mno na utafiti kuhusu masuala ya kisayansi. Katika utafiti wake Watt alifanikiwa kuvumbua nishati ya mvuke na kuzusha mapinduzi makubwa katika sekta ya viwanda hususan usafirishaji wa nchi kavu na baharini. ***
Miaka 226 iliyopita inayosadifiana na siku hi ya leo, alizaliwa Auguste Comte mwanafalsafa, mwanahisabati wa Kifaransa na mtaalamu wa falsafa umbile au positivism kwa kimombo. Comte alifikia daraja ya uhadhiri katika hisabati akiwa na umri wa miaka 18 tu. Vitabu mashuhuri vya mwanafalsafa huyo wa Kifaransa ni Auguste Comte and positivism na Early Political Writings. Comte aliaga dunia mwaka 1517. ***
Siku kama ya leo miaka 45 iliyopita, wananchi Waislamu wa Iran wenye imani na umoja walifanya maandamano makubwa kupinga mabaki yaliyosalia ya utawala wa kifalme Shah, yaani serikali ya Shapur Bakhtiyar.
Waandamanaji hao walitaka serikali hiyo ya kifalme itangazwe kuwa si halali, na pia kung'olewa utawala wa Shah na badala yale kuundwa Jamhuri ya Kiislamu nchini Iran.
Siku hiyo Imam Khomeini MA akiwa mjini Paris alitoa ujumbe wa maandishi kwa wananchi wa Iran akisema kama tunavyonukuu: "Kwa uwezo wake Mola hivi karibuni nitaungana nanyi ili niweze kuwatumikia na kushirikiana bega kwa bega na matabaka yote ya wananchi kuelekea katika njia ya kujitawala na kuwa huru Iran." Mwisho wa kunukuu. ****
Katika siku kama ya leo miaka 14 iliyopita, Abdul Rauf Mahmoud al-Mabhuh, mmoja wa makamanda waandamizi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) aliuawa shahidi huko Dubai, katika Umoja wa Falme za Kiarabu.
Mabhouh aliuawa na makachero wa Shirika la Ujasusi la utawala wa Kizayuni wa Israel walioingia nchini Imarati wakitumia pasipoti bandia. Mabhuh alizaliwa katika familia iliyoshikamana na dini katika kambi ya Jabalia katika Ukanda wa Gaza, Palestina. Shahidi Mahmoud al-Mabhuh ni miongoni mwa waasisi wa Brigedi ya Izzudeen al-Qassam tawi la kijeshi la Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS.
Baada ya kupita miezi kadhaa, Israel ilitangaza wazi kwamba, ilihusika na jinai ya kumuua Mabhuh. ***