Jumatatu, tarehe 22 Januari, 2024
Leo Jumatatu tarehe 10 Rajab 1445 Hijria sawa na 22 Januari 2024.
Siku kama ya leo miaka 1385 iliyopita alizaliwa Abdullah Bin Hussein maarufu kwa jina la Ali Asghar, mtoto wa Imam Hussein Bin Ali Bin Abi Twalib (as), mjukuu wa Mtume Muhammad (saw). Ali Asghar alizaliwa kipindi ambacho Yazid Bin Muawiya ndio kwanza alikuwa ameshika uongozi na kuanzisha mashinikizo na vitisho dhidi ya baba yake, Imam Hussein (as) akimtaka atoe baia na kiapo cha utiifu kwake. Kwa kuzingatia kuwa mjukuu huyo wa Mtume alimtambua Yazid kuwa mtu muovu na asiyefaa, alikataa kutoa baia kwa mtawala huyo. Ni kwa msingi huo ndio maana siku 18 baada ya kuzaliwa mwanaye huyo (Ali Asghar) akaondoka mjini Madina akiwa pamoja na watu wa familia yake. Nafasi muhimu ya mtoto huyo ilikuwa katika jangwa la Karbala, Iraq wakati wa vita kati ya jeshi la Yazid na Imam Hussein (as). Wakati wafuasi wote wa mjukuu huyo wa Mtume (saw) walipokuwa wameuawa shahidi, Imam Hussein alimchukua mtoto wake mchanga aliyekuwa na umri wa miezi sita kipindi hicho na kutoka naye nje ya hema kwa lengo la kumuombea maji kutokana na kiu kali iliyokuwa ikimsumbua. Maadui hao wa Uislamu waliokuwa wamewazuilia maji watu wa familia ya Mtume hawakuwa tayari kumpatia maji mtoto huyo mchanga na badala yake Harmalah Bin Kahil al-Asadi, kutoka katika jeshi la Yazid na bila ya huruma alimlenga mtoto huyo kwa mshale wenye ncha tatu ulioikatakata shingo yake na kumuua shahidi Ali Asghar. ***
Tarehe 10 Rajab miaka 1250 iliyopita, alizaliwa Imam Muhammad Taqi mmoja wa watu wa Nyumba Tukufu ya Bwana Mtume SAW katika mji mtakatifu wa Madina.
Imam Taqi Al-Jawad (as) alichukua jukumu la kuongoza Umma wa Kiislamu baada ya kuuawa shahidi baba yake yaani Imam Ridha (as). Mtukufu huyo alikuwa maarufu kwa lakabu ya 'Jawad' yenye maana ya mtu mkarimu mno, kutokana na ukarimu wake mkubwa. Nyumba ya Imam Jawad ilikuwa kimbilio la wahitaji waliokuwa wamekata tamaa na walitaraji Imam huyo awakidhie shida na mahitaji yao ya dharura. Sambamba na kutoa mkono wa kheri na baraka kwa mnasaba wa kumbukumbu ya kuzaliwa Imam mwema huyu, tunakunukulieni maneno ya hekima ya Imam Muhammad Taqi AS ambaye amesema: "Kila mwenye kuwa na imani na Mwenyezi Mungu, basi Allah humuokoa na kila baya na kumhifadhi na kila uadui."

Siku kama ya leo miaka 463 iliyopita inayosadifiana na tarehe 22 Januari 1561 alizaliwa mwanafalsafa na mtaalamu wa hesabati wa Uingereza Francis Bacon.
Awali, Bacon alijishughulisha na masuala ya kisiasa na baadaye alikamatwa na kufungwa jela baada ya kupatikana na hatia ya kula rushwa. Kipindi cha kufungwa jela kilikuwa fursa mwafaka kwa Francis Bacon kudhihirisha kipawa chake. Mwanafalsafa huyo alitoa mchango mkubwa katika kueneza sayansi asili nchini Uingereza na kuhuisha sayansi na falsafa barani Ulaya.
Bacon ameandika vitabu kadhaa kikiwemo kile cha New Atlantis. Msomi huyo wa Uingereza alifariki dunia mwaka 1626.
Miaka 249 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa Andre Marie Ampere, mtaalamu wa hisabati na fizikia wa Ufaransa.
Akiwa kijana mdogo alipendelea sana fani ya hesabati. Akiwa Chuo Kikuu cha Polytechnique cha mjini Paris, aligundua mambo kadhaa katika uga wa fizikia. Moja ya mambo aliyoyagundua Andre Marie Ampere ni pamoja na simu ya upepo "Telegrafu." Mtaalamu huyo alifariki dunia mwaka 1836.
Siku kama ya leo miaka 123 iliyopita, alifariki dunia Alexandrina Victoria, malkia maarufu wa Uingereza akiwa na umri wa miaka 82. Victoria alizaliwa mjini London mwaka 1819 Miladia, huku akichukua nafasi ya William IV kiutawala ambapo alisalia katika madaraka kwa kipindi cha miaka 64.
Katika utawala wa Alexandrina Victoria, kulishtadi ukandamizaji dhidi ya raia wa nchi hiyo. Kufariki dunia malikia huyo ilikuwa mwanzo wa kudhoofika utawala wa kifalme ambapo baada yake aliingia madarakani Edward VII.
Miaka 45 iliyopita katika siku inayosadifiana na hii ya leo, ikiwa ni katika mwendelezo wa wananchi Waislamu wa Iran kupinga utawala wa Shah na kukabiliana na wanajeshi wa utawala huo, idadi kubwa ya raia waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa.
Wananchi wa Iran ya Kiislamu wambao walikuwa wakisubiri kwa hamu kubwa kurejea nchini Imam Khomeini (M.A) walitayarisha mazingira hitajika kwa ajili ya mapokezi makubwa zaidi ya kihisitoria kwa kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Kwa mnasaba huo, wafanyakazi mbalimbali wakiwemo maulamaa na wawakilishi wa matabaka mbalimbali ya wakazi wa mji wa Tehran walikusanyika pamoja ili kuandaa hafla kubwa ya kumpokea Imam.
Watu wengi kutoka katika miji na vijiji vya Iran ya Kiislamu walimiminika kwa wingi mjini Tehran kwa lengo la kushiriki katika sherehe za kumkaribisha Imam Khomeini (M.A).
Katika upande mwingine, baada ya maandamano makubwa ya wananchi, wanajeshi elfu nne wa jeshi la anga pia waligoma kula wakitaka kuondoka Iran washauri wa kijeshi wa Marekani katika kuwaunga mkono wananchi wanapambano wa Iran.